Makocha 24 wenye msala wa kusaka ubingwa Euro 2020

Muktasari:
KITU cha Euro 2020 kinaanza rasmi leo Ijumaa.
LONDON, ENGLAND. KITU cha Euro 2020 kinaanza rasmi leo Ijumaa.
Hamu ya mashabiki kusubiri michuano hiyo sasa itafika mwisho na sasa watashuhudia vipute rasmi ambapo timu 24 zitashuka kwenye viwanja vya miji 11 kusaka ubingwa huo wa Ulaya.
Lakini, unajua makocha waliopewa msala huo wa kusaka ubingwa wa Ulaya kwenye michuano hiyo iliyochelewa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la corona?
Hawa hapa ni makocha 24 waliopewa majukumu ya kuzibeba timu za taifa kwenye michuano hiyo na rekodi zao za mafanikio walipokuwa wachezaji.
24. Denmark -
Kasper Hjulmand
Hjulmand alilazimika kujiuziulu akiwa na miaka 26 tu baada ya kusumbuliwa na majeraha ya goti, hivyo hakuwa na wakati mzuri kabisa wa kucheza soka la kulipwa na kufanikiwa. Ameondoka kwenye uchachezaji mapema, lakini kwa sasa anaonyesha ubora wake kwenye soka akiwa kocha.
23. Sweden -
Janne Andersson
Straika huyo wa zamani wa Sweden hakuwa na maisha marefu ya soka lake alipokuwa mchezaji, ambapo alizichezea timu za chini sana nchini humo, Alets IK na IS Halmia. Sweden inakwenda kwenye mikikimikiki ya Euro 2020 ikiwa na matumaini kibao kutoka kwa kocha Andersson.
22. Slovakia -
Stefan Tarkovic
Kuna taarifa chache sana za kuhusu taarifa za Tarkovic alipokuwa mchezaji, ambapo alitamba akiwa na kikosi cha Tatran Presov. Beki huyo wa kushoto anatajwa kwamba alionyesha kiwango bora cha soka lake alipokuwa mchezaji japo kwa uchache huo huo wa taarifa zake.
21.North Macedonia - Igor Angelovski
Angelovski alitamba kwenye Ligi Daraja la Kwanza Slovenia, akiwa kwenye kikosi cha Publikum Celje kati ya mwaka 1998 na 2000. Alishinda ubingwa wa Kombe la Macedonia mwaka 2003 alipokuwa na kikosi cha Cementarnica. Igor atakuwa na majukumu ya kuiongoza North Macedonia kwenye Euro 2020.
20. Uswisi -
Vladimir Petkovic
Kiungo huyo mzaliwa wa Sarajevo alitumikia muda mwingi wa soka lake nchini Uswisi, alikokwenda kuzitumikia klabu za Chur 97, Bellinzona na Locarno. Uswisi wanaamini katika uwezo wake na kumpa majukumu hayo ya kuiongoza timu yao kwenye mikikimikiki ya Euro 2020.
19. Croatia -
Zlatko Dalic
Alitumia muda mwingi akiwa mchezaji kwa ndani ya Croatia, lakini si kwenye klabu kubwa. Hajawahi pia kuitumikia timu ya taifa, lakini kwa sasa amepewa majukumu ya kuinoa timu ya taifa, tena yenye mastaa kibao akiwamo mshindi wa Ballon d’Or, Luka Modric.
18. Czech Republic -
Jaroslav Silhavy
Beki huyo wa zamani wa RH Cheb nchini Czechoslovakia kwa miaka 10, alicheza karibu mechi 250 kwenye ligi ya nchi hiyo. Kwenye soka la kimataifa, Slhavy, alipata nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo mara nne. Atakwenda Euro 2020 kuhakikisha Jamhuri ya Czech inafanya vizuri.
17. Finland -
Markku Kanerva
Beki huyo alitumikia muda mwingi kuichezea HJK Helsinki, alishinda ubingwa wa Finland mara tano. Kanerva aliitumikia timu ya taifa ya Finland mara 59, kati ya miaka 1986 na 1995. Kwa kipindi hicho alipokuwa mchezaji Kanerva alikuwa na mafanikio makubwa ndani ya uwanja.
16. Ubelgiji -
Roberto Martinez
Ametumikia muda mwingi wa wakati wake alipokuwa mchezaji kwenye kikosi cha Wigan na aliichezea pia Swansea. Hajawahi kuitumikia Hispania. Kipindi chake cha ukocha mafanikio yake yamezidi yale aliyopata wakati alipokuwa mchezaji.
15. Ujerumani - Joachim Low
Low kwenye maisha yake akiwa mchezaji, hakuwa na mbwembwe nyingi na kitu kinachokumbukwa kuhusu yeye ni wakati alipoichezea SC Freiburg kwa nyakati tatu tofauti. Lakini, amekuwa na mafanikio ya kimtindo tangu alipoanza kupewa majukumu ya kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani.
14. Ureno -
Fernando Santos
Santos alicheza nchini Ureno katika maisha yake yote ya soka akiwa mchezaji, ambapo alitamba na timu za Estoril na Maritimo na hakuwahi kuitwa kuitumikia timu yake ya taifa ya Ureno. Lakini, ndiye kocha wa Ureno kwa sasa, ambaye aliwapa ubingwa wa Kombe la Ulaya miaka mitano iliyopita.
13. Hungary -
Marco Rossi
Mtaliano huyo alicheza kwa mafanikio kwenye Serie A akizitumikia Brescia na Sampdoria. Mambo yake yalikuwa mazuri zaidi Sampdoria, wakati aliposhinda ubingwa wa Coppa Italia katika msimu wa 1993/94. Marco Rossi atakuwa kwenye mikikimikiki ya Euro 2020 akiwa na jukumu la kuipa ubingwa Hungary.
12. Austria -
Franco Foda
Anakumbukwa zaidi kwa nyakati zake alizokuwa kwenye klabu ya Bayer Leverkusen na FC Kaiserslautern, ambako kote huko alishinda taji la DFB-Pokal. Kwa upande wa timu ya taifa, Foda alikuwa mchezaji hakufurahia sana soka la kimataifa baada ya kuitumikia Ujerumani Magharibi mara mbili tu.
11. Russia - Stanislav Cherchesov
Kipa wa zamani aliyecheza klabu kibao za Russia ikiwamo Spartak Moscow na alikwenda kutamba pia Austria kwenye kikosi cha Tirol Innsbruck. Ameshinda mataji saba ya ubingwa wa ligi katika klabu hizo mbili. Aliichezea Soviet Union mara nane na timu ya taifa ya Russia mara 39.
10. Scotland -
Steve Clarke
Clarke aliitumikia kwa miaka mitano St Mirren kabla ya kwenda kutamba kwa miaka 11 huko Chelsea, alikocheza mechi 330 za Ligi Kuu kati ya mwaka 1987 na 1998. Licha ya jambo hilo, lakini Clarke aliitumikia Scotland mara sita tu kwenye soka la kimataifa akiwa mchezaji.
9.Wales - Rob Page
Nafasi hii ingemhusu Ryan Giggs na bila ya shaka angekuwa kocha mwenye mafanikio makubwa. Lakini, Wales kwa sasa ipo chini ya kocha Page, ambaye alicheza kwenye timu za Watford, Sheffield United na Coventry kwenye Ligi Kuu England. Timu yake ya taifa aliichezea mara 41.
8. Uturuki -
Senol Gunes
Gunes alikuwa kipa hodari, ambapo aliichezea Trabzonspor kwa miaka 15, ameshinda mataji sita ya Ligi Kuu Uturuki na makombe matatu ya Uturuki. Kwenye soka la kimataifa, Gunes alikuwa kwenye goli la miamba hiyo mara 31.
7. England -
Gareth Southgate
Kitu kinachokumbukwa zaidi ni tukio lake la kukosa penalti Euro ’96, lakini maisha yake ya soka la klabu amecheza kwenye Ligi Kuu England, akitamba Crystal Palace, Aston Villa na Middlesbrough. Aliichezea pia timu ya taifa ya England mara 57.
6. Italia - Roberto Mancini
Ni gwiji wa Sampdoria baada ya kucheza mechi 424 za ligi na kufunga mabao 132 katika miaka 15 aliyodumu na timu hiyo. Alibeba Serie A akiwa na miamba hiyo huku akiwahi pia kuitumikia Lazio. Ameshinda Coppa Italia mara sita na kombe la washindi mara mbili. Ni mchezaji bora wa Serie A mwaka 1997.
5. Poland -
Paulo Sousa
Benfica, Sporting, Juventus, Borussia Dortmund na Inter Milan - zipo kwenye CV ya Sousa kwa klabu alizowahi kuzitumikia akiwa mchezaji. Alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi cha Juventus na Borussia Dortmund, huku akiichezea Ureno pia mechi 52 za kimataifa.
4. Hispania - Luis Enrique
Enrique ni moja ya wachezaji wachache waliohama kutoka Real Madrid kwenda Barcelona. Alidumu miaka mitano Bernabeu, alishinda ubingwa wa ligi kabla ya kwenda Barcelona alikocheza kwa miaka minane. Alibeba mataji mengine mawili ya ligi na kombe la washindi. Amechezea Hispania mechi 62.
3. Uholanzi - Frank de Boer
De Boer alicheza kwa miaka 11 kwenye klabu ya Ajax kabla ya kutimkia Barcelona alikocheza kwa miaka minne. Akiwa Ajax, alishinda mataji matano ya ubingwa wa ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja. Alishinda La Liga pia alipokuwa kwenye kikosi cha Barcelona.
2. Ukraine -
Andriy Shevchenko
Moja ya mastraika bora kabisa kwenye kizazi chake. Kiwango chake bora kilikuwa AC Milan alikocheza kwa miaka saba na kushinda Serie A mara moja na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alibeba mataji matano ya ligi kule Dynamo Kiev na Ballon d’Or 2004. Ameifungia Ukraine mabao 48 katika mechi 111.
1. Ufaransa -
Didier Deschamps
Marseille, Juventus na Chelsea - ni klabu tatu za kibabe kabisa alizowahi kuzichezea Deschamps, ameshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili na mataji matano ya ligi. Alikuwa nahodha wa Ufaransa ilipobeba Kombe la Dunia 1998.