HISIA ZANGU: Nimemkumbuka Anko Mrisho Ngassa katika ubora wake?

GHAFLA nimemkumbuka Anko Mrisho Ngassa katika ubora wake. maisha yanayoyoma kwa kasi. Kwa sasa yupo mitandaoni akiposti video zake na kuelezea kila anachokifanya katika maisha. Huku katika soka amebakia kuwa shabiki tu.

Baada ya Edibily Jonas Lunyamila kutamba sana katika soka kwa miaka mingi kama winga, Mwenyezi Mungu alituletea Anko Ngassa. Hawakuwahi kufanana kwa mambo mengi lakini pande za pembeni wanaweza kuwa wachezaji bora wa zama zao waliokabidhiana vijiti.

Ngassa alikuwa winga bora kwa sababu alikuwa ana kasi na matumizi mazuri ya akili katika eneo la mwisho. Angeweza kufunga mwenyewe kwa ustadi mkubwa na angeweza kupika mabao kwa wenzake. Kasi yake haikuwa ya mwendabure.

Achilia mbali mikimbio yake upande wa pembeni lakini Ngassa pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia eneo la katikati na kusababisha madhara makubwa kwa wapinzani. Alichohitaji ni nafasi ya kukimbia tu. lakini hata kama kungekuwa na kundi kubwa la maadui mbele yake alikuwa na uwezo pia wa kupiga chenga.

Anabakia kuwa mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ingawa taifa hili lilibarikiwa kutoa wachezaji mahiri ambao wamewahi kukipiga katika timu ya taifa kwa mafanikio. Usiwasahau akina Zamoyoni Mogella.

Nimemkumba Anko Ngassa kwa sababu tatu za msingi. Sababu ya kwanza ninapomuonea huruma kwa kupishana na maisha ya soka ya kizazi hiki katika ngazi ya klabu. Ngassa alicheza mpira mkubwa na alifanya mambo makubwa katika klabu yake ya Yanga katika zama ambazo Yanga haikuishi hivi kiuchumi, kimawazo na kimafanikio.

Wakati ule walikuwepo watu walioonekana kuwa matajiri lakini wasingeweza kwenda Morocco kuweka kambi kama GSM walivyofanya. Wasingeweza kuiweka timu katika kambi ya kisasa kama ya Avic kama ambavyo sasa hivi Yanga wanakaa.

Kuna maandalizi mengi ya Yanga ya leo ambayo yamekuwa tofauti na Yanga ya zamani. Hata wachezaji wengi aliocheza nao hawakuwa na ubora mwingi kama hawa wa leo akina Khalid Aucho na wengineo. Najaribu kuwachomoa mawinga wawili wa sasa wa Yanga na naamini Yanga ingekuwa bora zaidi leo kama ingekuwa na Ngassa kuliko ilivyo sasa.

Wachomoe Jesus Moloko na Tuisila Kisinda kisha muweke Anko Ngassa katika ubora wake. Nadhani Fiston Mayele angefunga mabao mengi zaidi ya haya anayofunga sasa. Unaweza kuwauliza akina Boniface Ambani na watakuthibitishia hiki ninachokisema.

Sihitaji tubishane kuhusu Tuisila na Moloko dhidi ya Ngassa. Nadhani wote tunafahamu kwamba Ngassa alikuwa bora zaidi yao. Tatizo ni namna gani ambavyo Anko amepishana na zama hizi. Anko wa wakati ule katika kikosi hiki cha Yanga angekuwa staa mkubwa anayekaribiana kuhusudiwa na mashabiki kama ilivyo kwa Mayele.

Bernard Morisson ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji kikubwa, inawezekana zaidi ya Ngassa. Lakini muda wowote ule namchukua Ngassa mbele ya Morrison kwa sababu Ngassa alikuwa bora kila wikiendi na kila uwanja wowote aliocheza soka.

Morrison ana homa ya vipindi. Kuna mechi anacheza vizuri halafu inayofuata hatuonyeshi makali yake. anaweza kupotea uwanja ni katika mechi tatu halafu akaibuka katika mechi moja. Ngassa hakuwa mchezaji wa namna hiyo.

Sababu nyingine ambayo imepelekea nimkumbuke Anko Ngassa ni namna ambavyo kila siku wachezaji wazawa wanavyopotea katika umuhimu ndani ya klabu kubwa. Sio tu kwa Yanga, lakini hata kwa Simba Ngassa angetamba upande wowote wa pembeni.

Muda pekee ambao ingebidi agawane umuhimu na mtu katika upande wa pembeni ni pale Simba walipokuwa na Jose Luis Miquissone. Pale kungekuwa na changamoto na nadhani mmoja angecheza kulia na mwingine angecheza upande wa kushoto.

Lakini kwa hali ilivyo sasa pale Simba, Ngassa ni bora kuliko Ousmane Sakho, ni bora kuliko Kibu Dennis, ni bora kuliko winga yeyote ambaye anapangwa pale Simba. huu ndio ukweli kwamba Ngassa amepishana na hivi vikosi vya dhahabu.

Amepishana na vikosi vya Simba na Yanga ambavyo vimeimarika pia kisaikolojia. Tangu mwanzo wa msimu huwa vinaangalia namna ya kufika hatua za robo fainali katika michuano ya Ligi ya mabingwa au ile ya shirikisho.

Wakati yeye anacheza hakufika robo fainali ya michuano yoyote katika ngazi ya klabu. Kufika makundi tu ilikuwa ni mtihani na hakuwahi kufika. Nadhani ni kwa sababu ya kupishana na vizazi hivi vya wakubwa ambavyo vimeimarika zaidi.

Bila ya kujali nafasi zao uwanjani kinachosikitisha zaidi ni kwamba katika maeneo ya mbele ya vikosi hivi wazawa wametoweka. Kijana Clemence Mzize anajaribu kuchomoza baada ya Fei Toto kutoweka. Hassan Dilunga katika Simba alikuwa mzawa wa mwisho kuwa tishio katika eneo la mbele akishirikiana na John Bocco.

Huku pembeni inasikitisha zaidi. kila nafasi inayojitokeza inakwenda kwa mgeni. Labda Simon Msuva pia aliitendea haki lakini kuanzia hapo zimekuwa nafasi za wageni. Wakati mwingine tunaishia kuwalaumu viongozi wetu kwa kusajili wachezaji wa kigeni lakini tuzungumze ukweli ni winga gani bora wa pembeni ambaye hachezi Simba na Yanga.

Hapa karibuni Simba na Yanga zimejaribu wachezaji wengi wa nafasi za mbele lakini ukweli ni kwamba wanashindwa kumudu mapigo pindi wanapoingia katika timu kubwa. Dogo ambaye nilimtegemea hivi karibuni, Dickson Ambundo naye anaonekana kuniangusha.

Vipi kuhusu rafiki yangu, Habib Kyombo? Mambo yanaonekana kwenda kombo pia pale Msimbazi. Vyovyote ilivyo, leo nimemkumbuka sana Anko Ngassa. Alitamba katika nyakati zake lakini nadhani hakutamba katika nyakati sahihi. Huu ungekuwa muda mwafaka kwake.