Prime
JICHO LA MWEWE: Kipa bora hatokani na 'clean sheet', anatokana na hili...

Muktasari:
- Wakati mwingine tunabishana kuhusu ubora wa Moussa Camara na Djigui Diarra kwa kuangalia idadi ya mechi ambazo wamecheza bila ya kuruhusu bao.
TUNABISHANA kila kitu siku hizi. Na mchezo wenyewe ulipokwenda katika masuala ya namba tumezidi kubishana zaidi na zaidi. Wachezaji tunawaangalia ubora wao kwa namba. Hata langoni siku hizi mashabiki wetu wamekuwa wakiangalia ubora wa magolikipa kwa kitu kinachoitwa idadi ya 'clean sheet'.
Wakati mwingine tunabishana kuhusu ubora wa Moussa Camara na Djigui Diarra kwa kuangalia idadi ya mechi ambazo wamecheza bila ya kuruhusu bao. Kama kipa alicheza mechi tano mfululizo bila ya nyavu zake kuguswa basi mitandao inaanza kumponda kipa mwingine na kumsifia kipa mwenye clean sheet nyingi. Imekuwa kitu cha kawaida siku hizi kwa sababu tunapenda kubishana kwa kila kitu na kila mtu anavutia kwake.
Tunachosahau ni namna ambavyo clean sheet hailindwi na kipa peke yake. Kipa ana asilimia chache za kusababisha timu itoke uwanjani bila ya kuruhusu bao. Zipo nyakati ambazo anaweza kuiweka timu mchezoni lakini ukichunguza kwa haraka haraka kuna rundo la wanaume wanafanya kazi ngumu kumlinda mtu mmoja tu. Aliye nyuma yao.
Utazame ukubwa wa lango. Ni namna gani mwanadamu mmoja anaweza kuzuia lango lisitikiswe na mpira. Ndo maana linapofika suala la penalti takwimu zinaonyesha penalti nyingi zinafungwa kuliko kuzuiwa. Ni suala la ukubwa wa lango. Kipa anapokabiliana na mpira uliotuama wa mpigaji penalti ndipo anapokumbushwa kwamba suala la Clean sheet huwa ni la wote. Pale anakabiliana na mtu ambaye hajakabwa.

Ndio maana linapokuja suala la Clean sheet kinachopelekea timu kutoruhusu bao au mabao ni ulinzi wa pamoja wa timu. Ukabaji wa pamoja na uzuiaji wa pamoja. Kwa namna ambavyo lango ni kubwa na bado pambano linatoka bila bila ni ngumu kufikiria namna gani kipa pekee anaweza kuifanya kazi hii.
Kule katika mchezo wa kikapu hakuna kikapu na lango ni dogo lakini unaweza kuona namna mpira unavyotumbukizwa mara nyingi. Vipi kwa lango la soka ambalo ni kubwa na bado pambano linaweza kumalizika bila ya kufungana. Kazi hii anaweza kuifanya mwanadamu mmoja? Ni ngumu kufikiria kwamba inawezekana kama utakaa chini na kutafakari.
Wakati mwingine ubora wa timu pia unasababisha kipa wao asifikiwe. Kuna timu bora ambazo zinakaa na mpira kwa muda mrefu na zinampumzisha kipa. Nakumbuka namna Rais wa zamani wa Barcelona, Joan Laporta alivyogoma kumlipa mshahara mkubwa kipa wa zamani wa timu hiyo, Victor Valdes akiamini kwamba kipa huyo alikuwa hapati mikiki ya kuthibitisha ubora wake kwa sababu mara nyingi Barcelona ilikuwa inakaa na mpira zaidi na Valdes alikuwa anakwenda likizo langoni.

Na katika soka la kisasa timu zimekuwa na ukabaji mkubwa kuliko wakati mwingine wowote ule. Habari za ukabaji wa kiungo mmoja wa chini zimetoweka na sasa timu inakaba kuanzia juu katika kile kinachoitwa 'high pressing'. Habari ya kumuachia kiungo mmoja kama Patrick Vieira au Javier Mascherano akabe zimepitwa na wakati. Sasa hivi kila mtu anakaba katika maeneo yote.
Kama mnafanya haya kwa usahihi mashambulizi kwa golikipa wenu yanakuwa machache. Umoja huu ndio unaotengeneza clean sheet kwa timu husika. Mtu mmoja peke yake hawezi kutengeneza clean sheet. Anaweza kusaidia kwa kiasi chake lakini timu nzima inahusika kutengeneza clean sheet.
Kwa mtazamo wa kawaida kipa bora ni yule anayeokoa zaidi michomo kwa sababu ni jambo binafsi zaidi. Hata hivyo kuzuia mabao linapaswa kuwa jambo la kitimu zaidi. Kuna nyakati unaweza kumpata kipa bora katika timu za kawaida kuliko hizi timu kubwa kwa sababu timu za kawaida zimekuwa zikipokea mashambulizi mengi kuliko timu kubwa.
Kuna makipa wa timu za kawaida wamekuwa wakifungwa, lakini wamekuwa wakiokoa michomo mingi kwa sababu timu zao zinashambuliwa zaidi. Ni kweli hawa kina Diarra na Camara wanaokoa michomo lakini haizidi ile ambayo inatokea kwa makipa wa JKT Tanzania, Coastal Union, Pamba na wengineo. Tulipaswa kuangalia zaidi takwimu za uokoaji wa michomo kuliko clean sheet. Tatizo huwa hatuangalii takwimu za uokoaji wa michomo.

Hizi timu za kawaida unakutana na kipa ambaye amefungwa mabao matatu lakini ameokoa michomo saba ya wazi. Lakini unakwenda katika timu kubwa unakutana na kipa mwenye clean sheet ambaye ameokoa mchomo mmoja tu wa wazi katika mechi nzima. Muda mwingi wa mechi alikuwa anarudishiwa mpira na mabeki wake na kupiga pasi za hapa na pale.
Kuna makipa wachache wa timu kubwa ambao unaona ni kweli wameiweka timu katika mechi na wametengeneza clean sheet. Mfano ni David De Gea. Wakati akiwa katika ubora wake angeweza kuiweka timu mchezoni kwa kuokoa michomo nane ya wazi. Huyu ndiye aina ya kipa wa timu kubwa ambaye alikuwa anachangia kwa kiasi kikubwa kutengeneza clean sheet kwa timu yake.
Pambano moja dhidi ya Arsenal akiwa katika jezi ya Manchester United, De Gea aliokoa michomo 11 na kulitetea lango lake. Sio kila kipa wa timu kubwa anaweza kufanya jambo hilo. Mara nyingi makipa wa Wolves ndio huwa wanaifanya kazi hii. Ndio maana Clean sheet sio habari kubwa sana kwa wenzetu.

Wakati mwingine inakwenda mbali zaidi kwamba labda kwa utata wa kipa bora ni yupi ndio maana hatujawahi kuwa na mwanasoka bora wa dunia ambaye ni golikipa. Kama hatujamaliza utata kipa bora ni yupi kati ya yule mwenye clean sheet nyingi au ambaye anaokoa michomo mingi labda ndio maana hiyo nafasi haijawahi kutoa mwanasoka bora wa dunia.
Watunza takwimu ikiwabariki basi waanze kutuletea takwimu za makipa wanaokoa michomo zaidi. Hapa ni kabla hatujaenda katika kazi ya pili isiyo ya msingi lakini imeanza kutajwa kuwa muhimu. Kucheza kwa miguu. Kina Pep Guardiola wametuongezea sifa nyingine ya kipa kutumia miguu kwa usahihi zaidi.
Wakati huo hu pia ni muhimu kwa wachambuzi wetu kukumbuka takwimu nyingine ambazo hazionekani sana uwanjani. Mfano ni ile ya 'key passes'. Kuna wachezaji wanapiga pasi za namna hii ambazo hazizalishi pasi ya bao lakini zilikuwa muhimu uwanjani.

Lakini kwanza tuanze kutafakari kwa umakini hili suala la Clean sheet. Naona limeanza kukuzwa kwa kiasi kikubwa na wakati mwingine tunawapa ushujaa makipa wakati ukweli kuna kazi ngumu wanafanya akina Shomari Kapombe, Dickson Job, Ibrahim Bacca na wengineo. Tuanze kuwaangalia pia makipa ambao wanafanya kazi ngumu kutokana na timu wanazochezea.