Prime
Lamine Yamal, mitaa ya Catalunya chini ya nyayo zake

Muktasari:
- Hisia nzuri zinakwambia mji wenyewe umepata mmiliki mpya. Sijui anajisikiaje Lamine Yamal popote alipo. Sijui wanajisikiaje wazazi wake Mounir na Sheila popote walipo. Kila kitu kuhusu Barcelona kwa sasa ni yeye tu. Na ana umri wa miaka 17 tu. Mara ya mwisho kwenda Barcelona mfalme wa mji wote alikuwa Lionel Messi.
HISIA nzuri ni kukatiza katika vitongoji vya Barcelona ukiwa umevaa fulana nyepesi. Tofauti na Ulaya nyingine Barcelona kuna joto zuri tofauti na baridi kali. Unatembea katika vitongoji vya Plaza Catalunya, Espana Catalunya, Liceu, Port Vell na kwingineko ukiwa tumbo wazi.
Hisia nzuri zinakwambia mji wenyewe umepata mmiliki mpya. Sijui anajisikiaje Lamine Yamal popote alipo. Sijui wanajisikiaje wazazi wake Mounir na Sheila popote walipo. Kila kitu kuhusu Barcelona kwa sasa ni yeye tu. Na ana umri wa miaka 17 tu. Mara ya mwisho kwenda Barcelona mfalme wa mji wote alikuwa Lionel Messi.
Mapema wiki iliyopita nilikuwa Barcelona kushuhudia namna ambavyo Barcelona imepata mfalme mpya baada ya Lionel Messi kumaliza siku yake ya mwisho kuvaa jezi ya Barcelona na kutimkia kwingineko. Lamini zaidi ya mfalme wa kawaida pale Catalunya.
Niliifahamu Barcelona wakati Mfalme Messi akiwa pale. Kila kitu kilikuwa kimeandikwa Messi. Jezi nyingi zilikuwa Messi 10. Vikombe na glasi zilikuwa zimeandikwa jina lake na namba yake 10. Kuta za mitaani zilikuwa zimechorwa sura yake na jina lake na namba yake ya mgongoni. Namba 10.

Katika jiji linalojaza Watalii wengi Ulaya kama Barcelona karibu kila mtalii akinunua jezi alikuwa ananunua jezi ya Lionel Messi namba 10 akawaonyeshe kwao. Iwe Canada, Mbeya, London au kwingineko. Na sasa amepatikana Mfalme mpya.
Hapa katikati Barcelona ilipotea. Haikuwa na timu wala mtu ambaye ni alama ya timu. Walikwenda hadi kina Pierre Emerick Aubamayeng, lakini nani angeweza kuwaangalia kama kioo? Hakuna. Na hata katika kucheza kitimu, timu yenyewe ilikuwa imeparaganyika.
Sasa ni zamu ya Lamine Yamal. Na kitu kizuri zaidi kinachowapa ufalme kuanzia Messi hadi Lamine ni ukweli wanakuwa watoto wa nyumbani. Messi alikwenda Barcelona akiwa na umri wa miaka 13. Wanamuona mtoto wa nyumbani.
Lamine amezaliwa Barcelona na wazazi wenye asili ya Morocco na Guinea ya Ikweta. Anachukuliwa kama mtoto wa nyumbani. Wazungu huwa wanasema ‘our very own boy’. Kama Kylian Mbappe angekwenda zake Barcelona bado asingepewa upendo ambao Messi na Lamine wamepewa. Angekuwa amekwenda mkubwa na akiwa tayari ameshapikwa kwingine.

Lakini Barcelona chini ya kivuli cha Catalunya na Madrid wana upinzani mkubwa na wa kihistoria tangu enzi za dikteta Franco. Hawa Wacatalunya wanataka kujitoa katika nchi ya Hispania watengeneze nchi yao. Wanaona watu wa Madrid wanawapelekesha chini ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo.
Madrid kwa muda mrefu inashindwa kutengeneza watoto wa nyumbani kama Lamine. Imekuwa timu ya matanuzi zaidi na kununua wachezaji wenye majina makubwa. Barcelona huwa inanunua lakini inategemea zaidi mhimili wa mastaa waliozaliwa nyumbani.
Kwa upinzani wa Madrid na Barcelona inakuwa dhambi kubwa kwa mtoto wa nyumbani kuhamia kwa wapinzani. Inakuwa dhambi kubwa kwa mchezaji kama Messi au Lamine kwenda kucheza Real Madrid. Roberto Lewandowski anaweza kwenda kucheza na kusiwe na hasira kubwa kwa sababu sio mtoto wa nyumbani Catalunya.

Na sasa kila kitu mtaani pale Catalunya ni kuhusu Lamine. Jezi yake namba 19 inauzwa zaidi. Picha yake ikiwa na jina lake pamoja na namba ya jezi yake vinachorwa katika mitaa ya masela. Kila kitu ni Lamine, Lamine, Lamine, Lamine.
Bahati nzuri zaidi kwa Lamine ni ameibukia katikati ya ufukara wa Barcelona. Messi aliibuka na kuiteka Barcelona, huku mbele yake wakiwa wametangulia akina Ronaldinho, Deco na Samuel Etoo ambao tayari walikuwa wamechukua mataji kadhaa na timu ilikuwa ina pesa.

Barcelona ilimhitaji zaidi Lamine kwa sasa. Sio Lamine tu, hata kina Pedri na Gavi. Ilihitaji watu kutoka katika timu ya vijana ambao wangeweza kuvaa viatu kwa usahihi na kwa haraka ili waepuke matumizi ya pesa.
Kwa sasa sheria za mpira pale Hispania zimekuwa ngumu na Barcelona imeshindwa kununua wachezaji mahiri kwa sababu inaonekana haina vyanzo vikubwa vya mapato. Ilihitaji vijana kutoka katika ya pili waache uvulana chini na kucheza kama wanaume. Lamine ameongoza jahazi.
Ndani ya miaka 17 tu ameshaichezea Barcelona mechi 100 tangu acheze mechi yake ya kwanza chini ya kocha Xavi Hernandez. Juzi alikuwa akifunga bao la kwanza dhidi ya Espanyol ambalo liliipa Barcelona ubingwa wa Hispania.

Lakini, Barcelona amefikia hatua ya nusu fainali chini ya hawa kina Lamine. Ina maana watoto wameanza kurudisha pesa klabuni. Mauzo ya jezi yanakwenda juu. Viingilio vimeanza kwenda juu tofauti na enzi za kina Aubamayeng. Pesa za kufika hatua za juu za michuano zimeanza kuingia katika akaunti.
Kwa Lamine binafsi nadhani dunia ipo mkononi mwake. Kwanza kabisa anawakilisha kizazi cha wahamiaji ambao kimekuwa kikidharauliwa barani Ulaya. Bibi yake alikuja Hispania akitokea Morocco akiwa na miaka 40 na amefungua kizazi cha wahamiaji wenye mafanikio.
Lakini kwa Lamine mwenyewe amejifungulia milango ya utajiri akiwa kijana mdogo zaidi. Ukiweka kando pesa nadhani unaweza kushangaa Lamine anakuwa Mwanasoka Bora wa Dunia kabla ya Mbappe na Vinicius Junior.
Ile nafasi ya kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia ipo huru tangu kuondoka kwa Cristiano Ronaldo na Messi. Kwa sasa inaweza kutwaliwa na yeyote yule. Mfikirie mchezaji kama Vinicius Junior. Tulipambana tukiamini alikuwa amenyimwa kwa makosa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia msimu uliopita. Hata hivyo, msimu huu amerudi akiwa mchezaji wa kawaida kabisa.
Lamine pamoja na utoto wake msimu huu tayari amefika nusu fainali za Ligi ya Mabingwa na ametwaa La Liga. Nani anajua nini kinaweza kutokea katika tuzo za Mwanasoka Bora wa Dunia? Wakati huo huo yeye na kina Pedri wanaweza kuhamishia makali yao hadi mwakani katika fainali za Kombe la Dunia pale Marekani, Canada na Mexico.