Majeraha kichwani na madhara yake katika soka

SIKUKUU ya Pasaka iligeuka huzuni kwa wadau wa soka mkoani Songwe mara baada ya kutokea ajali ya kimichezo ya kugongana na mwenzake uwanjani na kusababisho kifo cha mchezaji wa Saza FC, Albert Andrea.
Tukio hili lakusikitisha lilitokea Jumapili katika mchezo wa kirafiki kati ya mashabiki wa Yanga na Simba uliokuwa na lengo la usherekeaji wa sikukuu ya Pasaka.
Aina hii ya ajali ya kimichezo si ambazo zinatokea mara kwa mara katika medani ya soka, kilichotokea ni bahati mbaya kwa mchezaji huyo aliyekuwa anachezea nafasi ya kiungo.
Kwa mujibu wa Ofisa wa habari wa Chama cha Soka mkoa wa Songwe, Charles Mwamlima mchezaji huyo kijana alifariki njiani wakati anakimbizwa kwa dharura Hospitalini.
Kwa upande wa jicho la kitabibu ajali hii ya kimchezo kama ajali iliyosababisha jeraha la aina tatu la ubongo ambalo linahusisha mchubuko au mchaniko wa ubongo hatimaye kuvujisha damu nje ya mishipa ya damu.
Aina hii ya jeraha huweza kusababisha kifo cha mapema kwa sababu ubongo ndio mdhibiti mkuu wa matukio nyeti ya mwili yanayotufanya kuwa hai ikiwamo mapigo ya moyo na upumuaji.
Hivyo ubongo unapopata majeraha makubwa na damu kuvunja ina maana kuwa tishu za ubongo zitakosa lishe ya damu yenye hewa safi ya oksijeni hatimaye tishu hizi zitakufa.
Jeraha la ubongo linavyosababisha kifo
Aina hii la jeraha hujulikana kitabibu kama Cerebral lacerations ni jeraha lenye matokeo mabaya linaloweza kusababisha kifo cha mapema au ulemavu wa kudumu.
Aina hii ya jeraha linatokana na nguvu kubwa kutua kichwani na kusukuma mfupa wa kichwa yaani fuvu na kujeruhi ubongo. Vile vile fuvu linaweza kuvunjika au kupasuka hatimaye kujeruhi ubongo.
Kazi kubwa ya fuvu ni kulinda ubongo usipate madhara na vitu kutokana nje ya mwili.
Madhara ya awali ya jeraha la aina hii ni kuvuja damu kulikotokana na shinikizo kubwa la kitu kilichogonga kichwani hivyo kuweza kusababisha majeraha ya vijinyuzi vya mishipa ya fahamu.
Hali hii ikitokea huweza kusababisha mlipuko katika tishu, mabadiliko ya shughuli za ndani ya tishu na ubongo kuvimba.
Hapa madhara ya muda mfupi yanayojitokeza ni kama vile kupoteza fahamu, kuweweseka au kuchanganyikiwa, kushindwa kuwezesha mihemko na mawasiliano ya mwili na kupata degedege.
Madhara mengine ni pamoja na ubongo kujaa maji, ute wa mfumo wa ubongo na uti wa mgongo kuvuja, mejaraha katika mishipa ya damu na fahamu katika ubongo na ogani kuu kusitisha utendaji.
Ubongo ni ogani nyeti iliyosheheni tishu za mfumo wa fahamu ambazo zimo ndani ya pango na hulindwa na tishu ngumu sana yaani fuvu la kichwa.
Ubongo huwa na ikiwa na kazi kama vile kutafsiri taarifa za misisimko mbalimbali, kudhibiti mapigo ya moyo na upumuaji na kuamrisha kutoka kwa vichochezi.
Ubongo una sehemu kuu tatu ikiwamo eneo la ubongo wa mbele katikati na nyuma. Ingawa sehemu hizi nazo zimegawanyika kuendana na utendaji.
Hivyo kupata majeraha makubwa ya ubongo ina maana mambo mengi mwilini yatasimama ikiwamo upumuaji, mapigo ya moyo na hisia za mihemko mbalimbali.
Hali hii ikitokea kifo cha mapema kinaweza kutokea au ulemavu wa kudumu unaweza kutokea ikiwamo kupooza viungo vya mwili.
Majeraha ya ubongo na historia katika michezo
Tukio kama hili si la kwanza, ingawa ni machache kwa majeraha ya kugongana katika soka kusababisha kifo. Majeraha mengi huwa ni mtikisiko au kuvimba ambayo hayana madhara makubwa.
Mchezo wa soka na michezo mingine inayohusisha kama vile kugusana kimwili ni kawaida kutokea kugongana na kupata madhara ya muda mfupi au ya muda mrefu.
Michezo inayoongoza kwa majeraha ya kichwa ni waendesha baiskeli na pikipiki, mpira wa miguu, mpira wa magongo, mchezo wa Ragbi, mpira wa kikapu na michezo ya majini.
Mwaka 2020 Mwanasoka wa Hull city ya Uingereza ajulikanaye kama Ryan Mason (26) alilazimika kutangaza kujiuzulu kucheza mpira wa miguu kutokana majeraha ya kichwa.
Alichukua uamuzi huo baada ya kushauriwa na wataalam wa afya kutokana na majeraha mabaya ya kichwa aliyoyapata januari mwaka 2017 katika mechi ya ligi dhidi ya Chelsea.
Kiungo huyo raia wa Uingereza alipata majeraha ya kichwa na kuvunjika fuvu baada ya kugongana na beki wa Chelsea, Garry Cahill.
Mwaka 2006 Peter Cech akiwa klabu ya Chelsea aliwahi kupata majeraja ya kichwa ambayo yalitishia kupoteza maisha mara baada ya kugonga kichwa katika miguu ya mchezaji wa Reading Stephen Hunt.
Ajali hii ilipasua fuvu la kipa huyu lakini ikawa bahati kwake hakuweza kupata majeraha makubwa ya ubongo ingawa hapo baadaye baada ya kupona alilazimika kuvaa kifaa maalum kichwani wakati wa kucheza ili kumpunguzia hatari ya kujijeruhi tena.
Mwendesha Magari maarufu duniani ya formula one Michael Schumacher alipata majeraha ya kichwa wakati akicheza mchezo wa kuteleza katika barafu mwaka 2013.
Ni moja ya ajali mbaya za kichwa kwa wanamichezo kwani ilimfanya kuwa katika hali ya coma kwa muda wa miezi 6 akiwa anauguzwa katika uangalizi maalum.
Majeraha haya yalimsababishia ulemavu wa kudumu kiasi cha kutegemea kuishi kwa kutumia mashine saidizi kwa ajili ya kuwezesha upumuaji na mzunguko wa damu na moyo.
KUPUNGUA HATARI
Majeraha ya aina hii yanaweza kuzuiwa kwa kuvaa kofia maalum kukinga kichwa kwa michezo ya waendesha baiskeli na pikipiki.
Kwa wanasoka wanatakiwa kuwa makini na kuwa na uungwana pale wanapowania mipira ya juu ili kuepusha ajali za kuwagonga wenzao kwa kiwiko au kwa kichwa.
Vile vile wanamichezo wazingatie mbinu wanazofundishwa kukwepa majeraha ya kichwani.