Man United inajitafuta; Ten Hag anaponea wapi?- Sehemu ya pili

Muktasari:
- Kauli hiyo iliwafanya mabosi wa Man United kufikiria shida ya timu hiyo kufanya ovyo haiishii kwenye benchi la ufundi peke yake, kwa maana ya mabadiliko waliyofanya mara nyingi kuajiri na kufuta kazi, bali kuamini kwa kocha mmoja na kuhakikisha anapewa sapoti kwenye usajili wa wachezaji wanaofaa kuingia kwenye kikosi.
MANCHESTER, ENGLAND: APRILI 2022, aliyekuwa kocha wa muda wa Manchester United, Ralf Rangnick alisema timu hiyo inahitaji juhudi za makusudi, kukifanyia maboresho makubwa kikosi hicho ili kuondoa tatizo ambalo limeonekana kuota mizizi na kuonekana kawaida.
Kauli hiyo iliwafanya mabosi wa Man United kufikiria shida ya timu hiyo kufanya ovyo haiishii kwenye benchi la ufundi peke yake, kwa maana ya mabadiliko waliyofanya mara nyingi kuajiri na kufuta kazi, bali kuamini kwa kocha mmoja na kuhakikisha anapewa sapoti kwenye usajili wa wachezaji wanaofaa kuingia kwenye kikosi.
Pengine hilo ndilo lililomfanya kocha wa sasa wa kikosi hicho, Erik ten Hag kuendelea kuvumiliwa na kubaki kwenye timu hiyo licha ya kufanya ovyo msimu uliopita, timu ilipomaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Kwa sababu kama ni ubora, Ten Hag bado hajavuka rekodi za Mourinho, ambaye alifunguliwa mlango wa kutokea.
Lakini, kuna eneo ambalo Ten Hag amewazidi watangulizi wake kwenye kiti cha moto za kuinoa Man United tangu Sir Alex Ferguson alipong’atuka. Huu ni msimu wa tatu kwa Mdachi huyo kufanya kazi kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, lakini misimu yote miwili iliyopita pamoja na ugumu wote, lakini timu hiyo haijamaliza msimu mikono mitupu.
Kwenye msimu wake wa kwanza aliipa Man United taji la Kombe la Ligi na msimu wa pili aliisaidia kunyakua Kombe la FA na hivyo kuwamo kwenye michuano ya Ulaya msimu huu, Europa League.
Tofauti na hilo, takwimu za uwanjani zinaonyesha Ten Hag timu yake ina wastani wa kushinda pointi 1.92 kwa kila mechi, akizidiwa na Mourinho pointi 1.97 – lakini amewazidi Louis van Gaal (1.81), Ole Gunnar Solskjaer (1.79), David Moyes (1.73) na Ralf Rangnick (1.45).
Hilo linampa pointi kubwa Ten Hag kwa maana ya makocha wote waliokuja Man United baada ya Ferguson, ukimwondoa Mourinho, ambaye ni kocha mkubwa kwenye mchezo wa soka, yeye ndiye mwenye rekodi zinazobeba matumaini na kuamini endapo kama atapewa wachezaji anaowataka na kupewa muda zaidi, kuna kitu atakifanya.
Takwimu za Ten Hag kwa misimu miwili ya kwanza zinadaiwa zipo juu kuliko hata kwa Mikel Arteta kwenye miaka yake miwili ya kwanza huko Arsenal na Jurgen Klopp kwenye miaka yake miwili ya kwanza huko Liverpool. Makocha hao, Arteta na Klopp walivumiliwa na timu zao hadi kwenye msimu wa tano kuanza kuonyesha kitu cha maana ndani ya uwanja.
Baada ya Ferguson kuondoka, Ten Hag ameonyesha matumaini mengine ya kushika namba mbili kwenye wastani wa ushindi wa mechi alizoongoza timu hiyo, akiwa nyuma ya Mourinho mwenye wastani wa 58.33%. Ten Hag ana wastani wa 57.89%, wakati Ole Gunnar Solskjaer alikuwa na wastani wa 54.17%, David Moyes (52.94%), Louis van Gaal (52.43%) na Ralf Rangnick (37.93%)
Tajiri mpya wa Man United, Sir Jim Ratcliffe, ameampa muda Ten Hag wa kuendelea kuleta mabadiliko kwenye timu hiyo na ndiyo maana anamsapoti kwenye usajili wa kunasa mastaa wapya. Kwenye ishu ya usajili, Ole Gunnar Solskjaer alipewa pesa nyingi zaidi, Pauni 441 milioni, lakini Erik ten Hag anaelekea huko, ambapo imedaiwa hadi sasa ameshatumia Pauni 411 milioni na bila shaka kwenye dirisha la Januari mwakani ataingia tena sokoni kuongeza watu wapya kwenye kikosi chake. Jose Mourinho alisapotiwa Pauni 392 milioni za usajili, Louis van Gaal (Pauni 259 milioni) na David Moyes (Pauni 65 milioni), ambaye alikuwa kocha wa kwanza kuchukua kijiti kutoka kwa Sir Alex.
Usiku wa jana Jumatano, Man United ilirusha kete yake ya kwanza kwenye Europa League, ilipomenyana na FC Twente, bila shaka, kocha Ten Hag atapambana kuboresha rekodi zake za ushindi katika kikosi hicho ili kujiweka pazuri zaidi.
Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kabla ya mechi hiyo ya usiku wa jana, Man United imecheza mechi sita, tano kwenye ligi na moja kwenye Kombe la Ligi. Matokeo ya kwenye ligi, imeshinda mbili, sare moja na kipigo kimoja, huku kwenye Kombe la Ligi ilipata ushindi wa kishindo mbele ya Barnsley, 7-0.
Rekodi za makocha wote waliopita Man United baada ya Ferguson kung’atuka, Moyes aliongeza timu hiyo kwenye mechi 51, ameshinda 27, sare tisa na vichapo 15.
Louis Van Gaal alioongoza kwenye mechi 103, alishinda 54, sare 25 na vipigo 24, wakati Mourinho alikaa benchi kwenye mechi 144, akishinda 84, sare 32 na vipigo 28.
Ole Gunnar Solskjaer, aliyekuwa kipenzi cha mastaa wa zamani wa timu hiyo hasa wale wa Class Of 92, aliongoza timu hiyo kwenye mechi 167, akishinda 91, sare 37 na vichapo 39.
Ralf Rangnick aliisimamia Man United kwenye mechi 29, ameshinda 11, sare 10 na vichapo 10, huku Ten Hag kabla ya msimu huu kuanza, aliisimamia timu hiyo kwenye mechi 114, ameshinda 66, sare 17 na vichapo 31. Rekodi hizo zinaishia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA, kabla ya kupoteza kwenye Ngao ya Jamii na mechi nyingine zilizoendelea kwenye msimu huu wa 2024-25.
Je, Ten Hag atawashinda wapinzani wake Arteta na Pep Guardiola kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kwa aina ya wachezaji anaowasajili kwenye kikosi hicho cha Old Trafford? Itaendelea…