Mambo haya yanasubiriwa Ligi Kuu Bara

Muktasari:
- Ligi hiyo iliyopanda chati ya ubora hadi nafasi ya nne kutoka ya sita barani Afrika na pia kushika namba 57 duniani kwa mwaka 2024 (kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la historia na takwimu za Mpira wa Miguu duniani - IFFHS), inarindima kuanzia Februari Mosi kwa ile michezo ya viporo.
LIGI Kuu Bara inarejea tena baada ya kusimama kwa takribani mwezi mmoja kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyokuwa inafanyika visiwani Zanzibar, ambapo kwa sasa inasubiriwa kuona ni kitu gani kitatokea kutokana na ushindani uliokuwapo.
Ligi hiyo iliyopanda chati ya ubora hadi nafasi ya nne kutoka ya sita barani Afrika na pia kushika namba 57 duniani kwa mwaka 2024 (kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la historia na takwimu za Mpira wa Miguu duniani - IFFHS), inarindima kuanzia Februari Mosi kwa ile michezo ya viporo.
Sasa wakati ligi hiyo iliyopanda kwa nafasi mbili na kuzipiku za Afrika Kusini na Tunisia ikirejea, Mwanaspoti linakuletea makala ya kinachosubiriwa kutokea kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo tangu mwanzo.

MOTO WA SIMBA
Simba inayoongoza Ligi na pointi zake 40, mbele ya Yanga yenye 39, itakuwa na kibarua cha kuhakikisha inaendelea kushika usukani katika msimamo kutokana na kukabiliwa na ratiba ngumu, kwa sababu ndani ya wiki tatu tu itacheza michezo sita.
Simba itaanza kushuka kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora Februari 2, kucheza dhidi ya Tabora United ambayo mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam, Wekundu wa Msimbazi walishinda mabao 3-0, Agosti 18, mwaka jana.
Baada ya hapo itasafiri hadi Babati mkoani Manyara kucheza dhidi ya Fountain Gate Februari 6, ambayo pia mchezo wa raundi ya kwanza jijini Dar es Salaam iliikanda mabao 4-0, Agosti 25, mwaka jana, kisha kuwakaribisha maafande wa Tanzania Prisons.
Mchezo huo na Prisons utapigwa Februari 11, ambapo Simba mechi ya kwanza ilishinda bao 1-0, Oktoba 22, mwaka jana, kisha baada ya hapo Mnyama ataialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC Complex, ambayo aliichapa pia bao 1-0, Septemba 29, mwaka jana.
Kituo kinachofuata kwa Mnyama kitakuwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Ruangwa kucheza na Namungo FC Februari 19, huku mechi ya kwanza zilipokutana Simba ilishinda mabao 3-0, Oktoba 25, mwaka jana, kisha kurejea Dar es Salaam kucheza na Azam FC.
Mchezo huo ambao hutambulika kama ‘Dabi ya Mzizima’, utapigwa Februari 24, ambapo timu hizo zitakutana huku Simba ikiwa na rekodi nzuri kwani mechi ya mwisho zilipokutana ilishinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar Septemba 26, mwaka jana.
Simba ilishinda mechi zote sita za awali dhidi ya timu itakazokutana nazo kuanzia Februari 2, huku ikijiwekea rekodi tamu ya kufunga jumla ya mabao 14, huku ikiwa haijaruhusu bao lolote kwenye nyavu zake kutikiswa jambo linaloipa nguvu zaidi.

YANGA KATIKATI YA MTEGO
Baada ya Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, mashabiki wa timu hiyo kwa sasa watahitaji kuona kile ambacho itakifanya katika Ligi Kuu Bara, hasa kutetea ubingwa wake ambao imeuchukua kwa mara tatu mfululizo.
Yanga ambao ni mabingwa mara 30 wa Ligi Kuu Bara, wana nafasi ya kurejea kileleni na kuishusha Simba endapo itashinda mchezo wake na Kagera Sugar utakaopigwa Februari Mosi, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 2-0, zilipokutana Agosti 29, 2024 kule Kaitaba.
Kikosi hicho cha kocha Saed Ramovic kitaendelea kusalia jijini Dar es Salaam kucheza na KenGold Februari 5, ambayo iko mkiani na pointi sita, huku mchezo wao wa kwanza uliopigwa jijini Mbeya, Yanga ilishinda kwa bao 1-0, Septemba 25, 2024.
Februari 10, Yanga itakuwa na kibarua cha kupambana na maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo Mbweni, ambako mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, timu ya wananchi ilishinda kwa mabao 2-0, Oktoba 22, 2024.
Mchezo huo hautokuwa rahisi kwa Yanga kutokana na ugumu ambao JKT imekuwa nao inapocheza Meja Isamuhyo kwani timu hiyo inayonolewa na kocha, Ahmad Ally haijapoteza mechi yoyote nyumbani msimu huu, ikishinda tatu na kutoka sare nne.
Februari 14 itacheza na KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge ambako mzunguko wa kwanza zilipokutana Yanga ilishinda bao 1-0, Septemba 29, 2024, wakati huo KMC ikiwa chini ya kocha, Abdihamid Moallin ambaye sasa ametua ndani ya kikosi hicho cha Jangwani.
Baada ya hapo itaialika Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne na pointi zake 33, ambapo mchezo wa mzunguko wa kwanza zilipokutana Yanga ilishinda kwa bao 1-0, la Pacome Zouzoua, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar Oktoba 30, 2024.
Februari 23 itakuwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma kucheza na Mashujaa FC, ambapo mchezo wa kwanza ilishinda mabao 3-2, Desemba 19, 2024, huku shujaa akiwa ni mshambuliaji, Prince Dube aliyefunga ‘hat-trick’ pekee iliyofungwa katika ligi hiyo hadi sasa msimu huu.
Kituo kinachofuata kwa Yanga kitakuwa ni jijini Mwanza kuifuata Pamba Jiji Februari 28 ambapo mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Oktoba 3, 2024, ilishinda mabao 4-0 na kuhitimisha mwezi huo kabla ya kukutana na Simba Machi 8.

MSERBIA KUIOKOA KENGOLD?
Moja ya jambo yanayosubiriwa pia kwa hamu ni kuona ni kwa jinsi gani kocha mkuu mpya wa KenGold, Mserbia Vladislav Heric ataweza kukiokoa kikosi hicho na janga la kushuka daraja, baada ya mwenendo mbaya tangu Ligi Kuu Bara imeanza msimu huu.
Kikosi hicho kilichoanza msimu na kocha mkuu, Fikiri Elias na kujiuzulu mwenyewe kutokana na mwenendo mbaya Septemba 17, 2024, kisha kukabidhiwa mikoba hiyo Omary Kapilima, kinaburuza mkiani na pointi sita baada ya kucheza michezo yake 16.
Ujio wa Heric huku viongozi wakifanya usajili mkubwa wakiwamo mastaa waliowahi kutamba na Yanga na Simba kama, Bernard Morrison, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani na Zawadi Mauya, ni jambo linalosubiriwa kuona ni jinsi gani wataiokoa timu hiyo.
Kocha huyo aliyejiunga na KenGold Januari 18 mwaka huu, amewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwamo za Club Africain ya Tunisia, Maritzburg United, Polokwane City na FC Cape Town za Afrika ya Kusini, jambo lililowavutia mabosi kumuajiri.
Kocha huyo aliyezaliwa Agosti 29, 1966, ameifundisha pia Chippa United ya Afrika Kusini, ambapo alianzia kucheza mwaka 1976 akiwa na Akademi ya FK Vojvodina kisha soka la kulipwa alizichezea FK Proleter Novi Sad na FK Fruskogorac Novi Sad.
Heric ambaye ni mzoefu wa mpira wa miguu akiwa na shahada aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Novi Sad huko kwao Serbia huku akipata leseni ya UEFA ‘A’, anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa yatakayoinusuru timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa msimu huu.

MATANO NA FOUNTAIN GATE
Moja ya kocha ambaye ataangaliwa kwa jicho la kipekee kutokana na wasifu wake (CV) ni Mkenya Robert Matano wa Fountain Gate aliyeteuliwa kuiongoza timu hiyo Januari 10, mwaka huu akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Mohamed Muya.
Kocha huyo anayefahamika kwa jina la utani la ‘Special One’, alikuwa akiifundisha Sofapaka msimu huu, baada ya mkataba wake na Tusker FC aliyoingoza kwa miaka sita kuanzia mwaka 2018, kuisha na kutwaa ubingwa wa Kenya msimu wa 2021-2022.
Matano aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwamo za AFC Leopards na Ulinzi Stars, ameiongoza Sofapaka katika jumla ya michezo 15, ya Ligi ya Kenya huku akishinda mitano, sare sita na kupoteza minne akiiacha katika nafasi ya saba na pointi 21.
Katika kipindi chake cha ukocha kocha huyo, amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mara nne akifanya hivyo na Sofapaka FC mwaka 2009 ambayo ameshaachana nayo msimu huu na Tusker FC kuanzia msimu wa 2012, 2020-2021, na 2021-2022.
Matano amekabidhiwa kikosi hicho baada ya Muya kutimuliwa Desemba 29, mwaka jana huku akitazamiwa ni jambo gani kubwa atakalolifanya katika Ligi Kuu Bara msimu huu, kutokana na kile alichokifanya wakati akiwa na timu mbalimbali za Kenya.

MAKALI YA NYUKI WA TABORA
Wakati Simba ikisubiriwa kukutana na Tabora United Februari 2, moja ya mambo yanayosubiriwa ni kuona kama kikosi hicho cha ‘Nyuki wa Tabora’ kitaendeleza ubabe kwa vigogo, licha ya mechi yake ya kwanza kuchapwa mabao 3-0, Agosti 18, 2024.
Kikosi hicho kinachonolewa na Mkongomani Anicet Kiazayidi, kimekuwa tishio kabla ya Ligi kusimama ambapo kilianza kwa kuichapa Yanga mabao 3-1, Novemba 7, 2024 na kumfanya aliyekuwa kocha wake, Miguel Gamondi kutimuliwa Novemba 15, 2024.
Pia ikaichapa Azam FC mabao 2-1, Desemba 13, 2024 na kuifanya kufikisha jumla ya michezo saba mfululizo bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 4-2 ugenini kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo na maafande wa JKT Tanzania Oktoba 18, 2024.
Kiwango bora ambacho imekuwa nacho ndicho kinachosubiriwa kuona kama timu hiyo itakuwa na mwendelezo pia mzuri na kuzidi kutishia vigogo katika mzunguko huu wa pili, hususani kulipiza kisasi kwa Simba wakati zitakapokutana tena Februari 2.
VITA YA ‘TOP FOUR’
Mbali na Simba na Yanga zilizopo nafasi ya kwanza na ya pili, timu nyingine zinazosubiriwa kama zitakoleza vita ya ‘Top Four’ ni Azam FC iliyopo ya tatu na pointi 34 na Singida Black Stars inayoshika nafasi ya nne kwa pointi zake 33.
Azam FC inayonolewa na kocha, Rachid Taoussi, imekuwa katika kiwango bora tangu ateuliwe kukiongoza Septemba 7, 2024, akichukua nafasi ya Msenegali Yousouph Dabo aliyetimuliwa Septemba 3, 2024 na kujiunga na AS Vita Club ya DR Congo.
Kocha huyo ameiongoza Azam FC katika michezo 15 ya Ligi Kuu Bara, akishinda 11, sare miwili na kupoteza pia miwili, ila kiujumla imecheza 16, ikishinda 11, sare mitatu na kupoteza miwili, ikifunga jumla ya mabao 25 na kuruhusu manane tu.
Kwa upande wa Singida inaingia ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya kocha mkuu, Miloud Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, aliyechukua nafasi iliyoachwa wazi na Mbelgiji Patrick Aussems aliyeondoka Novemba 29, mwaka jana.
Hamdi aliyezaliwa Juni Mosi, 1971, huku akipenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 katika timu mbalimbali alizofundisha, alikuwa hana timu yoyote tangu alipoachana na Al-Khaldiya FC ya Bahrain, aliyoifundisha Julai Mosi, 2023 hadi Desemba 13, 2023.
Kocha huyo mbali na kuifundisha Al-Khaldiya FC, timu nyingine alizowahi kuzifundisha ni USM Alger na JS Kabylie za kwao Algeria, Al-Salmiya ya Kuwait, Athletico Marseille na ES Vitrolles za Ufaransa na Al-Ettifaq FC (U-23) kutoka Saudi Arabia.
Kwa sasa anasubiriwa kuona kile atakachokifanya katika kikosi hicho ambacho kimesheheni lundo la wachezaji wazuri, huku viongozi wa klabu hiyo wakiweka wazi moja ya malengo yao makubwa ni kuleta ushindani na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

WACHEZAJI WA KUTAZAMWA
Katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu, wapo wachezaji wengi bora ambao watatazamwa kwa kile watakachokifanya kwenye timu zao, akiwamo aliyekuwa mshambuliaji wa AS Vita Club, Jonathan Ikangalombo aliyejiunga na Yanga.
Nyota huyo anayeweza pia kutokea pembeni kwa maana ya kucheza winga, anatazamwa ni kwa jinsi gani anaweza kuingia katika kikosi cha kwanza, huku akikumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa mastaa wengine kikosini kama, Prince Dube na Clement Mzize.
Wengine ni kiungo mshambuliaji, Bernard Morrison aliyetamba na miamba wa soka nchini Yanga na Simba ambaye amejiunga na KenGold, huku akitazamiwa ataisaidia vipi timu hiyo kukwepa janga la kushuka daraja ili isirudi tena huko Championship.
Mshambuliaji mpya wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah aliyejiunga na timu hiyo akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, ni miongoni mwa nyota watakaotazamwa, huku msimu uliopita akiingiza vitani Yanga wakati akiichezea Medeama ya kwao Ghana.
Amara Bagayoko aliyetua Coastal Union akitokea ASKO de Kara ya Togo alikoibuka mfungaji bora na mabao 19, anatazamiwa kuleta mageuzi ndani ya timu hiyo baada ya kuzichezea, FC Nouadhibou ya Mauritania, Al-Hala SC ya Bahrain na Djoliba AC ya Mali.
KAULI ZA MAKOCHA
Kocha wa KenGold, Heric amesema licha ya presha kubwa iliyopo na muda mchache aliojiunga na timu hiyo ila ataendelea kukisuka vyema kikosi hicho, huku akiamini usajili uliofanyika dirisha dogo utaleta matokeo chanya, wakati kocha wa Fountain Gate, Roberto Matano amesema anahitaji muda, lakini tayari anatengeneza mifumo ya kiuchezaji.
Kwa upande wa kocha wa Singida Black Stars, Hamdi amesema kitu anachojivunia tangu amejiunga na kikosi hicho ni kitendo cha wachezaji kufuata maelekezo yake vizuri, huku akijivunia ushirikiano mkubwa anaoendelea kuupata kikosini.