Kocha Yanga afunguka usajili Simba

Sunday February 21 2021
New Content Item (1)
By Thobias Sebastian

KOCHA wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu anasema kikosi cha Simba kimeimalika msimu huu tofauti na mara ya mwisho walipokwenda hapo na kuwafunga mabao 5-0, walikuwa kama wageni wa mashindano.

Simba wanaonekana wameimarika katika maeneo mengi kuanzia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, benchi la ufundi, wanacheza kama timu na si waoga kama walikuwa wanacheza awamu ya kwanza katika uwanja huu.

Ukiangalia ambavyo walicheza wanaonekana maandalizi yao yao yalikuwa mazuri katika kikosi chetu ambacho kilishindwa kufanya vizuri katika mechi ya nyumbani ingawa tulikuwa tifanya mashambulia ya mara kwa mara.

Mwanaspoti ambalo liliweka kambi DR Congo katika mji wa Kinshasa lilifanya mahojiano maalumu na Shungu ambaye alifunguka mambo mengi ikiwemo kuwashawishi wachezaji wengi wa Kikongomani kwenda kucheza soka Tanzania.


MUGALU AMFURAHISHA

Advertisement

Shungu anasema straika wa Simba, Mkongomani Chriss Mugalu ni moja ya wachezaji ambao wanamfurahisha kutokana na kiwango ambacho anaonyesha katika Ligi ya Tanzania licha ya ushindani ambao anakutana nao katika nafasi ambayo anacheza.

shungu pic 2

Anasema Mugalu ni moja ya wachezaji ambao aliwaona tangu akiwa mdogo na kumuibua huko mitaani na kuanza kumfundisha soka katika ngazi zote mpaka anapata nafasi ya kucheza nje ya DR Congo.

“Nilimwona kutokea mitaani huko kuwa anauwezo wa kucheza soka pamoja na kufunga mabao mengi ya mara kwa mara nikaanza kumtunza na kumuelekeza mafunzo mbalimbali katika timu za vijana mpaka amefikia hapa,” anasema.

“Mara zote huwa tunawasiliana katika maisha yake ya mpira kama kuna timu ambayo anataka kujiunga nayo kama ilivyokuwa Simba lazima anifuate na kutaka ushauri wangu ndio maana nilivyosikia anataka kujiunga nao nilimtakia kila la kheri na nilimpa baraka zote,” anasema.

“Baada ya kufunga bao katika mechi yetu kwa upande wa timu si matokeo mazuri lakini kwangu alinifurahisha kuonyesha kuwa amekuwa mkomavu zaidi kuifunga timu ambayo inatoka katika nchi yake na kucheza vizuri pia,” anasema Shungu.


KUPOTEZA AS VITA

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya mabingwa Afrika Simba waliweka rekodi ya kupata ushindi wa bao 1-0, katika mechi ya ugenini dhidi ya AS Vita ambao mara ya mwisho wanakutana nao walikuwa wamewafunga mabao 5-0.

Shungu anasema miongoni mwa mambo ambayo yamechangiwa kwa timu yao kupoteza kutokana na kushindwa kupata muda wa kufanya mazoezi na maandalizi ya kutosha, kikosi chao kinawachezaji wengi wapya wasiopungua kumi.

“Wachezaji hao wapya ambao tumewasajili kwa hivi karibuni hawana uzoefu wa kucheza mashindano kama haya makubwa pengine ndio maana Simba walituzidi na kupata nafasi ya kutufunga,” anasema.

“Kitaalamu timu inapopoteza mchezo tena katika uwanja wake wa nyumbani unatakiwa kumpa heshima mpinzani wako kwa kile ambacho amekifanya nasi tuwapongeze Simba walikuwa vizuri ndio maana wakatuzidi na kupata ushindi,” anasema.


SIMBA KIMATAIFA

Simba wanashika nafasi ya pili katika kundi ‘A’, wakiwa na pointi sawa dhidi ya vinara Al Ahly ambao wao katika mechi yao ya kwanza walishinda mabao 3-0, dhidi ya El Marreikh kutokea Sudan.

Shungu anasema kikosi cha Simba kutokana na ubora ambao wameonyesha msimu huu katika mashindano yao ya ndani na matokeo mazuri ambao wameyapata ugenini kama wakishinda mechi zao za Dar es Salaam watasonga katika hatua inayofuata.

“Simba watacheza mechi tatu nyumbani kwao ambazo kama watashinda zote maana yake watakuwa wamevuna pointi tisa ukijumla na tatu ambazo wamepata kwetu watakuwa na 12, ambazo zitawavusha robo fainali,” anasema.

“Ukweli kama Simba watacheza katika kiwango ambacho wameonyesha kwetu niwazi wanaweza kushinda michezo yao ya nyumbani lakini ikiwa tofauti na hivyo nao lolote linaweza kuwatokea,” anasema Shungu.


MAISHA BAADA YA YANGA

Shungu anasema tangu ameondoka Yanga maisha yake ya soka bado yanaendelea na wakati huu anafundisha timu mbili AS Vita pamoja na timu ya taifa ya DR Congo.

“Yanga ilinisaidia kujenga uzoefu na kupata maarifa zaidi katika ufundishaji wangu ambayo kuna mengine naendelea kuyatumia lakini kuna mabyo niliyacha kutokana na muda mrefu umeshapita,” anasema.

“Unajua hapa DR Congo timu zenye pesa zipo chache sana ndio maana huenda nashindwa kusikika zaidi kama ningekuwa naifundisha timu ya Yanga wakati huu,” anasema.

“Sikuwa na mambo mengi zaidi kwani tangu nimeondoka Yanga zaidi ya kuendelea na maisha yangu ya kufundisha soka ila nimehama tu eneo kutoka Dar es Salaam na kuwepo hapa Kinshasa,” anasema.

“Baada ya kuondoka Yanga kuna nyakati nyingine nilikuwa naendelea na masomo ili kuendeleza taalamu yangu ya ukocha ambayo ndio naitumia mpaka wakati huu,” aliongezea Shungu.


WANNE WAMVUTIA

Shungu amesema katika kikosi cha Simba ukiachana na kiwango ambacho ameonyesha mchezaji wake aliyemuibua tangu utotoni, Chriss Mugalu kuna wengine wanne ambao wamevutia katika na viwango vyao.

“Wachezaji ambao wamenivutia kutokana na uchezaji wao na katika mechi yetu walikuwa tatizo wapo wanne ambao ni, Clatous Chama, Luis Jose, Taddeo Lwanga na Meddie Kagere ambaye wamekuwa wakimfahamu kwa muda mrefu,” anasema.

“Si kama wachezaji wengine waliokuwa katika kikosi cha Simba ni wabaya hapana bali hawa wamekuwa wakinivutia kwa upande wangu kwani muda mwingi wanacheza katika kutimiza majukumu ya nafasi zao,” anasema Shungu.

“Ukiangalia hata katika mechi yetu wachezaji hao walikuwa na viwango bora pengine ni miongoni mwa sababu ambazo ziliwapa matokeo mazuri,” anasema Shungu ambaye katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti alionekana kuwa mtu mwenye ukarimu.


TUISILA / MUKOKO

Katika msimu huu vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamefanya usajili wa wachezaji wawili raia wa DR Congo, winga Tusila Kisinda na Mukoko Tonombe ambao wote wanacheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Shungu anasema wamekuwa wakiwafutilia wachezaji hao wawili tangu wameondoka nchini kwao ili kujua maendeleo yao kama kocha wa timu ya taifa lakini si wao pekee yao bali kuna wachezaji wengine wapo nchi kama za Morocco na Misri.

Anasema katika kuwafuatilia kwake wamegundua kuwa wanamaendeleo mazuri kutokana na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na AS Vita walipokuwa wanakutana na changamoto za ushindani wa nafasi ya kucheza.

“Ligi ya Tanzania inaushindani na inazidi kukua kila siku ni wazi kama watafanya vizuri thamani yao itaongezeka lakini wanaweza hata kupata nafasi ya kuitwa katika timu ya taifa,” anasema.


KURUDI TANZANIA

Shungu anasema kama akipata timu kutoka Tanzania ambayo inashiriki mashindano ya kimataifa kama ilivyokuwa AS Vita au Simba yupo tayari kurudi hapa nchini kuja kufundisha tena soka.

“Unajua napenda ushindani wa mashindano ya kimataifa iwe Ligi ya mabingwa au kombe la Shirikisho nitakubali kuja kufundisha lakini kama ikiwa haijapatikana timu ya namna hiyo sitawezakurudi huko,” ansema.

“Miongoni mwa nchi ambayo naipenda na nimeishi vizuri Tanzania ni moja wapo kwa maana hiyo nikipata timu yenye mahitaji ambayo nayataka nipo tayari kwenda kucheza,” anasema.


LIGI KUU BARA

Shungu anasema amekuwa anafuatilia Ligi Kuu Bara kutokana inaonyeshwa katika luninga na timu ambayo huiangalia mara kwa mara ni Simba kutokana wanamichezo nao miwili huku mmoja wakiwa wameshapoteza.

“Awali tulikuwa tukiwaangalia zaidi Simba katika michezo yao ua ligi na mashindano mbalimbali na tukajua wapo na ubora katika maeneo gani kama mapungufu yao yalivyo na tukawafunga mabao 5-0,” anasema.

“Sikuishia hapo nimekuwa nikiwaangalia hata msimu huu kabla ya kukutana nao lakini sitaacha kuandelea kufuatilia kutokana tunamchezo nao mwingine huko Dar es Salaam.

“Ligi ya Tanzania jambo la kuonyeshwa tu inaongeza thamani yake ya kuonekana kama ligi yenye kukuwa na maendeleo,” anasema Shungu.


KUWALETA WAKONGO

Tangu ameondoka hapa nchini katika kikosi cha Yanga kuna wachezaji wengi Wakongomani ambao wamekuja kucheza soka wakiwemo, Papy Tshishimbi, Heritier Makambo, Tonombe, Klaus Kindoki na wengineo wengi.

Shungu amesema kuna wachezaji wengi wa Kikongo wamekuwa wakimfuata na kumuomba ushauri wa kufanya maamuzi ya kuja kucheza soka la kulipwa Tanzania na amekuwa akiwasukuma na kuwashauri kukubali.

“Kuna ambao wamekuwa wakitaka kuja kucheza huku na nikiwapa ushari tu wanakuwa hawana kizuia lakini kuna ambao wanashindwa kukubali kwa urahisi mpaka kupata ushauri kutoka kwangu na hilo alikuwepo nalo Mugalu lakini baada ya kumuelewesha alikubali mara moja,” anasema Shungu.

Advertisement