Mabondia wanaomiliki ndinga zao

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mabondia ambao kwa sasa wanamiliki magari yao wenyewe pamoja na bei zake.

ZAMANI mabondia wengi wa Bongo walikuwa wanapanda daladala au kukodisha magari kwa ajili ya kufika katika maeneo mengine kabla ya kuibuka kwa uwepo wa pikipiki maarufu bodaboda ambazo wapo baadhi wamefanya ni biashara yao.
Lakini miaka ya sasa mambo yamebadilika kwani wapo baadhi ya mabondia wakali wanaomiliki na kuendesha ndinga zao wenyewe ambazo zimetokana na mchezo wa ngumi pamoja biashara wanazoendesha.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mabondia ambao kwa sasa wanamiliki magari yao wenyewe pamoja na bei zake.

Alto Kyenga
Kyenga huenda akawa hana jina kubwa kwa mashabiki wa ngumi nchini lakini ni mmoja kati ya mabondia wanaozisaka pesa kutokana na mchezo wa ngumi na harakati nyingine.
Kyenga mwenye rekodi ya kucheza mapambano sita akiwa ameshinda matatu na kupoteza mawili huku mmoja akitoka sare, anashikilia rekodi ya kuwa bondia anayemiliki ndinga kali aina ya Nissan Fairlady ambayo thamani yake kiasi cha Sh28 milioni ambayo imejumuishwa na kodi zote muhimu.


Karim Khalid Said ‘Mandonga’
Mandonga ‘Mtu Kazi’ kutoka kuwa mpiga debe hadi kuwa mmoja kati ya mabondia wanaosukuma ndinga kali mjini siyo kazi nyepesi kabisa yaani hata mkimsema kwamba anajitoa ufahamu wala hajali kwani mambo kwake yanamuendea sawa.

‘Ukimpiga ni kama amekupiga tu’ ndio kauli mbiu yake ilivyo, kiufupi Mandonga hajali kupoteza pambano. Amepigana mapambano 13, ameshinda 6, amepoteza matano na sare 2.

Mwamba huyo ameweza kuutumia vizuri umaarufu wake na kumwezesha kumiliki ndiga mbili ambazo ya kwanza ni Toyota Nadia yenye thamani ya Sh16 milioni na Subaru Impreza ambayo nayo imekula siyo chini ya Sh18 milioni huku akiwa miongoni mabondia wachache wanaomiliki ndinga zaidi ya moja.


Twaha Kiduku
Shujaa wa Morogoro kwa sasa katika mchezo wa ngumi Twaha Kiduku mwenye rekodi ya kucheza mapambano 33 akiwa ameshinda 23 kati ya hayo manane pekee ameshinda kwa KO na amepigwa mara tisa kati ya hayo moja ni kwa KO huku akiwa na sare moja.

Kiduku ni miongoni kati ya mabondia wanaomiliki magari mawili ambapo gari yake ya kwanza ikiwa ni Toyota IST ambayo ina thamani ya Sh16 milioni kabla ya kushinda Toyota Crown yenye thamani ya Sh18 milioni kwa kumtwanga Dullah Mbabe mwaka 2021.


Ibrahim ‘Class’ Mgender
Uwezo mkubwa wa kupiga jabu wa bondia mpole nchini Ibrahim Class, umeendelea kumpa heshima ya kutosha katika mchezo wa ngumi za kulipwa akiwa na rekodi ya mapambano 37 kati ya hayo ameshinda 31, 14 yakiwa ni kwa KO, amepigwa mara sita, tatu ikiwa ni kwa KO.

Class ni miongoni mwa mabondia wenye wanaomiliki magari mawili ambapo gari lake la kwanza ni Toyota Belta ambayo bei yake inafika Sh15 milioni kabla ya juzi kati kuweka wazi kuwa ameongeza gari nyingine mpya aina Nissan Dualis ambayo inafika thamani ya Sh18 milioni.


Seleman Kidunda
Mwenyewe anajiita ‘Nusu Mtu Nusu Jini’ akiwa anashikilia mkanda wa mabara wa WBF huku rekodi yake yenye jumla ya mapambano 11, akishinda tisa kati ya hayo saba ni kwa KO na akitoka sare mara mbili.

Mwanajeshi Kidunda yeye anamiliki gari aina ya Toyota Rumion ambayo thamani yake nchini ni Sh16 milioni ambayo imejumuishwa na kodi za serikali ambapo pambano lake la mwisho alipata upinzani mkali kutoka kwa Asemahle Wellem kutoka Afrika Kusini walipotoka sare katika ‘Usiku wa Vita’.

Dullah Mbabe
Akiwa bado anapambana na upepo mbaya unaomuandama katika mchezo wa ngumi nchini, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ rekodi yake inaonyesha amecheza mapambano 50 akiwa ameshinda 33 kati ya hayo 29 ni kwa KO na amepoteza mara 15 kati ya hizo mara nne ni kwa KO na ametoka sare mara moja.
Mbabe yeye ni miliki wa gari aina ya Toyota IST ambayo inavuta jumla ya Sh16 milioni.

Tony Rashid
Licha ya kuporomoka nyota kutoka nyota tatu na nusu hadi nyota mbili na nusu na kuwa bondia namba moja Tanzania katika ‘Pound for Pound’, Tony Rashid ni mmoja kati ya mabondia wanaomiliki magari yao kwa mujibu wa watu wake wa karibu.
Tony au AK 47 anatajwa kumiliki gari aina ya Toyota IST ambayo thamani yake ni Sh16 milioni huku akiamua kuitupa kwenye biashara ya usafiri wa mtandaoni huku yeye akiendelea na harakati za ndani ya ulingo.

Haruna Swanga
Mmoja kati ya mabondia wachache wa uzito wa juu akiwa ni mwajiriwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huku rekodi yake ikisoma amecheza pambano moja pekee.
Swanga yeye anasukumua ndinga aina ya Toyota Premio ambayo thamani yake nchini ni Sh16 milioni kama ambayo anamiliki Mfaume Mfaume ambaye maarufu zaidi kama Mapafu ya Mbwa.

Mfaume Mfaume
Mfaume Mfaume mara zote anajiita Mapafu ya Mbwa kutoka anga za Nakoz Camp Mabibo akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 30, kati ya hayo ameshinda 18, manane yakiwa ni kwa KO amepoteza mara manane na sita ikiwa ni kwa KO huku akitoka sare mara mbili. Mfaume yeye ni mmiliki wa ndinga aina ya Toyota Premio ambayo thamani yake ni Sh16 milioni.