Jichanganye kwa Nabi uumie

JICHANGANYE akumalize. Ndivyo unavyoweza kusema jinsi kocha mkuu wa Yanga, Nasredinne Nabi anavyoonekana kuwa mkali wa kusoma mchezo na kuwamudu wapinzani wake kwa mabadiliko ya wachezaji ‘sub’.

Nabi amekuwa kinara wa kufanya mabadiliko mazuri ya wachezaji yanayobadili mchezo na kumpa ushindi mara kwa mara jambo ambalo limekuwa kivutio. Katika mechi sita mfululizo za mashindano yote ikiwemo ile ya mwisho ya msimu uliopita, kocha huyo alibebwa na sub nzuri anazofanya zenye macho. Cheki ubabe wake katika sub.


KAMALIZA KIBABE

Katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa Juni 29, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam alifanya mabadiliko mazuri yaliyoipa timu yake ushindi wa bao 1-0.

Nabi alifanya mabadiliko dakika ya 66 kwa kumtoa Jesus Moloko na Bryson David na kuwaingiza Dennis Nkane na Yassin Mustapha - mabadiliko ambayo yalizaa matunda kwani dakika ya 80 Nkane alifunga bao kwa kichwa akimalizia krosi ya Chico Ushindi na kuipa pointi tatu muhimu timu hiyo.Kocha huyo aliendelea kung’ara na sub katika mchezo uliofuata wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Coastal Union uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Julai 2, mwaka huu na kuipa ubingwa timu yake.

Katika mchezo huo hadi dakika ya 47 Yanga ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union na hapo Nabi aliamua kumtoa Chico Ushindi na kumuingiza Heritier Makambo ambaye alibadilisha mchezo kwa kiasi kikubwa.

Dakika ya 56 timu hiyo ilisawazisha bao lililofungwa na Feisal Salum akimalizia krosi ya Makambo kabla ya Makambo kufunga la pili dakika ya 81. Hata hivyo, dakika ya 87 Costal Union ilisawazisha na hivyo hadi dakika 90 matokeo kuwa 2-2 hivyo mchezo kwenda dakika 30 za ziada. Baada ya dakika 90, Nabi alifanya tena mabadiliko na kuwatoa Djuma Shaban na Bakari Mwamnyeto na nafasi zao kuchukuliwa na Denis Nkane na Kibwana Shomari.

Mabadiliko hayo yalimnufaisha tena kwani wakati Coastal Union ikiongoza kwa mabao 3-2 hadi dakika ya 111, Nkane aliisawazishia Yanga bao dakika ya 112 na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 hivyo kuamuriwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Yanga waliibuka mabingwa wa michuano hiyo baada ya kushinda kwa penalti 4-1.


KAANZA NA UTAMU WAKE

Mabadiliko ya Nabi yameendelea kuipa faida timu hiyo hata katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba uliofanyika Agosti 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Katika mchezo huo wakati Simba ikiongoza kwa bao 1-0 hadi mapumziko, mwanzoni mwa kipindi cha pili Nabi aliwatoa Salum Abubakary ‘Sure Boy’ na Farid Mussa na kuwaingiza Bernard Morrison na Jesus Morocco - waliobadilisha mchezo na kupata mabao mawili kupitia kwa Fistion Mayele, hivyo kutwaa Ngao ya Jamii.

Ubora wa kocha huyo kwenye sub ulidhihirika pia katika mechi ya Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania Agosti 16 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Yanga kushinda kwa mabao 2-1. Katika mchezo huo hadi dakika ya 55 timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1, na hapo ndipo Nabi alipofanya mabadiliko dakika ya 57 kwa kuwatoa Feisal na Gael Bigirimana na nafasi zao kuchukuliwa na Morrison na Dickson Ambundo, ambapo dakika ya 84 beki na nahodha wa timu hiyo Bakari Mwanyeto aliifungia bao la ushindi akimalizia krosi ya Morrison.

Pia, Nabi alitisha na sub mchezo uliofuata wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Agosti 20 ambao mabingwa hao watetezi walishinda kwa mabao 2-0. Bao la kwanza la dakika ya nne la Bernard Morrison na hadi mapumziko na kipindi cha pili dakika ya 55 Nabi alimtoa Makambo na kumuingiza Mayele ambaye dakika 12 tu aliipatia timu yake bao la pili.

Kocha huyo aliendelea na sub za maana katika mchezo dhidi ya Azam uliofanyika Septemba 6 ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Katika mchezo huo ambao Azam walicheza kwa kiwango bora zaidi na kuongoza kwa bao 1-0 hadi mapumziko, Nabi alifanya mabadiliko mwanzo mwa kipindi cha pili kwa kumtoa Dickson Ambundo na Dickson Job na kuwaingiza Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Djuma Shaban. Hadi mwisho ilikuwa sare ya 2-2.