JICHO LA MWEWE: Mtibwa ni Tottenham Hotspurs inayojifia taratibu

Tuesday April 20 2021
MTIBWA PIC
By Edo Kumwembe

KWANINI Simba wanapata mafanikio katika michuano ya kimataifa? Jibu ni rahisi tu. Wamekusanya mastaa kutoka katika nchi mbalimbali wakawaunganisha na mastaa wachache wa ndani na hatimaye wamepata mafanikio unayoyaona.

Je, Ligi inawasaidia Simba kutamba katika michuano ya kimataifa? Sidhani. Sina uhakika. Sidhani kama ligi yetu inawasaidia sana kutamba katika michuano ya kimataifa. Kwamba Ligi yetu inawakomaza Simba kuwa kama walivyo sina uhakika.

Majuzi wametoka kuwachapa Mtibwa Sugar mabao 5-0 pale Uwanja wa Taifa Temeke. Usishangilie sana matokeo haya. Ni kweli kwamba inatokea timu moja kubwa kuifunga timu nyingine kubwa kwa idadi kubwa ya mabao. Hata Ulaya hali hii huwa inatokea.

Kinachosikitisha katika matokeo haya ni kwamba yalitabirika kabla ya mechi. Mara nyingi matokeo ya timu moja kubwa kumfunga mwingine mabao mengi huwa hayatabiriki kabla ya mechi. Binafsi nilitabiri kwamba Mtibwa angefungwa nyingi.

Kwanini? Jibu rahisi. Wakati Simba wakienda juu zaidi Mtibwa sio kwamba wamebakia pale pale, hapana, wamekwenda chini zaidi. Hii ni timu ambayo hadhi yake katika Ligi yetu ilipaswa kuwa kama Tottenham pale England. Mtibwa walipaswa kuwa timu kubwa baada ya wakubwa wengine kupewa hadhi yao.

Mechi ya Simba na Mtibwa au Yanga na Mtibwa au Azam na Mtibwa ilipaswa kuwa ngumu kama vile Tottenham wanapocheza na Liverpool au wanapocheza na Manchester United. Hata hivyo siku hizi Mtibwa hawatupi hadhi hiyo kwa sababu wanaelekea kujifia.

Advertisement

Mtibwa ya leo ishaondokewa na makocha wawili mpaka sasa Zubery Katwila na Thierry Hitimana msim huu. Mtibwa ya leo ina wachezaji wenye hadhi ya kawaida kabisa. Haishangazi kuona hawana mchezaji yeyote katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars zaidi ya Baraka Majogoro.

Lakini hawa ndio Tottenham wetu hapa Tanzania. Walipaswa walau kutoa wachezaji kama akina Harry Kane, Dele Ali, Harry Winks na wengineo katika kikosi cha Taifa Stars. Ni kama zamani walivyokuwa wanatujazia walau wachezaji watano hadi sita katika kikosi cha Taifa Stars.

Wangeweza kutuletea kina Mecky Maxime, Shaaban Nditi, Dickson Daud, Abdi Kassim, Kassim Issa na wengineo. Leo Mtibwa wana mchezaji mmoja tu katika kikosi cha Taifa Stars, Baraka Majogoro na ni wazi kwamba wanastahili kuwepo walipo. Wapo maeneo ya kushuka daraja.

Zamani tu walikuwa na wachezaji wa maana ambao wangeipa Simba hii mechi ya uhakika. Zama za kina Abubakar Mkangwa, Geofrey Magori, Zubery Katwila na wengineo. Sasa hivi hawana wachezaji wa kariba hii na timu yenyewe kwa ujumla inasikitisha sana.

Kuondoka kwa timu ya aina ya Mtibwa hakusaidii sana Ligi yetu. Wakubwa wanashindwa kupata changamoto ya uhakika na utamu wa Ligi unapungua. Mtibwa ni timu iliyokuwepo kwenye Ligi Kuu kwa zaidi ya miaka 20. Ni timu ya kitamaduni katika Ligi yetu na ilipaswa kuendelea kuwepo katika nafasi yake nyuma ya Simba, Yanga na Azam.

Matokeo yake wamezipisha timu nyingine za kawaida kuwa imara zaidi na kukaa juu yao. Timu kama Namungo na KMC zimekwenda kukaa mahala ambapo Mtibwa wamekaa kwa miaka mingi. Tatizo bado hatuwezi kuziamini timu hizi kwa sababu huwa zinakuja na kuondoka.

Mtibwa wanapaswa kubadilisha sera zao ili warudishe makali yao. Wanapaswa kwanza kuwa na mfumo wa kiskauti imara zaidi kwa ajili ya kuimarisha timu yao. Lakini hapo hapo waamue pia kuwekeza kwa kununua wachezaji mahiri kutoka katika klabu kama Namungo au KMC.

Unaruhusu vipi timu kama Namungo iwe na mastaa kama Lucas Kikoti, Steven Sey, Charles Manyama na wengineo? Kwanini usiwafanye kuwa wako? Unaruhusu vipi mastaa kama Charles Ilamfya, Hassan Kapalata, David Bryson na wengineo wacheze KMC? Hawa ndio wachezaji wenye hadhi ya Mtibwa.

Sawa wanaweza wasiwe wachezaji wenye hadhi ya Yanga na Simba lakini wanaweza kuwa Mtibwa na kuwasumbua wakubwa. Matokeo yake nguvu ya soka imehama kutoka Mtibwa imekwenda KMC na Namungo kwa sababu kina Jamal Bayser wamekubali wachezaji wazuri waende hizi timu mbili huku wao wakiendelea kuokota wachezaji mitaani.

Itakuwa aibu kama Mtibwa watashuka daraja au watakuwa wameingia rasmi katika kundi la timu zinazofungwa kirahisi na wakubwa. Zamani hawakuwa hivi. Wakisalimika kushuka basi wajichunguze na matajiri wao waamue kitu kimoja. Kuvunja timu au kuingia katika ushindani.

Sawa timu kubwa hufungwa na timu kubwa lakini Mtibwa walitabirika kufungwa nyingi na Simba na hii haileti afya katika soka. Mtibwa ni Tottenham wetu. Washindane na sio kushiriki.

Advertisement