Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kicheko cha Haaland miaka 87 penzini na Isabel

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo wa Manchester City alichukua mpira na kuuweka chini ya jezi eneo la tumbo, huku kidole gumba kikiwa mdomoni akiashiria kuwa mpenzi wake wa muda mrefu, Isabel Johansen, 21, ni mjamzito.

Akiwa anasherehekea kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu yake ya taifa ya Norway kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Slovenia, Erling Haaland, 24, alitumia nafasi hiyo kuitangazia dunia anatarajia kuwa baba.

Mshambuliaji huyo wa Manchester City alichukua mpira na kuuweka chini ya jezi eneo la tumbo, huku kidole gumba kikiwa mdomoni akiashiria kuwa mpenzi wake wa muda mrefu, Isabel Johansen, 21, ni mjamzito.

Haaland aliweka rekodi hiyo Oktoba 10, 2024 akienda kambani mara mbili na kufikisha mabao 34 katika mechi 36 na kuvunja rekodi ya Jorgen Juve iliyodumu kwa miaka 87 akiwa amefunga mabao 33 katika michezo 45.

Ilikuwa ni siku nzuri yenye furaha na iliyobeba maana pana ya maisha kwa mzawa huyo wa Leeds, West Yorkshire, England upande wa kazi na familia akiivunja rekodi ya miaka 87 na kutangaza ujauzito wa mpenzi wake.

Baadaye Haaland alichapisha picha hiyo katika ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 30 na kuweka emoji ya mtoto ikifuatiwa na maneno ya Kiingereza 'coming soon' yaani hivi karibuni anazaliwa na mama yake ni Isabel.

Picha linaanza miaka 19 iliyopita wakati Haaland anajiunga na Bryne nchini Norway akiwa na umri wa miaka mitano na kujifua kuanzia 2005 hadi 2016 akiwa katika akademi hiyo ndipo akakutana na Isabel.

Hata hivyo, kabla mambo hayajapamba moto, Isabel ambaye alikuja kuichezea timu ya wakubwa ya wanawake ya Bryne Fotballklubb, aliachwa mpweke na rafiki yake huyo baada ya kuhamia Red Bull Salzburg alikocheza tangu 2019 hadi 2020.

Uhusiano wao ulianza kipindi Haaland anakipiga Borussia Dortmud, vigogo wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) aliowatumikia kuanzia 2020 hadi 2022 akicheza michezo 67 kisha kutimkia Man City ya Ligi Kuu England (EPL).

"Isabel amesafiri kwenda Ujerumani na Uingereza kila mara ili kuonana na Haaland, na sasa amekuwa naye. Isabel anajulikana sana kwa uzuri wake huko Bryne. Wote wanafahamiana vizuri kwa muda mrefu," chanzo kimoja kiliiambia The Sun.

Chanzo kingine kilisema Haaland anatembea na ulimwengu miguuni mwake, ni wanawake wengi wamepanga foleni wanatamani kuwa naye, lakini alihitaji mtu ambaye anaweza kumuamini ili kujikita katika kazi ya mpira wa miguu.

"Hata hivyo, yeye ni mvulana mwenye busara na inaeleweka kuwa yuko katika uhusiano na msichana kutoka mji wa nyumbani kwao (Bryne) ambaye anajulikana kwa miaka mingi," chanzo hicho kilieleza.

Isabel aliyezaliwa na kukulia katika mji mdogo wa Bryne wenye takribani watu 12,465, mara nyingi huwa uwanjani kumshangilia kipenzi chake, Haaland na kwa miaka ya hivi karibani wamekuwa wakiongozana katika hafla ya tuzo mbalimbali.

Marafiki zake wengi wanamtaja kama msichana mwenye bahati zaidi kwa jinsi maisha yake alivyobadilika kwa haraka sana, miaka michache nyuma alikuwa ameketi katika moja ya madarasa ya sekondari huko Kusini- Magharibi mwa Norway.

Aliendesha baiskeli kwenda shule na kula chakula cha mchana kawaida na wanafunzi wenzake, lakini sasa anaendesha gari la kifahari aina ya Rolls-Royce Cullinan lenye thamani ya Euro400,000 na kula kwenye migahawa mikubwa ya Manchester.

Kutokana na kwamba Norway haikufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022, wawili hao walienda kupumzika katika jumba la kifahari la Haaland huko Marbella na wiki chache baadaye walionekana katika mgahawa wa kifahari wa Manchester, The Ivy kwenye mkesha wa mwaka mpya.

Walipita pamoja juu ya zulia jekundu katika hafla ya tuzo za Ballon d'Or mwishoni mwa 2023. Pia walionekana wakimtembelea Baba yake Haaland, Alfie, beki wa zamani wa Man City na Leeds United ambaye alikuwa amenunua nyumba mpya huko Marbella.

Isabel alikuwepo hapo Machi 2014 wakati Haaland anasaini mkataba na Nike wenye thamani ya Euro20 milioni kwa ajili ya kuzalisha viatu vyake huku akiungana na mastaa kama Ronaldo, De Bruyne na Mbappe wanaodhaminiwa na kampuni hiyo ya Marekani. 

Wawili hao walikuja kujaliwa mtoto wao wa kwanza hapo Desemba 2024, Kocha wa Man City, Pep Guardiola ndiye aliyefichua habari hizo njema katika mahojiano baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Leicester City ambao walishinda magoli 2-0.

"Wakati mwingine Erling amehukumiwa vibaya lakini ni sehemu ya soka. Amechoka, amecheza dakika nyingi. Amekuwa baba kwa mara ya kwanza katika siku chache zilizopita, hivyo alikuwa na hisia nyingi na msisimko siku chache nyuma," anasema Guardiola.

Ni wazi Haaland kulea mtoto na Isabel ilikuwa ndoto yake ya muda mrefu na anashuhudia ikitimia mapema kama ilivyokuwa ile ya kuwa mfungaji bora wa Norway kwa muda wote akiisambaratisha rekodi iliyoishi kwa miaka 87, sawa na takribani siku 31,755.