HISIA ZANGU: Mnyama atapimwa zaidi kwenye makundi

Wednesday October 20 2021
hisia pic
By Edo Kumwembe

MNYAMA alikuwa Gaborone juzi. Alimaliza mechi ndani ya dakika tano tu za kwanza. Ilikuwa katika pambano la awali kwao kuelekea katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana. Walistahili kufanya walichofanya.

Walicheza kwa mara ya kwanza katika michuano hii bila ya kuwa na Clatous Chama na Luis Miquissone ambao wameuzwa. Nadhani hawakuwahitaji mastaa hao katika pambano la juzi. Hata aina ya mabao yao hayakuwahitaji Chama na Miquissone.

Wageni wa michuano hii walionekana kuwa wageni haswa. Walishindwa kukabiliana na kona mbili za haraka haraka zilizopigwa katika dakika tano za mwanzo za mchezo. Unaruhusu vipi mpira uanguke katika sita ya lango lako huku wapinzani wakiwa wengi kuliko wachezaji wako?

Ulikuwa ni uchanga wa wachezaji wa wenyeji katika michuano hii. Lakini zaidi ni kwamba walionekana kuwa na vipaji lakini hawakuwa na malengo makubwa wala uzoefu mkubwa katika maeneo mengi ya uwanja.

Kocha wao alijisifu kwamba alikuwa amemiliki mpira zaidi kuliko Simba. Alitegemea nini? Simba walikuwa wamekipata walichokitaka kwa urahisi zaidi kuliko walivyotegemea na wakaamua kushusha presha ya mechi. Waliwapa wenyeji mpira wao na wao wakamlinda Aishi Manula kwa nidhamu kubwa.

Kuna mashabiki wengi wa Simba ambao hawajaridhishwa na kiwango cha timu yao licha ya ushindi huu. Hapa yanakuja maswali matatu muhimu baada ya pambano hili. Je Simba hii ni ile ile? Kuna kitu cha kuangalia.

Advertisement

Kwanza kabisa kama Simba wasingepata mabao mapema tungeweza kupima kiu yao ya kutafuta matokeo haya kwa nguvu. Tungepima ëflowí yao kwa ujumla. Baada ya kufunga yale mabao mawili ni kama vile kiu iliondoka. Tungepima kiu yao ya kusaka ushindi kwa nguvu bila ya uwepo wa Chama na Miquissone.

Kwa sasa kinachosemwa ni kwamba Simba waliupoza mpira kwa sababu walipata mabao ya haraka haraka. Tuhifadhi jambo hilo kwa muda mpaka pale Simba watakapoingia katika hatua ya makundi. Tutaweza kumpima zaidi Didier Gomes da Rosa.

Hapo hapo tujiulize kuhusu kukosekana kwa Chama na Miquissone. Kulionekana juzi? Inawezekana, hasa nafasi ya Chama. Larry ëSoft Touchí Bwalya anaonekana sio mbadala wa moja kwa moja wa Chama. Bwalya anacheza taratibu zaidi kuliko Chama na anaonekana ana umiliki mzuri wa mpira lakini sio katika kupika mambo kama ilivyokuwa kwa Chama.

Upande wa Miquissone bado hatujaona sana kama kuna pengo. Tutasubiri mpaka mechi ngumu zije tuone kama kina Duncan Nyoni kama watakuwa na uwezo binafsi wa kuamua mechi zao za kimataifa kama alivyokuwa anafanya Mmakonde. Kumbuka bao lake dhidi ya Al Ahly.

Kifupi Simba hakupimwa vema na wapinzani wake katika mechi hii. Hauwezi sana kuilaumu Simba kwa sababu walifanya kazi yao ndani ya dakika tano na katika mechi hizi kitu muhimu zaidi ni kusonga kwenda katika hatua ijayo.

Huenda katika mechi ijayo uwanja wa Taifa ikatupa picha lakini haitatoa picha kubwa kama wapinzani wao wakiendelea kutoziona nyavu za Simba katika kipindi cha kwanza. Huenda Simba wakapata bao la kuongoza na kuua mechi, au wakachelewa kupata bao lakini wakaendelea kuidekeza mechi kwa sababu tayari wana mabao mawili mkononi waliyofunga Gaborone.

Natamani zaidi kuiona Simba ya katika makundi ambayo itakabiliana na timu zenye afya zaidi kuliko Jwaneng. Kikubwa zaidi ni kwamba wakati mwingine timu inakuwa bora zaidi baada ya kukabiliana na timu zilizo bora. Kwa pambano hili ni ngumu kuipima Simba halisi.

Advertisement