Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Tuipokee tu fainali ya Ligi za Wakulima, PSG v Inter Milan

PAZIA Pict

Muktasari:

  • Yeye alikuwa mtu wa mwisho mwisho tu, lakini kabla ya hapo waandishi wa habari wa nchi nyingine zilizopo juu kimpira wamekuwa wakiitaja kama ligi ya wakulima 'Farmers League'. Kisa? Kwamba kiwango cha ushindani kipo chini.

MTU wa mwisho kabisa, kabisa kujaribu kutoa kashfa kwa Ligi Kuu Ufaransa alikuwa ni Cristiano Ronaldo. Akiwa Riyadh, labda kwa sababu ya kulewa pesa na sifa kwamba ameibadilisha Ligi Kuu Saudia Arabia alisikika akidai kwamba ligi hiyo ya Waarabu ni bora kuliko Ligi Kuu Ufaransa.

Yeye alikuwa mtu wa mwisho mwisho tu, lakini kabla ya hapo waandishi wa habari wa nchi nyingine zilizopo juu kimpira wamekuwa wakiitaja kama ligi ya wakulima 'Farmers League'. Kisa? Kwamba kiwango cha ushindani kipo chini.

Hata Lionel Messi alipokwenda PSG aliambiwa amekwenda kucheza ligi ya wakulima.

Na sasa mikononi tuna fainali ya PSG dhidi ya Inter Milan. Nilikuwa uwanjani Jumatano usiku pale Paris kushuhudia timu yangu ya Arsenal ikitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya nusu fainali na PSG. Ndio, mlima ulikuwa mrefu kwa Arsenal. Luis Enrique Martinez alikuwa anaitupa timu nyingine ya Kiingereza katika michuano hii.

PAZ 01

Aliwatupa Liverpool, Aston Villa na Jumatano usiku alikuwa anawatupa nje Arsenal. Siku moja kabla, Simone Inzaghi alikuwa akiwatupa Barcelona nje katika hatua ya nusu fainali. Hii inamaanisha nini? Tuna fainali za bingwa wa Ufaransa na bingwa wa Italia. Mpira unazidi kumchanganya mwanadamu anayeitwa mchambuzi.

Kule Italia mpira wao umedharaulika siku hizi. Uliheshimika zamani enzi za kina Ronaldo de Lima, Roberto Baggio, Paolo Maldini na wengineo. Wakati ule wanasoka ghali duniani walikuwa wanatoka Italia. Kila kitu kilikuwa Italia. Hata haki za matangazo ya mpira zilikuwa ghali Italia. Sasa hivi limetokea anguko kubwa ndani na nje ya uwanja.

Ndani ya uwanja inaonekana wachezaji waliofeli kwingineko ndio wanaoweza kwenda Italia. Kina Romelu Lukaku, Loftus Cheek, Tammy Abraham na wengineo. Hata Cristiano Ronaldo ilipoonekana kama uwezo wake umeanza kupungua pale Santiago Bernabeu rafiki yetu Florentino Perez ndipo akamruhusu kwenda Italia kucheza Juventus. Huu ni ukweli ulio wazi.

PAZ 02

Kwa sasa hakuna mchezaji aliye fomu maeneo mengine ambaye anaweza kwenda Italia. Vinicius Junior, Kylian Mbappe, Bukayo Saka, Lamine Yamal hawawezi kwenda Italia. Lakini zamani wachezaji wa namna hii ndio walikuwa wanakimbilia Italia na kuvunja rekodi ya uhamisho. Maisha yamegeuka. Sasa hivi mchezaji bora wa Italia ndiye atahitajika England na kwingineko.

Hata hivyo, mikononi tuna Inter Milan ambayo imepenya fainali na kwenda Munich. imeitoa Barcelona ambayo ni mbabe wa Hispania. Inzaghi amefanyaje? Hatujui. Kumbe kuna wakati linakuwa jambo la mbinu binafsi za kocha na kundi lake la wachezaji. Usingeweza kufikiria kwa viwango vya ligi kwamba kuna timu moja ya Italia ingekwenda fainali za Ligi ya Mabingwa.

Sisi tunaotazama soka la Ulaya kila siku tunaamini kwamba bingwa alipaswa kutoka Hispania, England au kule juu ambako tunamchota rafiki yetu Bayern Munich. Lakini, Inzaghi alionyesha makali yake kuanzia hatua za awali hadi ametinga fainali. Ametushangaza ambao tulikuwa tunaiona Ligi Kuu Italia kama ligi ya wakulima tu.

PAZ 03

Na pale Ufaransa umetoka pia mshangao kutoka kwa ligi ya wakulima. Sawa, Waarabu wameweka pesa nyingi kwa sasa pale PSG, lakini tuliamini kwamba ushindani mdogo wa ligi ya ndani usingeweza kuipa PSG nafasi kubwa katika Ligi ya Mabingwa hasa zilipokutana na Liverpool na Arsenal. Hata hivyo Luis Enrique Martinez alikuwa na jibu lake.

Ilikuwa inaaminika kwamba kwa PSG licha ya kuwa na kina Ousmane Dembele, Achraf Hakimi, Vitinha na wakali wengine, lakini ingekuwa katika kiwango kidogo cha ushindani kutokana na kucheza na kina Bastia, Lens, Montpellier kila wikiendi. Ni tofauti na England ambako bingwa hucheza mechi ngumu za ndani.

Na sasa yeyote ambaye atachukua ubingwa wa Ulaya atakuwa ametoka katika ligi ambayo hatukuitazamia. Atakuwa ametoka katika ligi ya wakulima. Wakulima wamerejesha heshima yao kwa kiasi kikubwa baada ya kudharaulika kwa muda mrefu. Mara ya mwisho Inter Milan kutwaa ubingwa huo ilikuwa 2013 ikiwa na Jose Mourinho.

PAZ 04

Kule katika michuano ya Europa haki inaonekana kama vile imetendeka. Manchester United na Tottenham Hotspur zimefika fainali ya michuano hiyo. Zote zinatoka Ligi Kuu England ambayo inaonekana kuwa ngumu zaidi duniani. Kitu kinachoshangaza ni kwamba timu zote zinasuasua vilivyo katika Ligi Kuu England.

Inaacha maswali kwa baadhi ya timu ambazo zilikuwa zinashiriki michuano hiyo huku zikionekana kuwa na nguvu. Vibonde wawili wa soka la England kwa sasa wamewezaje kukutana katika fainali ya michuano hii? Hapo Ligi Kuu England imethibitisha ubora wake kuliko katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Tuachane na hilo, na sasa turudi katika swali jingine la ubingwa wa Ulaya. Nani atakuwa bingwa wa Ulaya? PSG au Inter Milan? Ni swali gumu kidogo ingawa nafsi yangu naipeleka kwa Inter Milan. Inacheza kimbinu hasa na inajua inachokifanya. Namna ilivyocheza na Barcelona imenitia mashaka mawili.

Ina uwezo mkubwa wa kushambulia hasa kutokea pembeni. Inapiga mipira mirefu kwa watu wa pembeni. Mabeki Denzel Dumfries na Federico Dimarco wana mapafu ya mbwa. Na katikati kuna Lautaro Martinez anayecheza nyuma ya Marcus Thuram wamekuwa na kasi na uwezo wa kutazamana kwa haraka.

PAZ 05

Wasiwasi wangu ni namna wanavyoweza kujilinda. Mechi mbili za Barcelona ziliwaacha watupu kiasi cha kuruhusu mabao sita, licha ya ukweli kwamba nadhani PSG haipo katika kiwango cha Barcelona yenye Lamine Yamal linapokuja suala la kushambulia. Nadhani Inter Milan watakuwa bora katika kujilinda dhidi ya PSG pengine kuliko ilivyokuwa dhidi ya Barcelona.

Mbinyo ambao Inter Milan walipewa kwa Barcelona utakuwa mdogo tofauti na itakavyokuwa kwa PSG. Hata hivyo itakuwa fainali nzuri kuitazama huku wote tukiwa tumelazimishwa kutazama pambano la ligi mbili za wakulima. Tulidhani timu zetu pendwa za England na Hispania zingefika, lakini hakukuwa hata na moja ambayo iliweza kufika. Kelele zitapungua sana kuelekea fainali hiyo.