JICHO LA MWEWE: Chama na Sure Boy walivyokomba noti miezi ya karibuni

KAMA ni bahati nzuri au bahati mbaya. Huyu mchezaji aliyetangazwa kurudi Simba Ijumaa mchana, Clatous Chotta Chama amelamba noti za kutosha ndani ya kipindi kifupi kilichopita. Wanadamu wengine wanazaliwa na bahati zao.

Kiungo mwenzake, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ambaye ametimkia Yanga katika dirisha hili la Januari akitokea Azam naye ni miongoni mwa wachezaji waliopita katika njia za pesa ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Tunaanza na nani? Chama. Amejua kuihangaisha mioyo ya mabosi wa Simba na mashabiki wake. Kabla hajauzwa kwenda Morocco Agosti mwaka jana, miezi michache kabla ya hapo Chama alikuwa amehangaisha mioyo ya mashabiki wa Simba.

Mkataba wake ulikuwa unakaribia kukata roho na uvumi wa Chama kuhama Simba ulikuwa mwingi. Machi mwaka jana Simba walifanikiwa kuinasa saini ya Chama ikiwa ni miezi michache kabla ya mkataba wake wa awali kumalizika.

Alisaini mkataba wa miaka miwili na alikuwa amevuta pesa ndefu ya kusaini mkataba huo (signing-on fee). Presha ya kwamba Yanga walikuwa wanamtaka Chama kwa dau lolote lile ilikuwa imewakumba Simba. inadaiwa kwamba alivuta zaidi ya Sh300 milioni kwa ajili ya kusaini mkataba mpya Msimbazi.

Pengine ni mkataba alioutumikia kwa muda mfupi zaidi ndani ya Simba. miezi mitano baadaye Chama alikuwa amehitajika Morocco katika klabu ya Berkane. Waarabu nao ni watu ambao pia wanatoa ‘signing-on fee’ kwa mchezaji.

Achilia mbali makubaliano ya ada ya uhamisho kati ya Simba na Berkane, bado Chama alipata pesa ya uhamisho. Ni kitu cha kawaida kwa Waarabu. Mchezaji lazima avute pesa na wakala wake pia lazima avute pesa kukamilisha uhamisho.

Wakati mwingine katika dunia ya giza unakuta pia unakuta kocha naye anaweza kuvuta chake kupitia mgongo wa wakala bila ya mabosi wa timu kujua. Lakini hapa kwa sababu tunamzungumzia Chama basi hiyo itakuwa topiki ya siku nyingine.

Ina maana ndani ya miezi mitano Chama alikuwa amevuta pesa Simba na kisha Berkane. Na baada ya hapo tukaanza kusikia kelele za Chama kutokuwa na amani na maisha ya Morocco. Kama ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi zamani ambaye alikuwa anakwenda na kurudi, watu wa Simba walianza kumuandalia makazi Chama tena.

Haikuwa kazi rahisi. Kulikuwa na presha kubwa ya jina la Chama kuhusishwa na Yanga. Ingawa mkataba wa Chama kwenda Berkane ulikuwa unaonyesha kwamba Simba wangekuwa chaguo la kwanza lakini bado Yanga walikuwa wanapiga presha ya kwamba wanaweza kumshusha Chama Jangwani.

Kwa mara ya pili ndani ya miezi michache Simba walilazimika kukabiliana na presha ya wapinzani wao kupitia jina la Chama. Ilikuwa haijapita hata mwaka tangu wampe pesa nyingi kupitia presha hii na bado walijikuta katika wakati mgumu kwa mara nyingine tena.

Hatimaye mkataba wa Chama na Berkane ulichanwa baada ya mchezaji mwenyewe kuonyesha kutoridhishwa na maisha ya Morocco. Simba wamelazimika kumrudisha tena klabuni na usidhani kama amerudi bure tu. watu wa Yanga waliweka presha na Chama alikuwa anajua hilo.

Chama alikuwa anasoma mitandaoni na anaona jinsi ambavyo anavalishwa jezi ya Yanga kila siku. Kwake ni karata muhimu kupata pesa nyingi katika mkataba achilia mbali masuala ya mshahara. Sijajua Simba wamempa kiasi gani lakini haikuwa lazima kwa Chama kucheza Simba kama ofa yao ilikuwa ndogo kuliko Yanga. Kwahiyo Simba wamempa tena pesa mchezaji ambaye hata kabla mwaka haujatimia walishampa kiasi kikubwa cha pesa.

Tumgeukie Sure Boy. Huyu dogo ndani ya miezi 10 tu aliiandikia timu yake ya Azam barua mbili za kuomba kuondoka. Sijui kama alikuwa anataja anataka kwenda wapi lakini wote tunafahamu kwamba mwelekeo wake ulikuwa Yanga.

Wakati Chama akikaribia kuelekea Morocco, Sure Boy alikuwa ameiandikia klabu yake ya Azam akiomba kuondoka klabuni hapo. Yanga walikuwa wamepeleka ofa yao ya Sh70 milioni kwa ajili ya kupata huduma zake.

Azam waligoma katakata. Baadaye wakaweka wazi kwamba Sure Boy alikuwa hauzwi kwa dau lolote lile. Bwana mdogo akavutwa kati na kufanyiwa kikao na mabosi wake wa Azam. Akakubali kubaki. Haikuishia hivi hivi tu akasaini mkataba mpya wa miaka miwili.

Kumbuka kwamba wakati linatokea kasheshe la yeye kutaka kwenda Yanga Sure Boy alikuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja tu. Licha ya kwamba Azam walikuwa wamefanikisha kumbakisha lakini angeweza kuondoka bure mwishoni mwa msimu huu.

Azam wakampa pesa akasaini mkataba wa miaka miwili. Haikuwa pesa ndogo. Naambiwa ni zaidi ya Sh80 milioni. Sure Boy akarudi kuivaa jezi ya Azam mpaka yalipotokea yale ambayo yalitokea pamoja na wenzake Agrey Morris na Mudathir Yahya kusimamishwa.

Hatuhitaji kurudia namna gani ambavyo wachezaji hawa waliingia katika mgogoro na klabu yao lakini ni wazi kwamba Azam walionekana kuchoshwa zaidi na vitimbi vya Sure Boy. Pande zote mbili zikaamua kuachana.

Yanga wakaitumia nafasi hiyo. Wakampa mkataba wa miaka miwili. Haukuwa mkataba wa bure. Walilazimika kujikamua kuipata saini yake ingawa hapa kidogo Sure alikuwa tofauti na Chama. Wapinzani wa Yanga, Simba hawakuhitaji saini yake kwahiyo Sure Boy alikosa upinzani ambao ungemnufaisha zaidi kama ambavyo ulimnufaisha Chama.

Kama Simba wangeingia katika mbio za kuiwania saini yake, Sure Boy asingekosa Sh100 milioni na kuendelea. Hata hivyo, kwa sababu anatajwa kuwa ni shabiki mnazi wa Yanga alijikuta akipata kiasi cha chini ya hapo ingawa nafahamu kwamba alipewa pesa nyingi.

Lakini hii ina maana kuwa ndani ya miezi sita tu Sure Boy alikuwa amelamba signing-on fee mbili. Hata hivyo, Chama hawezi kumzidi Chama ambaye ndani ya mwaka mmoja tu amelamba signing-on fee tatu. Maisha yamewatendea haki.