JICHO LA MWEWE: Na Abdi Banda naye kanyoosha mikono juu

WIKIPEDIA inaonyesha mchezaji anayeitwa Abdi Banda ana miaka 26 tu. Ametoka Afrika Kusini amerudi Tanzania akisaini klabu ya MtibwaSugar. Banda ni bonge la beki. Kizuri zaidi ana akili ya mpira na ana umbo kubwa la mpira.

Sijui nini kimetokea kwa Banda lakini amerudi nchini. Nilidhani angefika mbali lakini haijawezekana. Alianza vema Afrika Kusini wakati anacheza Baroka lakini hatukumsikia tena katika miaka ya karibuni. Hata timu ya taifa hayupo tena wakati kuna nyakati alikuwa tegemeo katika ulinzi.

Nilikuwa nampenda Banda kwa tabia moja ya ujeuri chanya. Kiasi alikuwa na majivuno lakini ni katika kiburi kile kile cha kujiamini ambacho ungependa wachezaji wetu wawe nacho. Kwamba mchezaji ajione ana uwezo kama wengine tu wa mataifa mengine. Huwa inasaidia katika mafanikio kwa sababu wakati mwingine wachezaji wetu hawajiamini.

Niliamini tabia hii ingemfikisha Banda mbali hasa kwa namna alivyoanza kutamba Baroka na ukijumlisha ukweli kwamba anajua soka. Taratibu jina lake lilianza kufifia na sielewi kwanini kwa sababu ni mchezaji mzuri. Labda ana mipango mingine na Mtibwa amekuja kujiegesha tu mara moja.

Dirisha hili hajarudi yeye tu. Amerudi pia Eliud Ambokile. Nasikia Eliuter Mpepo pia alikuwa anasaka timu hapa hapa nchini. Wapo wengi wamerejea katika dirisha hili. Ambao wamebaki ni wale wale ambao tumewazoea siku zote. Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Simon Msuva.

Mwingine ambaye ameanza kuchomoza ni Novatus Dimas. Huyu fundi wa mpira amefanikiwa kuingia katika kikosi cha kwanza cha Maccabi Tel Aviv na tunatazamia kwamba atafika mbali zaidi. Ni kijana na ana nguvu nyingi kwa sasa. Uamuzi unabakia katika miguu yake.

Kwanini mastaa wetu wanarudi? Jibu ni rahisi tu. Kucheza nje na kung’ara sio jambo la masikhara sana. Ni kazi ngumu. Nataka kuelezea daraja fulani ambalo wachezaji wetu wanashindwa kuvuka. Daraja la uvumilivu na fikra pevu.

Unapocheza nje kuna wakati mambo hayaendi sawa. Unalazimika kupambana zaidi na zaidi kuyaweka mambo sawa. Usitazame nyuma. Hapo katika kutazama nyuma huwa kunawashinda vijana wetu. Kwao kutazama nyuma ni rahisi zaidi.

Tunaishi maisha matamu ya kijamaa ambayo yanakufanya ujisikie amani ukiwa Tanzania hata kama hauna pesa nyingi. Wakati mwingine mchezaji analipwa dola 2,000 kwa mwezi akiwa nje ya nchi huku akiwa analipwa dola 3,000 kwa mwezi akiwa nchini. Inakuwa rahisi kwake kurudi nyumbani kwa sababu anahisi labda nyumbani analipwa zaidi.

Hata hivyo, kumbe kule anakolipwa mshahara pungufu kidogo kunamuweka sokoni zaidi kuliko huku ambako kuna ongezeko kidogo la pesa. Wachezaji wetu wanachukua maamuzi rahisi ya kurudi nchini kwa sababu ya mambo mawili.

Kwanza wanaamini kwamba nyumbani kunalipa vizuri zaidi lakini pili wanadai kwamba huduma za maisha nyumbani ni rahisi zaidi kuliko nje. Kwamba bora ulipwe dola 2,000 Tanzania kuliko kulipwa dola 3,000 nje ya nchi. Sidhani kama ni mtazamo sahihi.

Mtazamo sahihi wa Mnigeria ungekuwa ni kupambana aweze kulipwa dola 5,000 ili aweze kuishi maisha mazuri zaidi. Sisi mtazamo wetu ni kurudi nyumbani. Bahati nzuri kwa Mnigeria ni kwamba hiyo pesa asipofanikiwa kuipata hapo ataenda kuipata nchi nyingine lakini sio kwao.

Hauwezi kusikia mchezaji wa Kitanzania alikuwa Afrika Kusini kisha akaenda Dubai halafu akaenda Sweden halafu akaenda Singapore. Akienda katika nchi husika akishindwa basi atarudi nyumbani. Ni tofauti kidogo na wenzetu ambao hawana mpango wa kulegeza nati.

Haishangazi kuona Yikpe alipoondoka hapa hakurudi Ivory Coast. Alienda Falme za Kiarabu. Mambo yakimshinda ataenda zake kwingineko. Kurudi nyumbani sio chaguo la kwanza. Sisi ni chaguo la kwanza. Kuna wachezaji ambao wameamua lisiwe chaguo la kwanza.

Daraja hili ni gumu kuvuka lakini unapofanikiwa mambo yanakuwa mazuri. Ni daraja gumu kuvuka na ndio maana sio wote tunaweza kuwa wachezaji wazuri na kulipwa mamilioni ya pesa kama wanayolipwa mastaa wakubwa. Soka sio mchezo rahisi.

Katika mchujo wa waliofanikiwa na wasiofanikiwa kuna kazi ngumu ya kufanya ambayo wachezaji wetu hawafanyi. Vikwazo vipo vingi lakini maisha sio rahisi sana. Unahitaji kupambana kulikopitiliza na ndio maana tunapata tafsiri halisi ya neno mchezaji wa kulipwa.

Watazame pia wachezaji wa Nigeria, Ghana, Cameroon na kwingineko. Wanatafuta sehemu ya kuonekana tu kwa ajili ya kusogea kwingine. Mfuatilie mchezaji kama Asante Kwasi. Yuko wapi? Hapa nchini alianzia wapi? Tulimjulia akiwa Mbao.

Baadaye alisogea Lipuli ya Iringa akapigwa baridi. Baadaye akaonwa na timu kubwa Simba kama alivyotaka. Alipoondoka nchini baada ya mambo kuharibika hakurudi kwao. Alienda klabu ya Hafia ya Guinea. Hakurudi kwao. Haya ndio maisha yao.

Ni wachezaji wachache ambao wanarudi makwao baada ya umri kupita. Wengine pia hutokomea huko huko na kuanzisha biashara nyingine. Maisha ya kibepari waliyotoka huwaacha wakiwa majeuri maradufu. Sisi sijui kwanini wachezaji wetu huamua kugeuza na kupiga miayo hapa hapa.

Ni kweli, nje kuna baridi kali, hakuna urafiki, kuna ubaguzi, watu hawapeani pesa ovyo, na mengi mengineyo lakini hauwezi kupata pesa ya maana katika soka kama hautavumilia yote haya. Kina Didier Drogba walifanikiwa baada ya kuvumilia yote haya.

Maisha ya soka sio rahisi.