Prime
Simba yaacha msala CAF

Muktasari:
- Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam ikiwa ni wa tatu mfululizo kwa viporo ilivyonavyo na wa 21 msimu huu kupitia mechi 25 ilizocheza hadi sasa na umeifanya ikifike pointi 66 zilizowahakikishia kuungana na Yanga inayoongoza msimamo ikiwa na 70, kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao.
SIMBA imeendeleza kugawa dozi katika Ligi Kuu Bara baada ya jana kuifumua Pamba Jiji kwa mabao 5-1 na kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, huku ikiziachia msala Singida BS na Azam FC zilizo na siku 10 ngumu za kuomba miujiza iwabebe ili zitinge michuano ya CAF.
Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam ikiwa ni wa tatu mfululizo kwa viporo ilivyonavyo na wa 21 msimu huu kupitia mechi 25 ilizocheza hadi sasa na umeifanya ikifike pointi 66 zilizowahakikishia kuungana na Yanga inayoongoza msimamo ikiwa na 70, kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao.
Lakini imeziachia msala Azam na Singida zilizopo katika nafasi ya tatu na nne zikisikilizia tiketi mbili za kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika.
Msimu uliopita Simba ilikwama kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa vile ilimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam, ambazo hata hivyo zilitolewa mapema, zikiiacha Simba iliyoshiriki Shirikisho Afrika (kama ilivyokuwa kwa Coastal Union), ikifika fainali na inajiandaa kucheza na RS Berkane ya Morocco.
Kukata tiketi hiyo ya CAF kwa Simba ikiungana na Yanga kumefanya zisalie tiketi mbili za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambazo moja ni ya timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu na bingwa wa michuano ya Shirikisho (FA) ambako vigogo hivyo vipo nusu fainali pamoja na Singida BS na JKT Tanzania.
Azam ipo nafasi ya tatu kwa sasa ndani ya ligi ikiwa na pointi 54, ikifuatiwa na Singida yenye 53, huku JKT inajiandaa kuvaana na Yanga katika nusu fainali ya michuano hiyo kama ilivyo kwa Singida itakayovaana na Simba.
Ipo hivi. Kama Simba au Yanga itabeba ubingwa wa michuano hiyo ya Shirikisho, timu itakayomaliza nafasi ya tatu na nne katika Ligi Kuu zitaungana na vigogo hao kwenye michuano ya CAF ikicheza Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini kama itatokea bingwa wa michuano hiyo atakuwa ni JKT Tanzania, atafuzu CAF na itazilazimu Azam na Singida kupambania kumaliza katika nafasi ya tatu ya Ligi Kuu na hapo ndipo klabu hizo mbili zitalazimika kuingia kwenye maombi ya siku 10 kuanzia leo kuiombea mabaya JKT.
JKT itaanza kuvaana na Yanga Mei 18 katika mechi ya nusu fainali ya ‘FA’ itakayopigwa Mkwakwani, jijini Tanga kabla ya Simba na Singida kumenyama Mei 31, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati, mkoani Manyara na kama itavuka hatua hiyo hadi fainali itazipa kazi Azam na Singida kupambania kumaliza katika nafasi ya tatu, hasa kama maafande hao watabeba ubingwa.
Lakini kipigo chochote itakachopata JKT mbele ya Yanga na kuing’oa itawapa ahueni Azam na Singida kunasa tiketi ya CAF msimu ujao bila kujua nani ataibuka bingwa wa Kombe la Shirikisho (FA).
Msimu sita mfululizo iliyopita, timu zilizomaliza nafasi ya nne zilinufaika kukata tiketi ya CAF kwa Kombe la Shirikisho kutokana na Simba na Yanga kubeba mataji mawili kwa mpigo ya Ligi Kuu na Kombe la FA, zikiwamo Namungo, KMC, Geita Gold, Biashara United, Singida Big Stars na Coastal.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Jean Charles Ahoua aliyekuwa hajafunga katika Ligi Kuu tangu alipotupia mara ya mwisho Machi 14 katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji, alirudi na moto kwa kufunga hat trick yake ya kwanza msimu huu.
Hat trick hiyo ilimfanya Ahoua kufikisha mabao 15 na kuongoza orodha ya wafungaji akimpiku Clement Mzize wa Yanga aliyekuwa akiongoza kwa muda mrefu akiwa na mabao 13.
Hiyo ilikuwa ni hat trick ya nne pia katika Ligi Kuu msimu huu baada ya ile ya Prince Dube na Stephane Aziz KI wote wa Yanga na Steven Mukwala wa Msimbazi na kuifanya Simba ifikishe jumla ya mabao 58 kupitia mechi 25 ilizocheza hadi sasa na yenyewe ikifungwa mabao 10.
Pointi 66 ilizofikisha Simba, zimeifanya kusaliwa na nne ili kuifikisha Yanga, huku ikiwa na mechi moja mkononi itakayopigwa wikiendi hii dhidi ya KMC na hapo kila moja kusaliwa na nne kabla ya kufunga msimu ikiwamo ya Dabi ya Kariakoo iliyopangwa kupigwa Juni 15 baada ya awali kuahirishwa Machi 8.
Ahoua alifungua akaunti ya mabao jana kwa penalti ya dakika ya 16 baada ya refa Shomary Lawi kutoka Tanga kuamua kwamba Joshua Mutale alichezewa madhambi wakati akiwania mpira na mabeki wa Pamba Jiji, japo marudio ya Azam TV yalionyesha ilikuwa ni laini na hata kabla haijapigwa wachezaji wa Simba waliingia ndani ya eneo la lango la Pamba.
Hata hivyo, mwamuzi Lawi alikubali bao hilo na katika dakika ya 37, Ahoua alifunga bao la pili kwa mpira wa frii-kikii iliyotokana na Mutale kuchezwa madhambi na kufanya hadi mapumziko Pamba iwe nyuma kwa mabao 2-0.
Simba iliweka bao la tatu katika dakika ya 47 likiwekwa kimiani tena na Ahoua aliyemalizia pasi tamu ya Ellie Mpanzu iliyokuwa asisti yake ya tano msimu huu, lakini likiwa ni bao la tatu kwa Simba na hat trick ya mfungaji huyo raia wa Ivory Coast aliyetua msimu huu.
Pamba inayonolewa na kocha Fred Felix ‘Minziro’ iliishuka kwenye Uwanja wa KMC, ikiwa na mabadiliko kadhaa ya kikosi cha kwanza, ikiwamo kukosekana kwa kipa Yona Amos na nafasi yake kushikwa na Mohamed Kamara, huku ikicheza dakika za mwanzoni kwa umakini kabla ya kupoteana.
Matumizi ya nguvu na kukaba kwa macho sambamba na kushindwa kucheza kwa utulivu, viliifanya Pamba ishindwe kuonyesha lile soka ililoonyesha katika baadhi ya mechi hasa katika duru la pili la ligi hiyo na hiki kilikuwa kipigo cha pili mfululizo mbele ya Simba baada ya awali kulala 1-0 jijini Mwanza.
Bao la nne na tano kwa Simba liliwekwa kimiani na Leonel Ateba dakika 80 na 85, aliyefikisha mabao 12, huku bao la kufutia machozi la Simba likiwekwa kimiani na Mathew Momanyi akitumia makosa ya kiungo wa Simba, Augustine Okejepha aliyepiga pasi ya nyuma isiyo na macho na mpira kumkuta mfungaji aliyeenda kumharibia ‘clean sheet’ ya 17, kipa Moussa Camara.