JICHO LA MWEWE: Simba alivyoshikwa sharubu na mtani kwa mara nyingine

TTUANZIE wapi? Tuanzie wiki chache zilizopita wakati niliposisitiza kwamba kama Yanga wangekuwa wamecheza mechi sita za Ligi Kuu huenda wangewatoa Rivers ya Nigeria katika mechi ya awali ya kufukuzu Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kwanini nilisema hivi? Kwa sababu Yanga ina wachezaji wazuri. Kwa kiwango gani? Sijui lakini ni wazuri kuliko waliokuwa nao msimu uliopita na misimu miwili iliyopita. Niliwaona wachezaji hawa kambini Morocco. Nikawaona tena Nigeria.

Walichohitaji? Walihitaji mambo mawili. Kwanza walihitaji kurudi kikosini kwa Khalid Aucho, Fiston Mayelle na Djuma Shaban. Lakini zaidi walihitaji kuwa fiti na pia kutengeneza kitu cha pamoja uwanjani. Baadaya haya Yanga itakuwa na timu ya kushindana na timu nyingi barani Afrika bila ya kujali matokeo yatakuaje. Na ndicho kilichotokea juzi jioni katika Uwanja wa Mkapa pale Temeke. Yanga ilikuwa inahakisi kile ambacho nilikuwa nimekifikiria. Ilikutana na watani zao Simba na kuondoka na ushindi wao wa pili mfululizo dhidi ya watani wao katika uwanja huo. Sahau pambano la Kigoma ambalo lilichezwa mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Ilikuwa mechi iliyopoa nje ya uwanja. Sijui TFF walifikiria nini kuweka kiingilio cha chini kuwa shilingi 10,000. Nadhani kuna watu walijidanganya kwamba baada ya Yanga na Simba kusajili mastaa akina Peter Banda, Fiston Mayelle, Khalid Aucho, Kanoute na wengineo basi mashabiki wangepambana kwa kila hali. Haikuwa hivyo. Mashabiki wengi waliweka mgomo baridi wa kutokwenda uwanjani.

Mashabiki walibaki nyumbani katika televisheni zao na kama ilivyo kwa mashabiki wachache waliojitkeza uwanja wote walishuhudia Yanga ikianza pambano kwa kasi na kujipatia kona ya kwanza katika dakika ya kwanza tu ya pambano hilo.

Ilikuwa ikiashiria kitu kilekile ambacho kilijengeka katika miaka ya karibuni. Yanga inajiandaa zaidi katika pambno hili kimwili na kiakili kuliko Simba. Inaiheshimu zaidi Simba na kutumia nguvu nyingi kujaribu kushinda pambano kuliko ambavyo Simba inavyojiandaa.

Haikushangaza ilipopata bao la kwanza dakika ya 11. Ni dakika ile ile ambayo, Zawadi Mauya alifunga bao la kuongoza na la ushindi katika pambano la mwisho la uwanja huu baina yao. Safari hii Yanga hawakuhitaji kiungo kwa ajili ya kufunga. Walihitaji mshambuliaji kufunga bao na ni kweli kwamba safari hii wamesajili washambuliaji wawili wazuri, Herietier Makambo na Fiston Mayelle.

Alikuwa ni Mayelle ndiye aliyefunga bao. Lilianzia wapi? Kwa kipa wao mpya, Djigui Diarra. Walau lango la Yanga lipo salama kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote. Kipa wao anajua kudaka, anajua kusambaza mipira kwa miguu. Bao hili lilianzia kwake baada ya kupiga pasi ndefu iliyotua kwa Faridi Mussa ambaye alimchambuka vema Wawa Paschal na kutupia pasi kwa Mayelle ambaye alimalizia vema bila ya kutulia akimuacha, Aishi Manulaakiwa hana la kufanya.

Baada ya Mayelle kwenda kushangilia Kicongo na kumaliza, kuanzia hapo tukaanza kutazama mpira. Bahati nzuri kama ilivyo katika mechi nyingine kubwa na nzuri huko duniani, pambano hili liliamuliwa na eneo la kiungo. Hapo Yanga walikuwa bora zaidi. Fei Toto alikuwa wa moto akipima pumzi za Thadeo Lwanga mara nyingi lakini ilitokana na jinsi ambavyo Khalid Aucho na Yannick Bangalawalivyoliteka eneo la kiungo kuwaacha Sadio Kanoute na Larry Bwalya wakishindwa kutengeneza mashambulizi ya Kisimba zaidi ambayo tumeyazoea kwa muda mrefu.

Katika hili la Kanoute pamoja na wageni wawili, Papa Ousmane Sakho na Peter Banda ndipo unapozuka mjadala kama Simba imeziba mapengo yaClatous Chama na Luis Miquissone kwa ufasaha. Hii ilikuwa mechi ya pili mfululizo Simba inapoteza katika uwanja huo baada ya kuchapwa na TP Mazembe.

Wageni wapya ni hodari na wanaweza kuziba mapengo ya Chama na Miquissone? Kwa sasa bado lakini kumbuka kwamba hata Mmakonde na Chama walianza taratibu kuingia katika soka la Simba na baadae wakakomaa zaidi kwa kucheza mechi nyingi. Banda, Kanoute na Sakho ni mafundi wa mpira. Wanahitaji muda zaidi. Bahati mbaya pia kwao ni kwamba wametua katika soka lenye presha hapa nchini. Muda si mrefu watajitengenezea ufalme wao. Lakini kwa sasa wanaotakiwa kufukia mashimo na kuvaa ufalme kwa haraka ni Larry Bwalya na Ben Morrison. Haikuwa mechi nzuri sana kwa Sakho, Kanoute na Banda mwenyewe ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Sakho. Hata hivyo hili lilikuwa pambano lao la kwanza la watani wa jadi. Yanga ilikuwa na wachezaji wazoefu zaidi katika eneo la kiungo.

Mchezaji mwenye uzoefu aliyeikwamisha Simba ni Chris Mugalu. Huyu amekuwa akiiangusha Simba tangu mechi za kimataifa. Sijui ni kitu gani kinamtokea Mugalu lakini katika mechi zake za kwanza baada ya kuingia Simba alionekana kuwa tishio hasa. Sijui ni kitu gani kinamtokea.

Vinginevyo Yanga walikuwa wameonyesha nidhamu kubwa katika ulinzi pindi Simba walipokuwa wanamiliki mpira. Ndiyo, vipo vipindi ambavyo Simba walimiliki sana mpira lakini ubunifu binafsi ulikuwa ziro lakini pia Yanga walitengeneza kuta mbili ngumu kupitika.

Kama vile haitoshi Yanga walikuwa wazuri wakiwa na mpira. Walikuwa hawabutui. Aucho ni fundi hasa wa mpira ambaye kuna nyakati ambazo Simba walidhaniwa wanamtaka lakini mtu mmoja alininong’oneza kwamba walikuwa hawamtaki Aucho kwa sababu umri umeenda.