HISIA ZANGU: Simba vs Al Ahly, mechi inayofikirisha mengi

Tuesday February 23 2021
edo pic

BAADAE Simba itacheza na Al Ahly katika Uwanja wa Mkapa. Mechi tamu iliyoje. Ina mambo mengi ya kufikirisha. Mambo mengi sana. Hatujui tuanze kufikiria lipi na tumalize kwa kufikiria lipi. Yote yananogesha pambano hili.

Tuanze na ukweli huu hapa. Miezi 24 iliyopita Simba walicheza dhidi ya Al Ahly halafu wakashinda bao 1-0 pale Temeke. Al Ahly walikuwa wazuri na ndio maana waliongoza katika kundi lile. Hatuwezi kusema wabovu itakuwa ni kuwakosea heshima Simba. Mbona mechi ya Cairo Al Ahly walishinda 5-0? Walikuwa wazuri.

Lakini inafikirisha kwamba Al Ahly kuanzia pale wamekwenda kuwa mabingwa wa Afrika. Ina maana wameimarika zaidi. Watakubali kufungwa tena katika Uwanja wa Mkapa? Sio lazima. Hatuwezi kukariri matokeo yale. Litakuwa kosa kubwa lililopitiliza. Hii ni timu nyingine ya Al Ahly chini ya mchawi wa sasa wa soka la Afrika, Pitso Mosimane. Halafu hapohapo unawakumbuka siku chache zilizopita walipocheza na mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich. Sawa walipigwa 2-0 lakini walikwenda sambamba na Bayern kuanzia mwanzo hadi mwisho. Walichokionyesha kinatisha sana kama wewe ukiwa shabiki, mchezaji, kiongozi au kocha wa Simba.

Halafu inafikirisha pia kwamba baada ya hapo walicheza na Al Marreikh. Walibanwa kwelikweli mpaka kipindi cha pili. Hatimaye walifanikiwa kuilegeza mechi wakashinda 3-0. Haikuwa mechi rahisi kwao lakini walilazimisha kwelikweli. Walilazimisha mno.

Subiri kwanza. Kwanini tuizungumzie Al Ahly tu? Tuje upande wa Simba. Kuna mambo yanafikirisha pia kwa upande wa mnyama. Mambo mengi. Kwa mfano Simba nayo imeimarika kuanzia pale waliposhinda mara ya mwisho mpaka leo. Wameongeza watu wa maana na hata wale waliokuwepo wakati ule wameimarika zaidi.

Wakati ule Mmakonde Luis Miquissone hakuwepo. Mkorofi Bernard Morrison hakuwepo. Babu wa kazi, Joash Onyango hakuwepo. Chris Mugalu hakuwepo. Wameimarika zaidi na ndio maana wameongeza jeuri. Wamezifunga Plateau United na AS Vita ugenini. Simba watakubali kufungwa Uwanja wa Mkapa na Al Ahly kirahisi? Sidhani.

Advertisement

Lakini pia Simba wamefanya mabadiliko ya mtu muhimu kikosini. Kocha. Amekuja Bwana Gomes akitokea Al Marreikh. Mechi iliyopita dhidi ya Vita alionyesha mbinu za kisasa za kucheza ugenini. Hakuwa kama Patrick Aussems ambaye anadaiwa kwa kiasi kikubwa alichangia Simba kupigwa tano tano na Al Ahly na Vita wakati ule.

Katika pambano dhidi ya Vita, Simba ilikuwa na nidhamu kubwa ya ukabaji. Unategemea waonyeshe nidhamu hii katika pambano dhidi ya Al Ahly hawa ambao ni wazi watakuwa bora nyumbani na ugenini katika mechi zote za kundi lao. Gomes atawasaidia Simba? Atakuwa tofauti na Aussems? Inafikirisha sana.

Wiki moja iliyopita Al Marreikh walikuwa katika nidhamu hii hii lakini mwishowe walinyoosha mikono juu. Nataka kuona kama Simba watakuwa hawatanyoosha mikono juu. Wakati huohuo huku wakijaribu kupata ushindi kwa mara nyingine katika uwanja wa nyumbani.

Hili la kupata ushindi mwingine katika uwanja wa nyumbani nalo linafikirisha sana. Kama kuna bahati mbaya ambayo imetokea kwa Simba msimu huu basi ni kupangwa na timu mbili ambazo zilishawahi kuonja makali ya nyasi za Uwanja wa Mkapa. Al Ahly na AS Vita. Wote hawa watakuja na tahadhari zilizopitiliza kuelekea katika mechi.

Kinachofikirisha na kuchekesha ni pale ambapo Simba wamebuni kaulimbiu kuelekea katika mechi hii. Inaitwa Total War. Cha kushangaza ni kwamba Al Ahly wamejibu kaulimbiu hii kwa kutoa yao inayosema ‘We are set’ wakiwa na maana kwamba wamejiandaa.

Al Ahly sio watu wa mitandao. Inashangaza kuona wamejibu hivi. Labda kwa sababu walifungwa mechi ya mwisho kwa Mkapa. Au labda kwa sababu kwa sasa wanaongozwa na Mswahili Bwana Mosimane ambaye ana tabia kama zetu. Hatujui. Tunachojua ni kwamba wanajua sio kazi rahisi sana kupata pointi tatu katika Uwanja wa Mkapa. Kitu kingine ambacho kinafikirisha sana ni ukweli kwamba mara ya mwisho Al Ahly kuja Temeke na kupokea kisago walikuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu. Walikuwa na pointi takribani saba kibindoni. Walifungwa na Simba huku wakiwa na mechi mbili ambazo zingewapitisha katika hatua inayofuata kama wangeshinda mechi moja tu.

Leo wanaingia katika Uwanja wa Mkapa huku wakiwa na pointi tatu tu kama wapinzani wao Simba. Ina maana yeyote ambaye atashinda ataongoza kundi. Sare itawaacha wote wakiwa na pointi nne tu. Kama pambano la As Vita na Al Marreikh litakuwa na mshindi basi kundi litakuwa katika wakati mgumu. Mabingwa wetu wa Afrika watakubali matokeo mengine ambayo sio sare wala ushindi kwao? Hatuna uhakika.

Lakini hilihili lina upande mwingine wa shilingi kwa Simba. Mnyama anajua akishinda mechi hii basi hawezi kukosa pointi nne katika mechi mbili za nyumbani dhidi ya Al Marreikh na As Vita. Pointi nne tu ambazo zinaweza kumfanya apate pointi 10 na kwenda hatua inayofuata.

Endapo mnyama atafungwa Temeke leo, halafu mechi ijayo afungwe ugenini na Al Marreikh basi ghafla ushindi dhidi ya As Vita utabaki kuwa historia. Sidhani kama wapo tayari hilo litokee. Walau wapate sare leo na kisha kusubiri matokeo yoyote pale Khartoum. Huu ndio ukweli wa hesabu zao. Al Marreikh nao baada ya kuwatazama wakicheza dhidi ya Al Ahly hawaonekani kama watakuwa timu rahisi kwa Simba. Pambano la leo linafikirisha pia kuona Simba watafanya nini. Kama wakifanya maajabu mengine na kuwachapa Al Ahly, basi itainua matumaini ya Wanasimba kwamba timu yao imesogea kutoka katika hatua moja na kwenda katika hatua nyingine.

Kama hawatafanya hivyo, basi itaanza kutia shaka kama mradi wao wa kuwa miongoni mwa timu bora za Afrika unakwenda sawa. Wanahitaji kusogea kutoka pale walipokuwa miezi 24 iliyopita. Ushindi dhidi ya As Vita ugenini ni ishara nzuri. Kichapo kutoka kwa Al Ahly nyumbani itakuwa ishara mbaya.

Rafiki zetu Wacongo TP Mazembe katika ubora wao hakuna timu ya Waarabu ambayo iliwahi kuchukua pointi tatu pale Lubumbashi. Labda nyakati hizi ambazo TP Mazembe imeanza kusuasua. Simba wanahitaji kurudia kile walichokifanya miezi 24 iliyopita bila ya kujali Al Ahly wapo katika hali gani kwa sasa. Wataweza? Hatujui.

Tumtakie kila la heri mnyama. Ana kazi kubwa ya kufanya. Binafsi sijapenda jinsi ambavyo pambano limekuja mapema kwao. Al Ahly bado hajafunga hesabu zake katika kundi na atataka aendeleze hesabu zake vyema. Wakati mwingine inafikirisha kwamba huenda Simba wakawa na pambano zuri Cairo kuliko Dar kwa sababu pambano hilo la mwisho Al Ahly atakuwa amefunga hesabu.

Lakini huu pia haukuwa wakati mwafaka kwa Simba kucheza na Al Ahly. Hawa jamaa bado wana moto wa Qatar walikokwenda kucheza Klabu Bingwa ya dunia. Wakati mwisho sio fair kutoka kucheza Klabu Bingwa ya Dunia halafu ukatua Temeke kucheza na klabu ya Ligi Kuu Bara. Sio haki.


Imeandikwa na Edo Kumwembe

Advertisement
​