Mabao ya kibabe kwa wababe wa Ligi Kuu Bara

Saturday May 01 2021
DUBE PIC

By Charles Abel

MABAO ya nyota wanne wa Yanga, Simba na Azam huenda yakaleta wakati mgumu katika uteuzi wa bao bora la msimu pindi utakapomalizika mwezi Julai.

Wachezaji hao ambao kwa nyakati tofauti wamefunga mabao hayo ambayo yameonekana kuwa na mvuto wa kipekee kutokana na ufundi na hesabu zilizotumika kulinganisha na idadi kubwa ya mabao mengine yaliyofungwa katika Ligi Kuu Bara msimu huu hadi sasa.

Hapana shaka, kutokana na mvuto wa mabao hayo, ni vigumu kuyaondoa katika kundi la mabao 10 bora ambayo mwishoni mwa msimu mojawapo linaweza kuondoka na tuzo ya bao bora ambayo hutolewa katika tuzo za msimu ambazo huwa na vipengele tofauti.

Mabao hayo manne ambayo itakuwa ni vigumu kukosekana katika chati ya mabao 10 bora ya msimu huu ni ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Saido Ntibanzokiza dhidi ya Dodoma Jiji; mshambuliaji wa Simba, Luis Miquissone dhidi ya JKT Tanzania; straika wa Azam, Prince Dube dhidi ya Yanga na lile la beki wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ walipocheza na Gwambina FC.

Kati ya nyota hao wanne, Luis ndiye alianza kufunga bao la kusisimua katika mchezo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Oktoba 4, 2020.

Mshambuliaji huyo alinasa mpira uliomgonga beki wa JKT Tanzania baada ya shuti la Meddie Kagere na akiwa mbali kidogo na lango la wapinzani wao, Luis alipiga mkwaju wa mbali wa kuzungusha kwa mguu wake wa kushoto ambao ulikwenda kunasa kwenye nyavu za juu kulia za lango la wapinzani wao huku akimuacha kipa Patrick Muntari wa JKT Tanzania akiwa hana la kufanya.

Advertisement

Miezi miwili baadaye, Saido alimlipa Luis kwa kufunga bao la ustadi wakati Yanga ilipobuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Desemba 19.

Nyota huyo wa Burundi alifunga bao tamu la mkwaju wa faulo kwa kuuzungusha mpira pembezoni mwa ukuta wa Dodoma Jiji ambapo ulimshinda kipa Aron Kalambo, ukagonga mwamba na kujaa wavuni na kuipa Yanga uongozi katika mchezo huo.

Jumamosi, Aprili 24, Tshabalala aliongeza ugumu katika vita ya kuwania tuzo ya bao bora msimu huu baada ya kuifungia Simba bao kwa shuti la mbali la mguu wa kushoto ambalo lilimshinda kipa wa Gwambina, Mohamed Makaka na kujaa wavuni, mara baada ya kunasa pasi mkaa ya mmoja wa wachezaji wa Gwambina mbele kidogo ya mstari unaogawa uwanja.

Lakini wakati bao hilo la Tshabalala halijazungumzwa sana, juzi Jumapili straika wa Azam FC, Dube naye akaingia katika orodha ya nyota waiofunga moja kati ya mabao bora msimu huu pale alipoipachikia Azam FC bao pekee la ushindi dhidi ya Yanga.

Dube mara baada ya kunasa mpira uliomgonga kisogoni beki Abdallah Shaibu baada ya pasi ndefu ya Aggrey Morris, alimtazama kipa Farouk Shikhalo na kupiga shuti la wastani ambalo lilimshinda mlinda mlango huyo wa Yanga na kujaa wavuni katika dakika ya 87 ya mchezo.

Ukiondoa mabao hayo, yapo mengine sita ambayo nayo yanaweza kusumbua vichwa katika uteuzi wa bao bora msimu huu.


Ally Ramadhan

(KMC vs Gwambina)

Beki wa kushoto wa KMC alipokea vyema pasi ya Abdul Hillal akiwa nje ya eneo la hatari la wapinzani na kumtazama kipa wa Gwambina, Ibrahim Isihaka ambaye alikuwa amesogea kidogo na kisha kufumua kombora ambalo lilimshinda kipa huyo na kujaa wavuni


Rashid Juma (Namungo vs Polisi Tanzania)

Winga Rashid Juma alinasa pasi ya Tariq Seif akiwa upande wa kulia jirani na eneo la hatari la Namungo FC kisha akapiga shuti kali la mguu wa kulia ambalo lilienda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Nurdin Balora akiwa hana la kufanya.


Tariq Seif (Polisi Tanzania vs Dodoma Jiji)

Wakati Polisi Tanzania wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0, Hassan Maulid alipiga mpira mrefu ambao uliparazwa kwa kichwa na Marcel Kaheza kisha ukatua kifuani mwa Tariq Seif ambaye alikuwa jirani na eneo la hatari la Dodoma Jiji.

Alichokifanya mshambuliaji huyo ni kugeuka na kisha kuubetua mpira huo ambao ulimshinda kipa Aron Kalambo na kuipatia Polisi Tanzania, bao la pili.


Clatous Chama

(Simba vs Biashara United)

Akiwa anatazamana na kipa na beki wa Biashara United, Chama alinasa pasi ya Rally Bwalya na kuzuga kama anapiga shuti jambo lililovuruga hesabu za wapinzani ambao walilala upande wao wa kushoto wakiamini atapiga uelekeo na alichokifanya Chama baada ya hapo ni kuuelekeza mpira kulia ambao walinzi hao wawili walishindwa kuuzuia ukajaa wavuni


Jaffary Kibaya (Mtibwa vs Azam)

Jaffary Kibaya alipokea mpira uliookolewa vibaya na Yakubu Mohamed akiwa amelipa mgongo lango la Azam FC na alichokifanya baada ya kuutuliza aliusogeza mbele kidogo kisha kufumua shuti la mguu wa kushoto na kuiandikia Mtibwa Sugar bao pekee la ushindi katika mechi hiyo

Dube (Azam vs Kagera Sugar)

Mudathir Yahya aliyekuwa nyuma ya mstari unaogawa uwanja, alipiga pasi ndefu kuielekeza kwa Dube ambaye alimzidi ujanja na mbio mlinzi wa Mwadui FC na kuujaza mpira wavuni kwa staili ya kubetua na kumuacha kwenye mataa kipa Musa Mbisa.

Advertisement