KWAKO JESSE JOHN: Mvua inyeshe tuone panapovuja Ligi Kuu

Sunday October 10 2021
mvua pic

PAZIA la Ligi Kuu lilifunguliwa rasmi takriban wiki mbili zilizopita, huku tukishuhudia ushindani wa uhakika na moyo wa kujitoa mhanga katika kuitafutia ushindi timu pamoja na uhakika wa pointi tatu ili kukaa sawa katika msimamo wa ligi na kuepuka mwanzo mbaya wa kujihesabu fungu la kukosa na kuingia katika kapu la wadhani wao “kushuka daraja”.

Pamoja na yote hayo zipo timu ambazo zimeanza vibaya kwa kupoteza michezo yao ya awali, lakini pamoja na baadhi yao kuwa ndo msimu wao wa kwanza wameonyesha dhamira ya ushindani, pamoja na ugeni walionao huku tukishuhudia timu ngeni pia zikizitoa kamasi timu zoefu katika ligi. Na kikubwa zaidi timu kubwa hazina mteremko katika kupata pointi tatu bila jasho na damu.

Tofauti kubwa inayoonekana kwa timu hizi ziitwazo kubwa ni kuwa na rasilimali fedha, rasilimali watu - kuna wadau wa uhakika katika kuzibeba ikiwa ni pamoja na miundombinu kama vile viwanja, kambi za uhakika, usafiri, vifaa vya mazoezi na vya kuchezea.

Hii ni pamoja na waalimu wengi wao wakiwa wa kigeni, ila kwenye suala la dakika 90 za mchezo huwezi kutofautisha kubwa na ndogo na wakati mwingine kubwa huteseka hasa kipindi cha pili kiasi cha kuona makocha wao wakiulizia muda kwa kamisaa ili amalize pambano.

Tumesikia baadhi ya timu zikilalamika kuwa ‘motisha wanazoahidiwa timu pinzani zinawafanya wachezewe ndivyo - sivyo’ wanasahau kuwa hata wao wanatoa ahadi ya bonasi kwa wachezaji wao ikiwa watashinda ama kutoka sare na wakipoteza pia wanapewa chochote kitu, huku timu zinazoahidiwa dhidi yao kwa ushindi ama sare vinginevyo ahadi huwa ndoto, huyeyuka wakishindwa kuzifunga.

Kinachotakiwa kwa timu zote ni kuonyesha uwezo wao, ufundi na mengineyo katika kuchagiza ushindi.

Advertisement

Zipo timu zina walimu wa kigeni tena wanalipwa fedha nyingi kuliko anazolipwa Malale Hamsini ama Fred Felix Minziro kulalamika ni aibu kubwa timu ikiwa na wachezaji wa kulipwa pesa ndefu tofauti na anazolipwa kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda.

Aidha, ni jambo la fedheha kwa timu kubwa yenye makocha wa kigeni ‘kupiga kelele’ kila wakati kwa kamisaa kutaka amwambie refa muda wa nyongeza umeisha amalize mpira na hasa wanaposhambuliwa, ila wanaposhambulia wao hunyamaza na kuwasukuma wachezaji wao kwa ishara wasogelee goli la adui.

Thamani na ubora wa timu unaonekana katika mchezo, utulivu wa mwalimu na kukubali matokeo kama ambavyo amekuwa akifanya Lwandamina, kocha wa Azam au Baraza, kocha wa Kagera Sugar ni jambo la busara na ukomavu unaoonyesha kuwa kamili na kuondoa hulka ya ubabaishaji.


TUIMULIKE STARS KWA UCHACHE

Mapema juzi timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilishuka uwanjani kuikabili timu ya Taifa ya Benin katika mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar na bahati mbaya Stars ilipoteza kwa kufungwa bao 1 - 0 na kuacha maswali mengi kuliko majibu juu ya hatima ya Tanzania katika michuano hiyo.

Nikiri kuwa vijana wetu walicheza vyema kiasi hususan katika kipindi cha pili wakitengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo hazikutumiwa vyema.

Kilichoutofautisha mchezo ni ukomavu tu (maturity) baina ya wachezaji wetu ambao hawajakulia kwenye misingi sahihi ya mpira na hata bao la Steve Mounie lilitokana na ukomavu wa mfungaji kujua Stars wameacha mwanya mwepesi kwenye ulinzi na Aishi Manula yupo kwenye nafasi isiyo sahihi (off-position) na mpigaji akapiga mpira wa kuzungusha (cave) ambao ndio uliotamatisha mchezo.

Kocha Kim Poulsen ni lazima afanyie kazi eneo la umaliziaji kwani katika kila mchezo taifa Stars wana wastani wa kupoteza nafasi 2-4 za wazi na wanaadhibiwa kwa makosa mepesi au wanapojaribu kucheza kwa mtego wa kuwavuta wapinzani kwa kuwasubiri kwenye eneo la juu kitaalamu huitwa ‘tactical delay’.

Bado nafasi tunayo ikiwa tutakuwa na nidhamu ya kimaeneo kwa maana ya wepesi na usahihi wa matendo wakati wa kujilinda na wakati wa kushambulia sanjari na matumizi sahihi ya nafasi kwenye eneo la mwisho.

Kocha huyo aiandae timu dhidi ya mipira ya kutenga (set-pieces) kwani mabao yao 10 ya mwisho katika mashindano yote sita yametokana na mipira hiyo - iwe kwa faulo au kona.

Naiona kesho njema ya Taifa Stars ikiwa timu hiyo itatunzwa kwani vijana wengi waliocheza Afcon ya vijana kule Gabon 2017 kama kina Dickson Job, Kibwana Shomari, Israel Mwenda, Kibabage, Abdul Suleiman na Ramadhan Kabwili wanaanza kupata nafasi kwenye timu ya wakubwa. Ni dalili njema. Kila la heri Stars.

Nitumie maoni yako, nitakujibu: 0658-376417

Advertisement