Prime
Kilichomfanya mtoto wa Matumla kugomea shule, kugeukia ngumi

Muktasari:
- Lakini, kumbe ilikuwa danganya toto, Jay Msangi akapiga mkwanja wake maisha yakaendelea na Mohammed Matumla ndoto yake Las Vegas ikayeyuka, licha ya kumshinda Mchina kabla ya 2017, madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa Moi kutangaza kuwa Mohammed hatakiwi kucheza ngumi tena kwenye maisha yake kutokana na kufanyiwa upasuaji wa kichwa uliotokana na damu kuvia kwenye ubongo.
MWAKA 2015 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, promota mwenye maneno mengi na uwezo wa mkubwa wa ushawishi, Jay Msangi alimpiganisha Mohammed Matumla dhidi ya Xinghua Wang kutoka China na kutangaza mshindi atakwenda Las Vegas, Marekani, kupigana pambano la utangulizi katika pambano la Flody Mayweather na Manny Pacquiao.
Lakini, kumbe ilikuwa danganya toto, Jay Msangi akapiga mkwanja wake maisha yakaendelea na Mohammed Matumla ndoto yake Las Vegas ikayeyuka, licha ya kumshinda Mchina kabla ya 2017, madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa Moi kutangaza kuwa Mohammed hatakiwi kucheza ngumi tena kwenye maisha yake kutokana na kufanyiwa upasuaji wa kichwa uliotokana na damu kuvia kwenye ubongo.
Huenda matumaini ya familia ya mkongwe Rashid Matumla kuona kizazi chake kikiendelea na mchezo pendwa wa familia yao ilizimika na hakukuwa na matumaini tena kabla ya kuibuka kwa Amir Matumla ambaye kwa sasa amekuwa gumzo kwenye mchezo huo.
Amir anatajwa kurithi hadi aina ya uchezaji wa baba yake mzazi, huku akipendelewa kuwa na mwili mkubwa pamoja na kimo kinachoonyesha kwamba atakuwa moto wa kuotea mbali siku za usoni.
Bondia huyo aliyechukuliwa na uongozi wa Mafia Boxing Gym ili kuendeleza kipaji anatarajiwa kupanda ulingoni Februari 28, mwaka huu, kwenye Ukumbi wa City Centre, Magomeni, Dar es Salaam katika pambano la 'Knockout ya Mama' linaloandaliwa na Mafia Boxing Promotion ambalo awali lilitangazwa lingefanyika Februari 23 kabla ya kupelekwa mbele hadi Februari 28.
Amir katika pambano hilo amepewa dhamana ya kucheza pambano kuu (main card) dhidi ya Paulus Amavila wa Namibia ambalo litakuwa la raundi nane kwenye uzani wa super walter.
Bondia huyo ana rekodi ya kucheza mapambano sita ambayo amefanikiwa kushinda yote, mawili yakiwa kwa knockout ambapo anakamata nafasi ya tatu katika mabondia 53 wa uzani wa middle wakati duniani akiwa wa 158 katika mabondia 1970 huku akiwa na hadhi ya nyota mbili.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Amir ambaye ameeleza safari yake ilivyokuwa katika mchezo huo hadi kujiunga na Mafia Boxing Gym ambayo kwa sasa inatajwa kuwa menejimenti bora inayosimamia mabondia kwa weledi nchini.
Matumla anasema safari yake katika ngumi haikuwa bahati mbaya kwa sababu katika familia kucheza ngumi ni suala la lazima, siyo hiari labda mwenyewe uamue kufanya mambo mengine lakini upewe nafasi ya kujifunza.
"Kuna mambo mengi ndiyo yaliyonifanya niingie kwenye mchezo wa ngumi, lakini moja wapo ni kurudisha mchezo wa ngumi Temeke lakini familia kama familia heshima yake iendelee kubaki ilipokua zamani," anasema.
"Lakini kitu cha pili ni mimi mwenyewe maisha yangu kwa sababu sina elimu yoyote. Sijasoma, sijaenda shule, nimeona sehemu pekee ya kupambania ugali wangu au familia yangu ni katika mchezo wa ngumi ndiyo vitu vilivyonisukuma kuingia kwenye mchezo huu."
SWALI: Ilikuwaje ukashindwa kusoma wakati baba yako alikuwa na uwezo na jina kubwa nchini?
JIBU: "Kilichonifanya nishindwe shule, kitu cha kwanza nilikuwa mtu ambaye sipendi shule lakini kitu cha pili nilikuwa hata nikienda huko shule sikuwa msomaji, nilikuwa mtu wa kukaa nasubiri kengele ilie nirudi zangu nyumbani.
"Niliendelea hivyohivyo hadi darasa la saba nikahitimu na nilifaulu, lakini sikuwa na haja ya kuendelea na shule. Nikamwambia mzee kuhusu kusoma atapoteza pesa zake aache zaidi nataka niwe kwenye ngumi. Mzee alinikubalia japokuwa alikuwa na uwezo wa kunisomesha maana mwenyewe ndiyo nilikuwa najiona siwezi, lakini aliniambia kama nataka ngumi ila siyo kazi rahisi nijitume. Tulikuwa tunafanya mazoezi na ukweli, ngumi nimeanza nikiwa mdogomdogo maana familia yetu lazima ujue ngumi, akaanza kunisaidia halafu akanipeleka jeshini kucheza ngumi za ridhaa nikaenda JKT nilikaa kama miaka minne, nilivyotoka akaanza kunipa mazoezi upya kwa ajili ya ngumi za kulipwa."

SWALI: Umecheza pambano mengi na mengine ulipigwa, lakini hayapo kwenye rekodi yako?
JIBU: "Kuhusu suala mapambano niliyocheza ni mengi yanaweza kufika hata 10, lakini kwenye rekodi yangu kuna mapambano sita pekee. Lakini tatizo ni mapromota waliokuwa wanaandaa mapambano, hawakuwa makini na waliokuwa wakifanya. Nasema hivyo kwa sababu nimecheza mapambano mengi, lakini mengi ni mabonanza tu hayakufanywa kama biashara kwa kuingizwa kwenye rekodi na mtu mambo yako yakaenda. Lakini kutokana na hivyo ndivyo watu wakaniona, wakanichukua na kuanza kucheza kwa mapambano kuingizwa boxrec, lakini kabla ya hapo nimecheza mapambano mengi hayakuwahi kuingizwa."
SWALI: Jambo gani ulikutana nalo ukaona kwako ni gumu?
JIBU: "Changamoto za mchezo tu nilikutana nazo, nakumbuka nilienda gym moja Manzese, kipindi hicho nacheza ngumi za ridhaa wakati huo nilikuwa napenda kutafuta changamoto baada ya kusema nataka kucheza ngumi kweli yaani asubuhi jeshini lakini jioni naingia mazoezi mtaani. Sasa nilienda kupata 'sparing' huko Manzese ...sasa walinichangia ikafika hatua hadi nikazimia, wakanipeleka hospitali pale Mwananyamala. Nadhani nilipigwa ngumi raundi ya nane nikashuka (kuanguka) ndiyo nikapelekwa hospitali na ndiyo niliamkia huko ila kumbukumbu yangu kabla ya kuzimia nilicheza na mabondia wanne."
SWALI: Baba yako hakupata wasiwasi kwa kuwa Mohammed naye alipata tatizo lililomuondoa kwenye ngumi?
JIBU: "Kwanza tatizo lilikuwa dogo, nilitibiwa ingawa nilizimia saa 12 jioni nikaja kupata fahamu saa nane usiku. Mzee hakusema kitu kwa sababu anaelewa ni sehemu ya mchezo."
SWALI: Ni kweli umekuwa ukipendelewa kwenye mapambano yako kwa sababu ya jina la baba yako?
JIBU: "Hapana kwa sababu kwa upande wangu sioni hicho kitu. Mapambano yangu yote ninayocheza watu wanaona halafu wanafurahia mchezo, lakini wanaona ngumi zinavyochezwa na ushindi unavyopatikana, sidhani kama napendelewa."
SWALI: Umekuwa chini ya wadau mbalimbali na ikazuka migogoro kimkataba nini umejifunza?
JIBU: "Kikubwa ni kwamba mafanikio siku zote yanakuja kwenye njia ngumu, lakini kama ulivyosema suala kupitia migogoro imenifanya kuongeza na kuwa makini."
SWALI: Ni kweli uliwahi kuwa chini ya menejimenti ambayo kitu pekee ilichokuwa inakupatia ni kiroba cha unga?
JIBU: "Ni kweli niliwahi kuwa chini ya menejimenti ya namna hiyo wakati naanza ngumi za kulipwa, nilichukua watu wakawa wananisaidia na msaada wake ulikuwa ndiyo ulikuwa huo wa kiroba cha unga. Lakini nashukuru Mungu ameweza kunisaidia kusogea mahali na tumeacahana vizuri ila hakuna kibaya likichokuwa kinaendelea tumemaliziana vizuri."

SWALI: Kiasi gani kikubwa ambacho umewahi kulipwa kwenye ngumi?
JIBU: "Hakuna pesa kubwa ambayo niliwahi kulipwa zaidi ya laki tatu, laki mbili na laki tano. Pambano moja tu ndiyo nilipata milioni tena niliipata kwa mafungu baada ya kupelekana Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa (TPBRC).
Lakini nimeweza tu kununua vitu vya ndani, kitanda godoro, lakini hakuna kitu chochote cha maana nilichoweza kufanya mpaka sasa kupitia pesa ya ngumi."
SWALI: Nani amekupeleka Mafia?
JIBU: "Kitu ambacho naweza kusema ni kwamba bosi wa Mafia ana ukaribu na mzee wangu wanafahamiana kwa sababu wote wanatokea sehemu moja kiasili, hivyo kwangu haikumpa ugumu kwa sababu pia alikuwa akiniona nikipigana kwenye mapambano yangu. Mwenyewe ameona anaweza kunisaidia kwa sababu ni mtoto wa kaka yake, ndiyo maana unaona leo nipo hapa maana hata kwangu nilipoambiwa haikuwa ngumu, tulizungumza mambo yakawa sawa. Lakini hakuna mtu ambaye aliniambia nenda Mafia moja kwa moja, nawashukuru wamenipokea vizuri sasa mimi ni familia ya Mafia."
SWALI: Februari 28, unakwenda kucheza 'main card' ya KO ya Mama nini ambacho unakiona?
JIBU: "Kwanza inanipa hofu ya kufanya mazoezi kwa nguvu na bidii halafu kitu kingine ni kama heshima kwangu kwa sababu kuna zaidi ya wachezaji wakali zaidi yangu, lakini hawajapata nafasi. Nimeweza kupata mimi nafasi ya 'main card' naona ni heshima nimepewa. Binafsi sitaweza kuifanyia mchezo, nitaiheshimu na nitaonyesha sijapewa hiyo heshima kwa bahati mbaya na kuhusu kupata knockout naweza kusema huwa inaandaliwa mazoezini. Nina uhakika itapatikana kwa sababu tumeiandaa na kuitengeneza mazoezini, naamini Mungu yupo na mimi."
SWALI: Kwa nini ulisema unataka kuirudisha heshima ya Temeke?
JIBU" "Naweza kusema kwamba Temeke ndiyo kitovu cha michezo na kitovu cha mchezo wa ngumi yaani ukizungumzia ngumi Tanzania basi huwezi kuikwepa Temeke na heshima yake iliyokuwepo zamani sasa imeshuka, hivyo nimejivika mabomu kuirudisha heshima yake."