Prime
NONDO ZA LEJENDI: Mambo matatu yaliyojificha soka la Bongo

Muktasari:
- Kuna wanaoamini mabadiliko ya taratibu kwenye baadhi ya michuano inayohusisha klabu au timu za taifa ndio sababu ya kuonekana kama kuna hatua nyingi zimepigwa, mfano kuongezeka idadi ya timu kwenye michuano ya Caf kutoka nane mpaka kumi na sita.
KUNA hatua nyingi zimepigwa ki ushindani kwa soka letu kulinganisha na nyakati zilizopita. Inawezekana zisionekane mbele ya watu wengi kutegemea kipimo kinachotumika kwani hata mtu ili awe mrefu au mfupi inategemea amesimama na nani.
Kuna wanaoamini mabadiliko ya taratibu kwenye baadhi ya michuano inayohusisha klabu au timu za taifa ndio sababu ya kuonekana kama kuna hatua nyingi zimepigwa, mfano kuongezeka idadi ya timu kwenye michuano ya Caf kutoka nane mpaka kumi na sita.
Utaratibu wa awali ilikuwa makundi yanapangwa mawili yenye timu nne baada ya kila timu kucheza michezo sita huku timu mbili zilizokusanya alama nyingi zikienda hatua inayofuata ambayo ni nusu fainali.

Lakini sasa kuna makundi manne yenye timu nne-nne na timu mbili zilozokusanya alama nyingi kila kundi zinasonga mbele kwenye hatua ya kumi na sita bora au michuano ya timu za Taifa, mfano Afcon kutoka timu 12 mpaka 16 na hivi leo timu ni 24.
Ukiangalia Tanzania ilituchukua takribani miaka 30 kupata tena nafasi kwenye fainali za Afcon, lakini leo tunazungumza kufuzu mara tatu ndani ya misimu minne, unaweza kusema tunabebwa na mabadiliko pekee ya Kanuni za michuano peke yake ila utakuwa umesahau maeneo mengine kama ukuaji wa taaluma ya ukocha, ueledi kwenye uongozi na uwekezaji kwenye tasnia.

Kwenye eneo la ufundi na mbinu kuna mabadiliko makubwa na ni eneo muhimu sana lililoleta mapinduzi ya kiushindani ndani ya uwanja kwa kuwaandaa wachezaji kuanzia kwenye klabu zao na kufanya timu ya taifa kufaidika na kurahisisha kazi ya mwalimu wa timu ya taifa hasa anapotaka kuandaa mbinu za kuendea mechi kitu ambacho miaka niliyokuwa nacheza ilikuwa ni klabu chache, mchezaji anacheza mechi kwa kufuata maelekezo ukiachilia walioko Simba au Yanga ambao nao ndio wanaanza kujifunzia, hapo timu nyingi zilikuwa zinacheza kufuata kanuni tu kwamba sasa tuna mpira tunatanua uwanja, hatuna mpira tunabana uwanja na sio kila mchezaji kujua majukumu na wajibu wake ki mbinu kwenye nyakati zote za mchezo.
Uongozi pia ni eneo lingine ambalo limekuwa chachu ya hatua zilizopigwa kwa kuongeza weledi ki utendaji kuanzisha vitengo mbalimbali kusimamia, kufuatilia na kutathmini mwenendo wa soka letu mfano maono ya soka letu ndani ya uwanja yapo kwenye mikono ya mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo, hiyo ndio ofisi inayoandaa aina ya mpira ambao nchi yetu itaucheza (philosophy) kuzalisha walimu wenye uwezo wanaoendana na uhitaji wa tasnia kwa wakati huu kazi ambayo inafanyika kuwaongezea makocha uwezo kwa kuwaandalia madarasa ya kuwapandisha daraja kulingana na vigezo vya Caf.

Ukirudi miaka kumi nyuma tulikuwa na makocha wachache wenye Diploma A lakini leo ukiangalia ligi kuu wazawa wote ambao ni wakuu wa benchi la ufundi wana A huku A zingine zikiwa kwenye madaraja mengine, kuna Diploma B nazo chini yake zimezalishwa kwa wingi ukilinganisha na zilizokuwepo miaka kumi iliyopita, ni kundi ambalo wana sifa ya kuhudumu kama wasaidizi au wakuu Ligi Daraja la Kwanza, kuna kundi lingine lenye Diploma C, hili ndio naweza kusema ni kundi kubwa ambalo limejaa vijana ambao ndio matarajio ya mradi, tukijipa miaka kumi mingine kama sio 30 kufikia kuwa taifa lenye nguvu kwenye soka.
Katika uwekezaji, hii imekuwa nguzo na silaha ya kubadilisha mawazo kuwa matendo, tukianza na uwekezaji wa Azam Media kutangaza na kuiuza ligi yetu ndani na nje na kuifanya kuwa kivutio kwa wachezaji wa mataifa mbalimbali, walimu na wawekezaji wengine wa ndani na nje.

Kuwa na uhakika wa kuonekana kwa mechi zote imekuwa silaha inayotumiwa na klabu kuvutia wadhamini na kuongeza mapato ya timu.
Bila kuwasahau wapenzi na mashabiki wa mchezo wenyewe hasa utani wa timu mbili za Kariakoo una mchango mkubwa sana kwani sasa umetoka na kuangazia kimataifa, yaani kipimo cha ubora kimeanza kuwa ni kwa namna gani unashindana nje ya mipaka, hapo ndipo tumeshuhudia upepo ukihama kutoka kujivunia kuwa bingwa wa ligi na swali likiwa umefanya nini nje ya mipaka, aina ya usajili kulingana na wapinzani kimataifa imekuwa kama kipimo na sio ligi tena.
Tunakubaliana kanuni zimeongeza nafasi lakini haitoshi kuwa sababu pekee kwa timu kufanikiwa sababu hizi nafasi hazijaongezwa kwa ajili yetu bali ni kwa mataifa yote.

Kuna msemo wa watu wenye hekima unasema ukiwa ndani ya msitu unachokiona ni miti ila ukiwa nje ndio unauona msitu, kwa msemo huu inamaana sisi tuko ndani inawezekana hatuoni hatua zinazopigwa na klabu zetu, tunachotazama ni yale mapungufu tu na kuona hakuna kilichobadilika. Ukweli ni kwamba kuna hatua nyingi zimepigwa kwa kutazama tulipotoka.