Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichowakuta Manula, Mzamiru na Mkude ni hiki

KILICHOWAKUTA Pict

Muktasari:

  • Nyota hao kwa sasa si wa kutegemewa kabisa kwenye klabu zao kwani takwimu zinaonyesha hawajatumika hata robo ya mechi zote za kimashindano za msimu huu ambazo timu zao zimecheza hadi sasa.

UKIANGALIA kinachoendelea kwa nyota waliokuwa tegemeo Taifa Stars na klabu zao, Aishi Manula, Mzamiru Yassin na Jonas Mkude, unaweza kujiuliza imekuwaje ghafla kiasi hiki hadi hawana tena nafasi ya kucheza kama ilivyokuwa awali. Kuna nini kipo nyuma yake na wafanye nini kurudi kama zamani?

Nyota hao kwa sasa si wa kutegemewa kabisa kwenye klabu zao kwani takwimu zinaonyesha hawajatumika hata robo ya mechi zote za kimashindano za msimu huu ambazo timu zao zimecheza hadi sasa.

Tukirudi nyuma kidogo, wakati Simba ikitamba katika Ligi Kuu Bara ikibeba ubingwa mara nne mfululizo, kikosi chao cha kwanza mara nyingi kilikuwa hakikosekani nyota hao watatu, Aishi Manula, Mzamiru Yassin na Jonas Mkude ambaye Julai 2023 alitua Yanga.

Simba mbali na kutawala misimu minne mfululizo Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2018-19 hadi 2020-21, pia kikosi hicho kimekuwa na rekodi bora kimataifa kwa kucheza robo fainali sita za mashindnao ya CAF katika misimu saba mfululizo kuanzia msimu wa 2018–19 hadi 2024-2025 ambapo sasa imefuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika yakiwa ni mafanikio ya juu zaidi.

Ukiweka kando msimu huu wa 2024-25, ukirudi nyuma hadi 2017-18, Manula, Mzamiru na Mkude walikuwa wachezaji muhimu ndani ya Simba.

Hata uhamisho wa Mkude kutoka Simba aliyoitumikia tangu mwaka 2011 hadi 2023 na kutua Yanga, uliibua mjadala mzito kutokana na ubora aliokuwa nao kiungo huyo ndani ya Simba na Taifa Stars.

Kwa sasa habari imebadilika, nyota hao waliokuwa sehemu ya mhimili mkubwa kwa Taifa Stars na klabu zao, ni kama wamesahaulika, ufalme wao umepotea ghafla huku tukishuhudia nyota wengine wanaocheza nafasi zao waking’ara jambo linalofanya kusahaulika kwao mapema.

Kuna maswali mengi ya kujiuliza, je Mkude, Manula na Mzamiru ndiyo mwisho wao umefika au wakipewa nafasi ya nyingine wanaweza kuonyesha kitu cha tofauti na kurudisha tena ufalme wao?

Mshambuliaji wa zamani wa Mgambo JKT, Yanga na Lipuli, Malimi Busungu alisema ili Mkude, Manula na Mzamiru warudi katika viwango vyao, hakuna njia nyingine zaidi ya kupata nafasi ya kucheza.

“Hao ni wachezaji muhimu kwa timu ya taifa ukiondoa ushindani uliopo katika klabu zao, lakini bila kupata nafasi za kucheza ni ngumu kuwa bora,” alisema Busungu.

Beki wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Amir Maftah alisema: “Nikiangalia timu ya taifa bado naona Manula anahitajika ingawa wapo makipa wengi wanaofanya vizuri katika timu zao kama Yona Amos. Kwa upande wa Mkude na Mzamiru wakipata timu ambazo watakuwa muhimu kikosi cha kwanza bado watafanya kazi nzuri.”

Mtazamo wa Maftah haukutofautiana na wa kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Mohamed Banka aliyesema: “Mkude, Mzamiru na Manula bado wana umri wa kucheza, kama hawapati nafasi waende katika timu ambazo watacheza ili huduma zao ziwe msaada timu ya taifa.”

KILI 01

AISHI MANULA

Msimu wa 2017-2018, Simba ilimsajili kipa huyu akitokea Azam, akafanikiwa kuwa namba moja kikosini hapo kwa misimu sita mfululizo kabla ya uliopita na huu mambo kuwa magumu kwake.

Manula ambaye anashikilia rekodi ya kuwa kipa aliyeshinda tuzo nyingi za Ligi Kuu Bara (5), amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa, Ayoub Lakred kutokea FAR Rabat ya Morocco msimu uliopita.

Ujio wa Moussa Camara kutoka AC Horoya ya Guinea msimu huu, ukaongeza balaa zaidi kwa kipa huyo mzawa ambaye hajacheza mechi yoyote ya kimashindano kati ya 43 ilizocheza Simba ambazo ni Ngao ya Jamii (2), Ligi Kuu Bara (25), Kombe la Shirikisho Afrika (12) na Kombe la FA (4), zaidi akiishia benchini mara chache.

Mara ya mwisho Manula kusimama langoni ndani ya kikosi cha Simba ilikuwa Agosti 31, 2024 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Pia mara ya mwisho Manula kukaa benchini ilikuwa Aprili 13, 2025 wakati Simba ikishinda 2-1 dhidi ya Mbeya City hatua ya robo fainali ya Kombe la FA.

Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, huku mwenyewe akiwa amekubali yaishe ilimradi mkataba umalizike aondoke salama Msimbazi bila tatizo.

Kabla ya kutopata nafasi ndani ya Simba, Manula alionyesha uwezo mkubwa hadi kuitwa ‘Tanzania One’ kwani tangu ajiunge na kikosi hicho ametwaa mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-18, 2018-19, 2019-20 na 2020-21.

Hivi karibuni, Manula aliitwa katika timu ya taifa, Taifa Stars na kuwa mmoja ya walioisaidia kufuzu ushiriki wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 wakati Taifa Stars ikiifunga Guinea bao 1-0, Novemba 2024 licha ya kwamba hakuwa anatumika Simba.

Pia amekuwa akitumika kama kipa namba moja katika mechi za Taifa Stars kufuzu CHAN 2025 na hata mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, hiyo inaonyesha kuwa bado ni tegemeo la taifa.

Kutokana na uimara wake kabla ya sasa mambo kuwa magumu, Manula ambaye mkataba wake na Simba unamalizika mwisho wa msimu huu, tayari amecheza michuano miwili ya AFCON iliyopita ambayo Taifa Stars imeshiriki mwaka 2019 nchini Misri na 2023 pale Ivory Coast. Pia ameshiriki Chan 2020 nchini Cameroon.

KILI 03

MZAMIRU YASSIN

Ndani ya kikosi cha Simba, Mzamiru msimu huu amecheza mechi saba tu za Ligi Kuu Bara kwa dakika 253, huku wakati mwingine akiwa nje akiuguza majeraha. Lakini baada ya kupona, ameendelea kutoonekana uwanjani akishuhudia Yusuph Kagoma, Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha na Debora Mavambo wakipeana zamu ya kucheza eneo la kiungo cha chini.

Mzamiru ambaye alitua Simba Julai 2016 akitokea Mtibwa Sugar, tangu ujio wa Kagoma, Mavambo na Okejepha msimu huu, nafasi ya kucheza kwake imekuwa finyu. 

Kutokana na kutopata nafasi ya kucheza, kiungo huyo hana mchango wowote katika upatikanaji mabao kwani hajafunga wala kuasisti.

Mchango wake katika kikosi cha Taifa Stars, pia ulikuwapo hasa katika michuano ya AFCON 2023 iliyofanyika Ivory Coast ambapo alijumuishwa kati ya nyota walioshiriki mashindano hayo. Hata hivyo, Mzamiru aliikosa AFCON ya 2019 na CHAN 2020.

Mkataba wake na Simba bado umebaki msimu mmoja, hivyo ana fursa ya kupambania nafasi yake kwa msimu ujao au kuangalia ustaarabu mwingine kutafuta timu mapema kabla mambo hayajaharibika zaidi.

KILI 02

JONAS MKUDE

Kuanzia 2011 hadi 2023, Mkude alikuwa kiungo muhimu wa Simba. Nyota huyo alifanya makubwa wakati Simba ikicheza robo fainali nne za CAF kati ya sita. Ni katika msimu wa 2018–19, 2020–21 na 2022–23 upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika na 2021–22 Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu uliopita ukiwa ni wa kwanza kwake ndani ya Yanga, pia alipata nafasi kubwa ya kucheza kulinganisha na msimu huu aliotumika kwa mechi mbili tu za ligi tena akicheza dakika 26, hajafunga wala kuasisti.

Ndani ya Yanga, ametua na baraka ya kushinda taji la Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Ngao ya Jamii, pia msimu uliopita alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichocheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati ambao Mkude hachezi ndani ya Yanga, Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Duke Abuya wanakiwasha kwenye eneo la kiungo cha chini.

Ukilinganisha takwimu za Mkude na viungo hao, utagundua kwamba, benchi la ufundi la Yanga limemuweka nyota huyo nafasi ya mwisho kwenye machaguo yao.

Kwenye ligi, Yanga ikiwa imecheza mechi 26, Aucho amecheza mechi 20 kwa dakika 1,555, akifunga bao moja na asisti moja.

Abuya amecheza mechi 23 kwa dakika 1,209 akihusika kwenye mabao manne kutokana na kufunga mawili na asisti mbili.

Mudathir amecheza 23 kwa dakika 1,542, ndiye kiungo wa nafasi hiyo aliyecheza dakika nyingi zaidi pia amehusika kwenye mabao mengi (5) akifunga matatu na asisti mbili.

Mkude pia amezidiwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyecheza mechi tisa za ligi kwa dakika 369, pia Aziz Andambwile amecheza mechi nne kwa dakika 105 licha ya kwamba wote hawajafunga wala kuasisti.

Mkataba wa Mkude na Yanga unamalizika mwisho wa msimu.