JICHO LA MWEWE: Ukiyashangaa ya Etienne, utayakuta ya Kim Poulsen

SIJUI Kim Poulsen ataiandaa vipi Taifa Stars katika pambano dhidi ya Guinea ya Ikweta. Sijui. Atakuwa katika benchi katika pambano hilo la kufuzu Afcon 2021 Machi ugenini. Litakuwa pambano muhimu kwa Taifa Stars kushinda ili turudi tena katika fainali.

Sina utabiri na kikosi chake siku hiyo isipokuwa ninachojua ni kwamba kwa ujumla wake wakati akikitumikia kikosi cha Taifa Stars atawapa mashabiki wa soka nchini wakati mgumu. Alishawahi kutupa wakati mgumu huko nyuma na tujiandae kwa nyakati nyingine ngumu za uteuzi wa kikosi chake hadi upangaji kwa ujumla. Majuzi tumetoka kumshutumu kocha wa timu ya taifa aliyepita, Etienne Ndayiragije.

Hatukumuelewa kwa aina ya uteuzi aliokuwa anaufanya. Tukashangaa hata kwanini kwa sababu zake aliamua kuwaacha baadhi ya wachezaji wakati tulidhani ni bora sana. Mmojawapo alikuwa beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Nadhani katika hili, Kim Poulsen atatushangaza zaidi. Hasa sisi mashabiki wa soka la Tanzania ambao tumezoea kuukariri mpira. Kim atatushangaza zaidi. Ana tabia ya kuangalia kile ambacho hatuwezi kukiona kwa urahisi. Ana tabia ya kufanya anachofikiri sio kile ambacho sisi tunafikiri kwa haraka.

Kim ana uwezo mkubwa wa kuwafahamu wachezaji vema, hasa makinda. Lakini hapo hapo anajua namna ya kuingiza kizazi kipya cha wachezaji katika kikosi cha timu ya taifa. Sio tu kwamba wanaingia, lakini hapo hapo wanakwenda kucheza. Kuna mifano mingi lakini mifano ya haraka ilikwenda kwa Frank Domayo na Salum Abubakar wakati walipoitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Stars. Na hasa unapomzungumzia Domayo unabakia mdomo wazi zaidi. Domayo aliitwa katika kikosi cha Stars na kucheza akitokea katika timu ya vijana ya JKT Ruvu. Alikuwa hajagusa timu ya kwanza. Alimtoa katika kikosi cha vijana cha JKT akampanga katika kikosi cha wakubwa cha Stars.

JKT wenyewe walishangaa. Mashabiki wa Simba na Yanga nao wakashangaa. Domayo alikamata dimba kwa umaridadi mkubwa. Simba na Yanga wakaanza kukimbizana kuinasa saini yake na hatimaye Yanga wakamnasa. Kifupi Yanga walimuonea Domayo katika kikosi cha Stars. Huyu ndiye Kim. Ana jicho lake. Halafu sisi waswahili tuna macho yetu. Kinachomuepusha Kim katika lawama ni mambo matatu. Kwanza kabisa ni mzungu. Hajui sana siasa za Simba na Yanga.

Anapofanya maamuzi kama haya huwa tunamuamini moja kwa moja. Anapofanya maamuzi haya mtu kama Ndayiragije huwa tunamlaumu kwa sababu ni mswahili mwenzetu na tunaamini ameingia katika siasa za Usimba na Uyanga.

Kitu kingine kuhusu Kim ni kwamba wachezaji wenyewe ambao wanaingia katika kikosi cha kwanza kutoka kusikojulikana huwa hawamuangushi. Mfano ni kama huyo Domayo mwenyewe. Hii inampa kiburi cha kuendelea kufanya kazi yake vema bila ya kutazamana usoni na mastaa wa zamani tuliowakariri.

Lakini kitu cha tatu ni kwamba ni kwamba timu zake ucheza soka maridadi. Ziwe zile za vijana au ya wakubwa, Kim anafahamu namna ya kufundisha soka maridadi. Mara nyingi amekuwa akituziba mdomo kwa sababu hiyo. Kim anajua kufundisha soka.

Na ni katika kujua kufundisha soka, kuijua vema namna yake ya ufundishaji soka, Kim huwa anapenda vijana wadogo na ambao wanafundishika, huku wakiwa tayari kucheza mpira wake mgumu. Mpira wa Kim ni mgumu kwa wachezaji wetu. Inabidi uwe damu changa na uweze kufanya kazi ya kitumwa ili uendane na Kim. Haishangazi kuona mafaza wakishindwa kuendana na kasi yake.

Alipoita kikosi cha kujiandaa na Afcon mwaka 2012, Haruna Moshi nusura azimie kwa mazoezi magumu. Mwinyi Kazimoto akatapika pale Uwanja wa Karume. Maisha hayakuwa mazuri sana kwa wachezaji wakubwa ambao wengi wao hawapendi mazoezi magumu.

Soka la Kim linahitaji mchezaji ambaye yuko tayari kuwa na mpira, kuachia haraka, kuchukua nafasi kwa haraka kwa ajili ya kuupokea tena. Lakini kama mnapoteza inabidi muwe tayari kukaba kwa haraka na kuurudisha mpira katika himaya yenu. Kufanya hii kazi kwa dakika 90 inabidi uwe fiti. Wachezaji wakubwa wengi hawako fiti. Wanacheza kwa ajili ya uzoefu.

Kim anapenda zaidi wachezaji wanaonyambulika kwa urahisi ambao wengi unakwenda kuwapata katika kundi la damu changa. Haitashangaza kuona vijana wengi wa timu za taifa za vijana wakienda katika kikosi cha wakubwa na kucheza moja kwa moja.

Nipo Mauritania kwa sasa na kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Naona kabisa chini ya Kim kijana kama, Novatus Dismas anaingia katika kikosi cha wakubwa na kucheza. Kelvin John, Ben Starkie, Ally Msengi na wengineo wengi wataingia katika kikosi cha wakubwa na kucheza.

Ni katika nyakati hizo ndipo tutashindwa kumuelewa vema Kim. Bahati nzuri ni kwamba Stars yake itacheza soka maridadi na atatufunga mdomo. Vinginevyo tutamuona hana tofauti na Ndayiragije ambaye tulimlaumu sana kwa kutuletea akina Baraka Majogoro na Edward Charles Manyama.

Hata hivyo leo kina Majogoro na Manyama wanawindwa na watu wanaojiita mawakala wanaomiliki wachezaji ambao wamefurahishwa na viwango vyao walivyovionyesha katika michuano ya Chan pale Cameroon. Mpira wetu mara zote umejaa unafiki mwingi.

Na hapa hapa katika hili nadhani Kim atakuwa kocha ambaye atazuia fitina iliyojipenyeza katika soka letu miaka ya karibuni. Kuna watu wameanza kumiliki wanasoka wetu katika siku za karibuni.

Sio jambo baya. Lakini hawa wamekuwa wakitaka wachezaji wao waitwe na kupangwa katika kikosi cha Stars. Ndayiragije alijikuta katika wakati mgumu kwa sababu ya hawa watu. Nadhani chini ya Kim tabia hii itapata msiba kwa sababu siamini kama Kim anaweza kumchagua mchezaji kwa shinikizo la mashabiki. Ni kama nyakati zile ambapo aliwaacha nyumbani kina Boban na kwenda Ivory Coast kukabiliana na akina Didier Drogba akiwa na akina Domayo.


Imeandikwa na Edo Kumwembe