JICHO LA MWEWE: Niyonzima, Kwaheri 'Berghamp' wa Gisenyi

Tuesday July 20 2021
jicho niyonzima pic
By Edo Kumwembe

DENNIS Bergkamp aliwasili Arsenal mwaka 1995 akitokea Inter Milan. Alinunuliwa na kocha aliyeitwa George Graham. Kuanzia hapo aliacha alama kubwa Arsenal. Waingereza waliamini Bergkamp aliifanyia Arsenal mambo mawili makubwa.

Kwanza, alikuwa mchezaji mkubwa kutoka Udachini na Arsenal walikuwa ovyo nyakati hizo. Kuingia kwake Arsenal inaaminika kuliwashawishi wachezaji wengine wakubwa waamini kwamba kumbe unaweza kwenda Arsenal. Kwamba kumbe na wao bado ni timu ya maana. ‘Kama Bergkamp kaenda na kacheza sisi ni nani tusiende?’

Halafu Bergkamp akafanya kazi nyingine muhimu Arsenal. Alipoingia Arsenal akakuta wanacheza soka la Kiingereza zaidi. Akiwa ni mchezaji aliyezaliwa na kipaji maridhawa kisicho na mfano akapeleka soka lililoilainisha Arsenal. Akapeleka soka maridadi.

Mabao maridadi, chenga maridadi, pasi za mwisho maridadi, kuwaunganisha wenzake kwa umaridadi na mengineyo. Aliwatoa Arsenal katika Uingereza akawapeleka katika Ubrazil, katika udachi, katika Uargentina. Arsenal hawatamsahau. Alikuwa mchezaji pekee ambaye hakusajiliwa na Arsene Wenger, lakini bado akatamba katika zama za Mfaransa huyo.

Achana na hilo la kwanza, hili la pili ndilo ambalo mchezaji anayeitwa, Haruna Niyonzima alipeleka Yanga. Alhamisi iliyopita Yanga walimuaga Haruna katika pambano lao la Ligi Kuu dhidi ya Ihefu. Ni mchezaji ambaye watamkumbuka kwa miaka mingi ijayo.

Alitua Yanga mwaka 2011 akiwa mmoja kati ya wachezaji mastaa katika soka la Rwanda. Alihitaji ruhusa ya Rais Paul Kagame kuja kucheza Yanga. Kisa? Kagame alikuwa anamchukulia kama mwanae wa kumzaa. Na kumbuka alikuwa anacheza katika klabu yake ya APR.

Advertisement

Haruna alipotua Yanga alifanikiwa kwa kiasi kubwa kuibadilisha timu ndani ya uwanja. Timu ikaanza kucheza kama yeye alivyotaka. Yanga wanajulikana kwa soka la kasi na la moja kwa moja, lakini Haruna alikuja kuwatuliza.

Waliokuwa wanaumia zaidi walikuwa mashabiki wa Simba kwa sababu waliamini Haruna alikuwa ni mchezaji wao, lakini ambaye alikuwa anavaa jezi ya Yanga. Staili yake ya soka ilionekana kuifaa zaidi Simba kuliko Yanga.

Miaka nenda rudi Yanga wamekuwa wakitoa wachezaji wenye kasi pembeni kwa sababu wanapenda soka la mbio na matokeo. Simba wanapenda soka la kutandaza chini na haishangazi kuona wanajulikana kwa jina la Lunyasi.

Haruna kwa kiasi kikubwa aliisaidia Yanga katika kumiliki mpira zaidi. Sio kwamba Yanga haijawahi kuwa na viungo wanaotandaza sana soka, hapana, wamewahi kuwa na kina Athuman China na wengineo lakini kabla ya ujio wa Haruna hawakuwa na mchezaji wa aina hiyo.

Alipotua fundi mwingine kutoka Zimbabwe, Thabani Scara Kamusoko, Haruna aling’ara zaidi. Hawa ndio walituletea staili ya ‘Kampa kampa tena’ ambayo iliibadili kabisa Yanga na kuifanya icheze staili ya Barcelona na kuondoka na staili ya mbio.

Haruna hana rekodi nzuri katika ufungaji wala pasi za mwisho lakini ana maudhi mengi kwa adui wakati anapoisaidia Yanga katika umiliki wa mpira na kupiga pasi muhimu. Sawa, hatakumbukwa kwa kuifungia Yanga mabao mengi, lakini atakumbukwa kwa kuingiza staili yake ya uchezaji kwa wachezaji wengine.

Baadaye Haruna aliondoka zake na kwenda katika timu ambayo awali ilidhaniwa kwamba ilikuwa mwafaka kwake zaidi ya Yanga. Alienda kwa watani wao Simba. Hiki ni kitu ambacho baadhi ya mashabiki wa Yanga hawataweza kumsamehe.

Hata wakati alipoagwa Alhamisi iliyopita kuna mashabiki walikuwa na kinyongo na hawakutaka klabu yao imuage. Hili ndilo doa pekee ambalo Haruna hataweza kulifuta kamwe katika maisha yake ya soka. Mashabiki wa Simba na Yanga huwa hawasamehi kirahisi kama ulivuka mtaa mmoja kwenda mwingine.

Ndicho kitu hiki hiki ambacho kimeendelea kumtesa Ibrahim Ajibu Migomba. Anataka kurudi Yanga, na kuna watu wa Yanga wanataka kumrudisha lakini kuna kundi kubwa halimtaki. Kwanini aliwaacha wakati wanamuhitaji akarudi Simba?

Mashabiki hawa hawa wameendelea kumhoji Haruna, kwanini aliachana na wao akaenda kufuata pesa za Mohamed Dewji katika kipindi ambacho Yanga walikuwa wanamuhitaji kama roho? Mara nyingi mashabiki hawasamehi.

Kitu ambacho wanasahau ni ukweli kwamba wachezaji sio mashabiki. Wachezaji ni wafanyakazi kama wafanyakazi wengine. Ambao wanamhukumu Haruna kwa kucheza Simba wanakosea. Mpira ni kazi yake. Simba waliweka ofa nzuri mezani kwake kuliko Yanga. Angefanya nini zaidi?

Hata hivyo, mambo hayakwenda vema kwa Haruna akiwa na Simba. Kwanza kabisa alikumbwa na majeraha. Lakini hapo hapo ikumbukwe kwamba Simba ilikuwa imesheheni mastaa wengi ambao walipunguza umuhimu wake klabuni tofauti na alivyokuwa Yanga.

Kumbukumbu kubwa ambayo aliwaachia Simba ni pambano dhidi ya AS Vita ya Congo wakati alipocheza kandanda safi na kisha kusababisha bao la dakika za majeruhi la Clatous Chama. Aliuruka mpira kwa umaridadi mkubwa na ukamuhadaa kipa wa Vita. Chama akafunga kiurahisi. Hakuna kumbukumbu kubwa kwa Haruna Simba zaidi ya ile.

Mkataba wake ulipomalizika alirudi kwao Gisenyi, lakini Yanga chini ya GSM walimfuata na kumrudisha klabuni kwa mara nyingine tena. Kurudi kwake kuliwaganya mashabiki, lakini hawakuwa na jinsi kwa sababu wakati huo timu yao ilikuwa hoi baada ya tajiri wao Yusuph Manji kupata matatizo.

GSM waliamua kuanza kuvaa majukumu mengine yasiyowahusu nje ya mkataba wao wa jezi. Wakaenda Rwanda kumfuata Haruna kisha wakamchukua Ditram Nchimbi. Safari ya kuirudisha Yanga katika njia ya matumaini ikaanza upya.

Hata hivyo, miguu ilianza kumsaliti Haruna. Safari hii hakuwa Haruna yule wa ‘Kampa kampa tena’. Nguvu ni kitu cha kuisha. Makocha watatu wamepita Yanga na hakuna ambaye aliafiki uwezo wa miguu ya Haruna. Hatuwezi kuwalaumu. Angekuwa kocha mmoja sawa, lakini wote watatu waliona wazi kwamba miguu ya Haruna ilikuwa imechoka.

Na sasa Yanga wameafikiana na makocha hao kuwa miguu ya Haruna imefika mwisho. Wamemuaga Alhamisi iliyopita. Haruna anaweza kwenda katika klabu nyingine ndogo na miguu yake ikawa mipya kwao. Anaweza kwenda Uarabuni akaonekana ana miguu mipya. Kwa Yanga imetosha. Kwaheri Haruna.

Advertisement