JICHO LA MWEWE: Yanga itaweza kumzuia Mayele asiondoke?

ASUBUHI kitandani pale Johannesburg nilikuwa nasikiliza watangazaji wa Afrika Kusini wakimsifia straika wa Yanga, Fiston Mayele. Namna alivyofunga bao moja na kupika jingine dhidi ya Marumo Gallants katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kasi yake katika ufungaji wa bao la kwanza. Ufuatiliaji wake wa mpira hata baada ya kipa kupangua na kisha akafunga kwa utulivu viliwavutia. Lakini zaidi kasi yake katika bao la pili, inatokea mara chache kwa mshambuliaji kuwa na majivuno ya kasi yake.

Namna ambavyo aliupiga mpira mbele wakati ndilo eneo alililokuwepo beki wa Marumo, kisha akampita kama amesimama na kwenda kupika bao la Kennedy Musonda. Iliwashangaza watangazaji wa kituo kile. Walistaajabu.

Inawezekana kwa watangazaji ilikuwa mara yao ya kwanza au ya pili kumuona Mayele. Lakini kuna Papa wakubwa ambao watakuwa wamemfuatilia nyuma ya hapo. Hawa ni timu kubwa za Afrika, pia inawezekana na baadhi ya timu za Asia.

Hawa Papa, au tuwaite samaki wakubwa watarudi nyuma zaidi. Watatazama na kumuona Mayele akiwa na mabao sita katika michuano hii ya Shirikisho. Watatazama na kumuona kuwa ni Mfungaji Bora katika Ligi Kuu Bara. Msimu huu anaongoza, msimu uliopita alipitwa kwa bao moja tu na George Mpole aliyekuwa Geita Gold.

Kabla ya hapo msimu mmoja nyuma alikuwa kwao DR Congo na alishika nafasi ya pili ya ufungaji. Haya ya nyuma inawezekana ni katika kuongeza wasifu tu, lakini zaidi haya anayofanya sasa. Zaidi ya yote ni kwamba ukikusanya mabao yake katika video moja utagundua kwamba jamaa habahatishi.

Yanga wajiandae kupokea ofa nzuri kutoka katika klabu ya juu yao zaidi ambayo itamhitaji Mayele. Ninaposema klabu ya juu yao zaidi simaanishi klabu ambayo ilianzishwa kabla ya Yanga. Hapana. Namaanisha klabu ambayo ina kipato kikubwa zaidi ya Yanga.

Ninaposema klabu ambayo ipo juu yao zaidi simaanishi kwamba ni klabu ambayo nchini kwake imetwaa mataji mengi kuliko Yanga walivyotwaa nchini. Inaweza kuwa klabu mpya kama Pyramids lakini wana pesa nyingi kuliko Yanga.

Hapa utakuwa mtihani kwa watu wa Yanga. Biashara wataitatamani, lakini kubaki na Mayele watatamani. Moja kati ya sababu ambayo watatamani kufanya biashara ni ukweli kwamba inawezekana walimpata Mayele kwa bei rahisi halafu ghafla kuna mtu anaweka dola laki saba mezani.

Wataulizana lengo la kubakia na mchezaji kama yeye. Lakini hapo hapo ikumbukwe kwamba mchezaji mwenye ana maslahi yake na klabu ambayo itamtataka. Inaweza kumtangazia mshahara wa dola 25,000 kwa mwezi. Yanga analipwa pesa hiyo? Vipi kuhusu ‘signing fee’ yake binafsi? Kama ni dola laki moja?

Kitu ambacho unaweza kuwakubalia Yanga endapo wataipiga chini ofa kama hiyo ni ukweli kwamba Mayele ni miongoni mwa sababu za wao kupata pesa nyingi kutoka CAF mpaka sasa. Kila hatua waliyopiga mpaka kufikia hapa wamepata pesa nyingi.

Lakini tatizo ni kupambana katika habari ya maslahi binafsi ya mchezaji mwenyewe. Wakati mwingi klabu inalazimika kukubali kwa shingo upande kumuachia mchezaji aende anakotaka kwa sababu haiwezi kushindana na aliyeweka mezani mshahara wa dola 25, 000 kwa mwezi.

Hapa ndipo samaki mkubwa anapomla samaki mdogo. Imekuwa hivi hata kwa soka letu la ndani. Klabu ndogo zinalazimika kuwapoteza wachezaji wake wanaokimbilia kwenda Simba, Yanga na Azam kwa sababu haziwezi kuwalipa kile ambacho hawa wakubwa wanaweka mezani kama maslahi yao binafsi. Samaki mkubwa anamla samaki mdogo.

Kitu kibaya zaidi kwa Yanga linapokuja suala la Mayele ni kwamba washambuliaji wapo wachache siku hizi duniani. Mshambuliaji anayeweza kukuhakikishia mabao sita katika michuano ya Shirikisho wapo wachache. Mabao haya ni achilia mbali yale ambayo aliwafunga rafiki zetu Zalan katika mechi za awali.

Wazungu huwa wana msemo wao unaosema ‘The Golden Fish has no hiding place’. Wanamaanisha kwamba ‘Samaki mzuri hawezi kujificha’ kila atakapokimbilia ataonekana kuwa tofauti na wenzake. Yanga haiwezi kumficha Mayele kwa muda mrefu. Hivi tunavyoongea klabu zitakuwa zinapanga kupiga simu kwake.

Amejipeleka katika masoko mengi lakini juzi alijipeleka katika soko la Afrika Kusini mbele ya kamera za Supersport. Pale kuna wateja ambao wana uhaba wa washambuliaji na pesa wanazo. Hawa ndio rafiki zangu kina Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates na wengineo.

Kitu kibaya zaidi kwa Yanga ni kwamba ikitokea watamuuza Mayele watapata shida kumpata mshambuliaji wa aina yake. Hili ndio tatizo kubwa la soko letu kwa sasa. Unaweza kuuza kwa wema lakini ukakumbana na tatizo la kuziba nafasi.

Tatizo hili lipo hasa kwa kwa mshambuliaji wa aina ya Mayele pamoja na makipa. Kuwapata waliokomaa na ambao wapo tayari kwa mapambano huwa ni nadra. Na ndio maana huwa wanaweza kudumu katika klabu moja kwa muda mrefu huku maslahi yao yakipewa kipaumbele.

Baada ya kunogewa na kila kilichotokea msimu huu katika michuano ya CAF, Yanga watataka maisha yaendelee kuwa hivi kwa muda mrefu. Moja kati ya vita kubwa ambayo watalazimika kuipigana ni kuendelea kubaki na wachezaji wako walio bora kama Mayele.

Hapa ndipo klabu huwa inapimwa ubavu kama na yenyewe imeingia katika orodha ya klabu kubwa au la. Kuna tofauti kati ya klabu kubwa na klabu kongwe. Klabu kongwe ni ile ambayo imeanzishwa zamani. Klabu kubwa ni ile ambayo ina nguvu kubwa za kiuchumi na pia ina mataji mengi.

Majuzi hapa Simba na Yanga walipimwa katika ukubwa wao wakati klabu za Berkane ya Morocco na Al Ahly ya Misri zilipogonga hodi kuwataka Luis Miquissone, Clatous Chama na Tuisila Kisinda. Hakukuwa na aliyekuwa na ubavu wa kuwazuia wasiondoke.

Hatujui hodi ikigongwa sasa hivi itakuaje, hasa kwa rafiki zangu kama ikitokea kuna mkubwa atamtaka Fiston Mayele. Mashabiki na wanachama watataka kujua kama viongozi wao wana ubavu wa kutosha wa kuendelea kubakia na mshambuliaji kama huyu.

Kwa sasa gtusiudanganyane. Wapo wachache katika soka letu la ndani bara la Afrika. ukiruhusu wako aondoke usitegemee kama utampata wa mwingine kwa urahisi. Labda kama na wewe utajigeuza kuwa samaki mkubwa. Wenzetu huwa hawategemei uhamisho huru. Wananunua mchezaji.