KWAKO KASHASHA: Kikosi Bora msimu huu ni hiki

Sunday July 18 2021
kashasha pic

LIGI Kuu Tanzania Bara imefikia tamati leo Jumapili, Julai 18 ambapo kulikuwa na mechi tisa kwenye viwanja tofauti nchini ambazo zimehusisha jumla ya timu 18.

Simba imemaliza na pointi 83 akiwa ni bingwa, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 74, Azam watamaliza wakiwa nafasi ya tatu na Biashara United wameishia wakiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Katika Ligi Kuu msimu huu, wapo wachezaji ambao wamefanikiwa kuonyesha kiwango kizuri na kwa mtazamo wangu wanastahili kupewa sifa za kipekee.

Leo tutaangazia wachezaji 11 ambao kwa mtazamo wangu naona wanastahili kuunda kikosi bora cha Ligi Kuu msimu huu unaomalizika.

Wachezaji hao ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Charles Edward Manyama, Abdulmajid Mangalo, Joash Onyango, Mukoko Tonombe, Feisal Salum, Clatous Chama, John Bocco, Prince Dube na Luis Miquissone.

Kipa Aishi Manula tunajua uwezo wake. Amekuwa na uwezo mzuri wa kucheza mipira ya hewani. Timing yake ni nzuri na amekuwa akifanya vizuri kwenye Ligi.

Advertisement

Upande wa kulia, Shomary Kapombe amekuwa akifanya vizuri kutokana na uwezo wake wa kupanda kama ilivyo upande wa kushoto kwa Charles Edward Manyama ambaye pia ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa mipira ya vichwa kwa sababu ya urefu wake na frii-kiki.

Abdulmajid Mangalo ni beki wa kati na ana sifa pia ya kuwa kiongozi. Ni mchezaji ambaye hakati tamaa na anahamasisha wenzie muda wote wa mechi. Hachezi rafu za ovyoovyo na anaonekana kuwa mgumu sana kupitika hasa ukimjia kwa mbele.

Joash Onyango ni mchezaji mzuri. Ana uwezo wa kucheza mipira ya hewani na ameweza kucheza akipangwa na beki yeyote yule. Hana mechi ndogo na kila mchezo anacheza kwa kujituma.

Namba sita ni Mukoko Tonombe. Ameonekana kuwa imara kwa muda wote. Ni kiungo anayetuliza timu na anakaba lakini pia anaweza kucheza box to box kusaidia wenzie. Amekuwa ni msaada mkubwa kwa timu ya Yanga.

Feisal Salum amekuwa akitumika kama kiungo mshambuliaji. Sasa hivi amekuwa akipangwa kama false number nine. Ni mchezaji mbunifu na mtulivu na hizi mechi za mwisho akiwa chini ya mwalimu Nabi amekuwa ameendelea kufunga mabao. Ni mchezaji ambaye hapotezi nafasi kirahisi akiwa analitazama lango.

Namba nane ni Clatous Chama. Ni mmoja wa viungo bora nchini. Mchezaji ambaye anagawa mipira sana na hakati tamaa licha ya kwamba sio mzuri sana kama timu inakuwa inashambuliwa japo amekuwa anajaribu kuimprove taratibu kama ambavyo jinsi mwalimu anavyojaribu kumbadilisha.

Ni mchezaji ambaye amekuwa hatari sana anapokuwa mbele ya lango na kasi ya Chama imekuwa tishio sana.

Ukienda kwa Bocco ambaye ndiye mfungaji bora kwenye Ligi Kuu msimu huu hadi sasa ni mchezaji ambaye hakuachi mbele ya lango. Ni straika ambaye anaweza kukupa vitu vingi. Anakupa mabao lakini anaweza kutoa assist ya bao, kudrive mipira, anacheza mipira ya juu na anasaidia ulinzi.

Namba 10 ni Prince Dube. Huyu yuko clinical mbele ya lango. Ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao , kchezesha timu na kupiga pasi za mwisho. Ana timing nzuri na movement yake imekuwa tishio kwa walinzi wa timu pinzani.

Winga wa kushoto ni Luis Miquissone. Ni mchezaji mgumu, asiyekabika, anadrive na anapiga miguu yote. Ni mchezaji ambaye hakati tamaa na amekuwa ni msaada sana katika mafanikio ya Simba kwa msimu huu kwa namna moja ama nyingine.


IMEANDIKWA NA ALEX KASHASHA

Advertisement