Prime
JUDGEMENT DAY: Simba vs Bravos, Yanga vs Al Hilal utamu uko hapa

Muktasari:
- Unaweza kusema leo ni siku ya hukumu, sio kwa timu hizo tu za Tanzanuia bali hata huko Ulaya nako kuna mechi za uamuzi zitakazopigwa na kuamua hatma za timu husika.
HAKUNA namna nyingine ambayo mashabiki wa Yanga na Simba wanachotaka kusikia leo Jumapili zaidi ya timu hizo kushinda ugenini.
Unaweza kusema leo ni siku ya hukumu, sio kwa timu hizo tu za Tanzanuia bali hata huko Ulaya nako kuna mechi za uamuzi zitakazopigwa na kuamua hatma za timu husika.
Kule England, Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ambaye katikati ya wiki alikuwa na kilio cha mipira inayotumika kwenye Carabao Cup haiendani na ile ya Premier League na ndiyo sababu ya kuchapwa nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Newcastle United mchezo wa nusu fainali ya kwanza, leo ana nafasi ya kufuta machozi atakapowakaribisha watoto wa Ruben Amorim, Manchester United katika mchezo wa Kombe la FA raundi ya tatu.
Mchezo huo utakaoanza saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, umebeba hisia kubwa ukizingatia kwamba wikiendi iliyopita ilibaki kidogo Man United iikande Liverpool kwenye Premier kama sio uzembe wa beki wake na nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Harry Maguire kukosa nafasi ya wazi kufunga bao la ushindi dakika ya mwisho. Mechi ikaisha 2-2.
Man United ni kama imeamka huku ikionyesha upinzani wa kweli zinapokuja mechi kubwa, hivyo Arsenal wana kazi ya ziada kufanya leo kuhakikisha wanaifunga Man United na kufuzu raundi ya nne ya michuano hiyo ambayo wao ndio vinara wa kubeba taji hilo mara 14 wakifuatiwa na Man United (13) ambao ni mabingwa watetezi.
Tukitoka England, kule Saudi Arabia kwenye Dimba la King Abdullah Sport City kuanzia saa 4:00 usiku, itapigwa El Clasico matata sana, Real Madrid ikipambana na Barcelona katika fainali ya Super Cup.
Fainali ya mwaka jana iliyochezwa nchini humo kwenye Dimba la Al -Awwal Park, Real Madrid iliibuka na ushindi wa mabao 4-1, huku Vinicius Junior akipiga hat trick. Ubabe huo wa Real Madrid umekoma msimu huu kwani imeshuhudiwa mechi ya kwanza La Liga ikifungwa na Barcelona 4-0. Kabla ya hapo, mchezo wa kirafiki kipindi cha pre-season, Barcelona ilishinda 2-1. Leo kazi ipo.
Sasa basi, kama wewe si mpenzi wa soka la Ulaya, turudi katika soka letu kivyetu vyetu ambapo wawakilishi wetu, Simba na Yanga watakuwa na karata muhimu katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Uzuri wa mechi hizo huna sababu ya kuzikosa kushuhudia kwani zimepangwa muda rafiki. Wanaanza Simba kucheza saa 1:00 usiku dhidi ya Bravos do Maquis nchini Angola. Mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A ukimalizika utapata muda wa kujadili na kubishana na mtani wako huku ukiisubiri Yanga ikikaribishwa na Al Hilal ya Sudan katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wa Kundi A utakaochezwa katikaUwanja wa Cheikha Ould Boïdiya nchini Mauritania.
BRAVOS v SIMBA
Simba imeenda Angola ikiwa na lengo ya kubeba pointi tatu na ikishindikana basi moja lakini sio mikono mitupu.
Kocha Fadlu Davids anaamini mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa 11 de Novembro, umebeba hatma yao kwa asilimia kubwa kutokana na hivi sasa kuwa nafasi ya pili kundini kwa kufikisha pointi tisa sawa na CS Constantine wanaoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Bravos ambao wanacheza na Simba, wanashika nafasi ya tatu na pointi zao sita huku CS Sfaxien wanaocheza na Constantine leo hawana kitu kutokana na kupoteza mechi zote nne. Unaweza kuwaita vibonde wa kundi.
Ikitokea Constantine imeichapa Sfaxien leo jambo linaloonekana linaweza kutimia kwani mchezo wa kwanza wenyeji Sfaxien walichapwa nyumbani 1-0, basi moja kwa moja timu hiyo inafuzu robo fainali. Kazi inabaki kwa Simba na Bravos jambo ambalo linaifanya Simba kuhakikisha leo inaifunga Bravos au kupata sare ili mechi ya mwisho nyumbani Januari 19 dhidi ya Constantine iwe mtelezo.
MECHI YA DK 45 MOJA
Bravos na Simba ambazo tayari zimekutana katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar na wenyeji kushinda 1-0 kwa bao la Jean Charles Ahoua dakika ya 27 kwa penalti, rekodi zinaonyesha kwamba zote zimekuwa zikitumia vizuri kipindi cha kwanza kusaka ushindi kwani mabao yao asilimia kubwa yamepatikana muda huo.
Simba iliyofunga mabao manane katika mechi sita kuanzia hatua ya mtoano hadi sasa makundi, sita kati ya hayo yamepatikana kipindi cha kwanza huku mawili pekee yamefungwa kipindi cha pili. Hiyo inaonyesha moja kwa moja nguvu ya Simba ipo wapi.
Wachezaji wanaocheza eneo la kiungo wakiongozwa na Kibu Denis mwenye mabao matatu na Jean Charles Ahoua mawili kati ya nane yaliyofungwa na Simba kuanzia mtoano hadi sasa, wameonekana kuibeba zaidi timu hiyo na ndiyo tumaini lao kubwa lipo hapo.
Ukiangalia hata namna kikosi cha Simba kilichoenda Angola, utakubaliana na hilo kwani nusu ya wachezaji waliosafiri ni viungo ambao ni 11, huku nafasi nyingine zikikamilisha wachezaji wengine kwa jumla yake wapo 22.
Kwa upande wa Bravos ambayo msimu huu haijapoteza nyumbani katika mechi nane za Caf ilizocheza ikishinda zote, nayo kipindi cha kwanza kwao ndiyo wanakitumia vizuri kupata ushindi. Timu hiyo iliyofunga mabao 12 kuanzia hatua ya mtoano ikicheza mechi nane, saba yamepatikana kipindi cha kwanza na matano cha pili.
Wachezaji ambao wanaonekana kuwa hatari ndani ya Bravos ni Jo Paciencia na Francisco Cabuema Matoco maarufu kwa jina la Macaiabo ambao kila mmoja ana mabao tatu kati ya 12 yaliyofungwa na timu hiyo.
Ubora wa Ahoua unamfanya kocha wa Bravos, Mario Soares kuweka wazi kuwa nyota huyo ndiye anayemuhofia zaidi akibainisha kwamba ni mchezaji mzuri kutokana na kiwango chake japo anaamini Simba kiujumla imeimarika zaidi tofauti na mchezo wao wa kwanza waliokutana Kwa Mkapa.
“Nafikiri ni mchezo unaoweza kutoa taswira kwa timu zote mbili katika harakati za kufuzu hatua inayofuata, Ahoua ni mchezaji mzuri aliyeleta mabadiliko chanya, lakini tutapambana pia kuhakikisha tunapata ushindi nyumbani,” alisema.
Ahoua namba zake zinambeba zaidi kwani kwa mujibu wa mtandao wa fotmob.com, kiungo huyo ndiye kinara wa kutengeneza nafasi katika kikosi cha Simba hatua ya makundi akiwa amefanya hivyo mara tisa na kiujumla anashika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo nyuma ya kinara Yassine Labhiri wa RS Berkane aliyefanya hivyo mara 14.
Pia Ahoua ndiye amehusika kwenye mabao mengi ambayo ni manne ndani ya kikosi cha Simba hatua ya makundi akifunga mawili na asisti mbili. Kwenye hatua hiyo kwa ujumla anashika nafasi ya pili nyuma ya kinara Ismail Belkacemi wa USM Alger akiwa amehusika na mabao sita.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids, alisema: “Hatujapata muda mrefu wa kupumzika lakini bado tunaendelea kuishi katika malengo tuliyojiwekea, umuhimu wa mchezo wetu wa Jumapili sio kwetu pekee bali hata kwa wapinzani tutapambana ili kushinda na kupunguza presha ya mechi ya mwisho. Tumepata mapokezi mazuri kutoka kwa watu wa Angola, timu ipo kwenye hali nzuri. Hali ya hewa ni kama Dar es Salaam, tupo tayari kwa mchezo.”
Kiungo wa Simba, Debora Mavambo ambaye ni mzaliwa wa Angola, alisema: “Utakuwa mchezo mgumu natambua Bravos wanacheza nyumbani na wanahitaji alama tatu ila tunajua malengo ya Simba ni kufanya vizuri.”
Mavambo mwenye uraia wa Angola na Congo, akijiunga na Simba msimu huu akitokea Mutondo Stars ya Zambia, soka lake kwa kiasi kikubwa amecheza Angola akizitumikia klabu za Académica Petróleos do Lobito na Ferrovia Huambo hivyo ni amerejea nyumbani kuipambania Simba.
Licha ya kuonekana itakuwa ni kama mechi ya kipindi cha kwanza kutokana na rekodi zilivyo, lakini pia suala la kushuhudia nyavu kutikiswa lipo kwa asilimia kubwa kwani Bravos ikiwa nyumbani katika michuano ya Caf msimu huu haijawahi kuondoka bila ya bao. Ilianza kuifunga Coastal Union 3-0, kisha Lupopo 1-0. Hatua ya makundi ikaichapa Sfaxien 3-2 na ushindi kama huo ikaupata mbele ya Constantine.
Simba yenyewe mechi tatu za ugenini ilizocheza kuanzia ile ya mtoano dhidi ya Al Ahli Tripoli iliyotoka 0-0, mbili imefunga bao dhidi ya Constantine ilipofungwa 2-1 na ushindi wa 0-1 mbele ya Sfaxien.
SHOO YA WABUKINABE
Katika mechi ya leo, kipenga kitapulizwa na Jean Ouattara akisaidiwa na Seydou Tiama atakayekuwa namba moja na Levy Sawadogo msaidizi namba mbili, wakati mwamuzi wa akiba ni Hamidou Diero.
Rekodi zinaonyesha mwamuzi Jean Ouattara ni mzoefu wa mechi za CAF akitumika zaidi kucheza mechi za timu za taifa zikiwamo za mtoano za Afcon, huku akitajwa sio mtu anayependa sana kutoa kadi uwanjani, lakini huwa ni mkali wachezaji wanapozingua.
AL HILAL v YANGA
Hakuna namna kwa Yanga kurudi Dar bila ya pointi kwani inawalazimu kuichapa Al Hilal iliyofuzu robo fainali mapema ili kumalizana kikubwa na MC Alger, Januari 18 hapa nyumbani.
Ulazima wa Yanga kushinda leo unatokana na matokeo ya MC Alger iliyoyapata juzi Ijumaa ikiwa nyumbani dhidi ya TP Mazembe iliposhinda 1-0.
Ushindi huo wa MC Alger unaufanya mchezo wa leo kwa Yanga kuwa wa lazima kushinda ili kufikisha pointi saba na kuifanya kuwa nyuma ya MC Alger kwa tofauti ya pointi moja hivyo itawataka mechi ya mwisho pia kushinda nyumbani. Suala la Yanga kushinda leo mbele ya Al Hilal linawezekana kutokana na wapinzani wao kwamba hawana cha kupoteza zaidi ya kutaka kulinda heshima ya kumaliza kundi kileleni na heshima hiyo wanaweza kuipata hata mchezo wa mwisho mbele ya TP Mazembe ambayo nayo haina cha kupoteza baada ya kutokuwa na nafasi ya kufuzu robo fainali.
Kwa sasa TP Mazembe inashika nafasi ya mwisho katika kundi lake ikiwa na pointi mbili. Itamalizana na Al Hilal nyumbani Januari 18 katika mchezo wa kukamilisha ratiba tu kwa wote.
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic, anauona ugumu wa kukabiliana na presha iliyopo kuhakikisha anakusanya pointi sita zitakazowavusha kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo hivyo alichoamua kufanya ni kufumba macho, hataki kuona wapinzani wanafanya nini zaidi ya kuiandaa timu yake ya ushindi.
“Simuangalii mpinzani ili kuwa bora, napambana kuhakikisha najenga timu yenye ushindani, ninachokifurahia zaidi ni namna timu yangu inavyoimarika na ipo kwenye morali nzuri, hivyo naamini kila kitu kinawezekana kwa kushindana sisi wenyewe kwa kuboresha timu yetu.
“Tunakutana na mabingwa wa ligi kutoka mataifa tofauti na kuna timu ambazo zina uzoefu mkubwa, tumecheza na TP Mazembe ambayo imeshatwaa mataji ya michuano hii, sasa tunajiandaa kukutana na timu nyingine bora na kongwe kwenye michuano hii, hatutakiwi kuangalia nini wanafanya zaidi kujipanga ili tuwe washindani,” alisema Ramovic
Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge, alisema: “Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa na umuhimu mkubwa kwao, lakini kwa upande wetu, tunahitaji kujiandaa kwa hali yoyote. Siwezi kujivunia mapema. Wachezaji wangu watahitaji kupumzika kidogo kabla ya michezo inayofuata.”
Kauli hiyo ya Ibenge inatokana na ukweli kwamba kufuzu kwake mapema hana cha kupoteza katika mechi mbili zilizobaki, huku akisema anataka kuwapumzisha mastaa wake kwa ajili ya kukusanya nguvu za kupambana robo fainali.
PACOME KAIBEBA MECHI
Kwa mujibu wa mtandao wa fotmob.com, umemtaja Pacome Zouzoua kuwa ndiye mchezaji wa Yanga aliyetengeneza nafasi nyingi katika mechi nne za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa nazo nane, sawa na wastani wa nafasi mbili kwa mchezo akifuatiwa na Aziz Ki Stephane ambaye ametengeneza nafasi saba.
Hata hivyo bahati mbaya ya Pacome ni kwamba nafasi hizo zote nane alizotengeneza, hazijaweza kubadilishwa kuwa mabao lakini kama washambuliaji wakiwa makini kutokana na ubora wa kiungo huyo, inaweza kuwa faida kubwa kwao. Wakati Pacome akitengeneza nafasi hizo, mshambuliaji Clement Mzize ameonekana kuwa na namba nzuri katika ufungaji kuanzia mtoano hadi sasa makundi huku mabao yale mawili dhidi ya TP Mazembe mechi iliyopita yakimfanya kufikisha matano.
Ushirikiano wa Mzize na Pacome huku Clatous Chama akirejea, unaweza kuipa faida Yanga katika mchezo wa leo.