Mangungu: Tunamalizana na Al Ahly, kisha atafuata Yanga

SIKU 15 tu tangu achaguliwe kwa kishindo katika Uchaguzi mdogo wa Simba, Mwenyekiti mpya, Murtaza Mangungu amenza rasmi kazi na kuchimba mkwara wanamalizana kwanza na Al Ahly kisha atawageukia Yanga waliopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ili kutetea taji lao.

Mangungu amesema ameanza kazi yake kwa kudili na wanachama ikiwa ni wiki kama mbili tu tangu wanachama walipomchagua kwa kura nyingi dhidi ya mpinzani wake, Juma Nkamia, uchaguzi uliofanyika Februari 7.

Mwanaspoti ilifanya mahojiano na Mangungu kabla ya kuchaguliwa na kueleza mikakati yake baada ya kupata nafasi hiyo na kufichua yeye na wenzake wanavyoipigia hesabu mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mwarabu kisha kukomalia mechi za Ligi Kuu ili kubeba ndoo kwa mara ya nne mfululizo. Ebu msikie anachokisema...! Endelea naye


UMOJA NA MIPANGO

Mangungu anaamini umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, hivyo ameamua kuanza na Wanasimba kukutana nao na kubadilishana mawazo ili azidi kujifunza zaidi na kuyafanyia kazi mambo mbalimbali.

Anasema, bila ya kuwa na umoja kufanikiwa ni ngumu hivyo ameanza na matawi ya Simba hapa Dar es Salaam na baadae atazunguka Nchi nzima.

“Simba imetapakaa nchi nzima, hivyo kama kiongozi ni wajibu wangu kuhakikisha nakutana na Wanasimba kote waliko kwa wakati tofauti tofauti japokuwa sio kwa wakati mmoja lakini nitafanya hivyo,” anasema Mangungu ikiwa ni moja ya ajenda katika ilani yake.


MICHUANO YA FA

Simba ni bingwa mtetezi katika michuano ya Kombe la FA, Mangungu anaamini kwa ubora wa kikosi chake timu hiyo itatetea ubingwa huo. Ikumbukwe michuano hii katika hatua za juu itatakiwa kupigwa katika viwanja tofauti na timu hizo zinavyovitumia.

“Naona ni utaratibu mzuri sana, mpira sio kuingiza tu mapato hata kujenga tu burudani inapendeza,”

“Ninachowaomba TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wawasiliane na uongozi wa mikoa wahakikishe viwanja vinafanyiwa maandalizi mazuri viwe katika ubora wa kutumika ila Simba ina wachezaji wengi wazuri hatuwezi kuwapeleka kucheza kwenye mahandaki.”

Anatolea mfano Simba wakienda Songea au Tabora inakuwa ni fursa kwa Wanasimba kujionea timu yao mpira unatakiwa kuchezwa sehemu yoyote ile na Simba wako tayari.


MECHI NA AL AHLY

Februari 21, Jumapili mwaka huu Simba inashuka dimbani kucheza na Mabingwa wa Afrika, Al Ahly mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam huku wakiwa na imani ya kupata pointi tatu kwa mikakati na mipango iliyopo na iliyokwishafanyika ili kuzidi kujiweka nafasi nzuri zaidi.

“Sio Al Ahly tu Simba iko vizuri na kikosi ni kizuri ndicho kinachonifanya nitambe na nijivunie, tumeshinda kwao AS Vita na huyu hapa nyumbani tuna imani tutashinda cha muhimu ni umoja.”


VYANZO VYA MAPATO

Katika ilani yake ya uchaguzi ilikuwa ni moja ya ajenda, ambayo anakiri ataiwasilisha katika vikao vya Bodi ya Wakurugenzi ili waweze kudadavua zaidi.

“Tutahakikisha katika vikao vyetu vya Bodi tunatizama vyanzo vya mapato na tunavisimamia kama nilivyosema hapo awali Simba ina rasilimali watu,”

“Simba ina vitu vingi sana, hata suala la jezi kuwa holela sio kabisa, unaweza kwenda huku unakuta jezi inauzwa Sh7000 ukaenda kwingine kama hiyo hiyo inauzwa 9000 sio sawa jezi ya klabu haiwezi kuwa na gharama holela kama hizo,”


WATANI ZAO YANGA

Mangungu ana imani utani kwa timu hizo, lakini amewataka wakae mkao wa kula kuwapisha katika nafasi hiyo waliopo hivi sasa ambapo Yanga ndiyo wanaongoza ligi wakiwa na pointi 46 wakiwa wamecheza mechi 20 wakati Simba wana pointi 42 na mechi 18.

“Kwanza mpira hauchezwi na maneno unachezwa uwanjani hivyo basi hiyo tofauti ya pointi tutazipata kutoka kwao acha waongee lakini pale kileleni wapo kwa muda tu,” anasema Mangungu.


SIRI YA MAFANIKIO

“Simba ina timu nzuri muunganiko mzuri hiyo ni silaha kubwa inayotufanya tutambe, ni ngumu kuwa na timu mbovu ukawafunga AS Vita kwao hivyo mpira ni maandalizi na usajili mzuri ndio matunda yake.”

Kwa namna ya umoja uliopo ndani ya timu hiyo Mangungu anaamini hakuna litakaloshindikana.


KUHUSU SH 20 BILIONI

Licha ya Simba kufanikiwa kuingia katika mfumo mpya wa uwekezaji lakini mpaka sasa mfumo huo haujakamilika ili kumpa nafasi Mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’ kuweka fedha hizo.

“Tukikamilisha mchakato wa mabadiliko mzigo utaingia mwekezaji yuko tayari sema bado utaratibu haujakamilika, tuko kwenye majadiliano na vikao vinaendelea. Nimevikuta na tunaendea tukikamilisha tu anaweka pesa, hajawahi hata kukataa ni jambo la muda tu,” anasema


BARBARA KIBOKO

Kwa utendaji kazi wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez hakuna anayeweza kupinga namna ambavyo mwanadada huyo anajituma kuhakikisha Simba inazidi kupiga hatua zaidi.

Mangungu anasema, Barbara ni mtu tofauti na msikivu katika kuhakikisha jambo linaenda sawa, hivyo kwa kushirikiana wataifanyia Simba makubwa.

“Barbara huyu mtu kwanza ni msikivu, msomi mzuri sana huyu binti, hata kama kuna jambo anafanya kimakosa kutokana na usikivu wake analifanya kwa usahihi yuko vizuri sana.”


NIDHAMU KWA TIMU

Kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa na utovu wa nidhamu unaopelekea kusimamishwa mfano hivi karibuni Jonas Mkude alikumbana na adhabu huku kurejeshwa kwake kundini kukizua maswali mengi sana kwa Wanasimba. Mangungu anasema, katika maisha ya kila siku nidhamu ni jambo kubwa na la kheri hivyo kwa mchezaji asipokuwa nayo ni ngumu kufanya vizuri.

“Wachezaji hawawezi kufanya vizuri kama hawana nidhamu, kila mchezaji anatakiwa kuzingatia suala hilo, sio wachezaji tu nidhamu mpaka kwa mashabiki pia, hata waandishi mnatakiwa kuwa na nidhamu na sio wachezaji peke yao,” anasisitiza.

Anasitiza kuwa, mpaka sasa tayari kafanya makubwa kwa klabu hiyo mara tu baada ya kuchaguliwa ambayo hawezi kuyaweka wazi kutokana na mengine kuwa ya ndani zaidi.