Libya chimbo la mapro Simba, Yanga

SOKA siku hizi ni biashara kamili inayojiuza kwani eneo kubwa la dunia mchezo huo umekuwa pendwa na unachezwa.
Tanzania ni kati ya nchi za Afrika ambazo mazingira yake kwenye soka yanaimarika kila uchao huku ikiwa ni sehemu salama kwa wageni.

Kila timu ya Ligi Kuu Bara inaruhusiwa kusajili wageni wasiozidi 12 ingawa katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) hakuna idadi maalumu inayowazuia kusajiliwa kwani kwa sasa iko katika hatua ya kujitangaza zaidi.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea majina ya nyota wanane waliowika kwenye Ligi Kuu Bara na sasa wapo wanacheza soka la kulipwa Libya.


JESUS MOLOKO
Huyu ni raia wa DR Congo aliyekuwa mchezaji wa Yanga katika misimu miwili iliyopita na sasa yuko Libya akiichezea klabu ya Al Sadaqa SC ya Ligi Kuu nchini humo inayoshika nafasi ya nane kwenye kundi lake la 'A' baada ya kucheza mechi 11.

Ikumbukwe Ligi Kuu ya Libya ina jumla ya timu 20 zikiwa zimegawanywa katika makundi mawili A na B hivyo kikosi hicho cha Moloko katika michezo 11 kiliyocheza kimeshinda miwili, sare tatu na kupoteza sita kikijikusanyia pointi tisa.

Winga huyo wa zamani wa AS Vita Club akiwa Yanga aliiwezesha kutwaa taji la Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara mbili na Ngao ya Jamii mara mbili na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

JEAN BALEKE
Huyu alikuwa mshambuliaji kinara wa Simba kabla ya kuondoka dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu na kujiunga na Al Ittihad ya Libya kwa mkopo.

Baleke ni mchezaji wa TP Mazembe hivyo hata alivyokuwa Simba alikuwa kwa mkopo ambapo hadi anaondoka tayari alikuwa na mabao manane ya Ligi Kuu Bara akiwa ndiye kinara huku timu hiyo aliyojiunga nayo iko kundi 'B' ikishika nafasi ya tano.

HAFIZ KONKONI
Huyu ni mshambuliaji wa Yanga, raia wa Ghana aliyepelekwa Al Olympique ya Libya kwa mkopo na Wananchi ambapo tangu nyota huyo ajiunge na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Bechem United ya kwao Ghana mambo yamekuwa ni magumu zaidi kwake.

Kuondoka kwake kulitoa nafasi kwa viongozi wa Yanga kumsajili mshambuliaji mwingine, Joseph Guede kutoka Tuzlaspor ya Uturuki.

HARUNA NIYONZIMA
Moja ya malijendi wa soka la Tanzania waliotwaa taji la Ligi Kuu Bara mara nyingi zaidi ni Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyeitumikia Yanga kwa zaidi ya miaka minane katika misimu tofauti.

Haruna aliyewahi pia kuicheza Simba kuanzia mwaka 2017 hadi 2019, alishinda mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu Bara akiyabeba matatu mfululizo akiwa na Yanga kisha mawili mfululizo akiwa na Simba.

Kwa sasa, Niyonzima anamalizia soka lake Libya katika timu ya Taawon Ajdab ambapo licha ya ukongwe wake ila nyota huyo ameendelea kutegemewa kutokana na uzoefu wake wa kupita klabu mbalimbali.

Katika Ligi Kuu ya Libya, timu hiyo anayoichezea Haruna ya Ajdab iko kundi 'A' ambapo inashika nafasi ya tano na pointi 18.

STEVEN SEY
Huyu ni Mghana aliyejizolea umaarufu kwenye Ligi Kuu akiwa na Namungo kutokana na ubora wake wa kufunga mabao sambamba na staili yake ya kushangilia kwa kuchomekea kisha kupunga mkono ikitajwa kama staili ya kuwakera.

Sey aliyewahi kuichezea pia Dodoma Jiji, kwa sasa yuko zake Libya akikipiga kwenye timu ya Al Suqur SC inayoburuza mkia kwenye kundi A la Ligi Kuu.