HISIA ZANGU: Injinia Hersi amegeuka 'sterling' wa kihindi uchaguzi mkuu wa Yanga

Wednesday June 15 2022
hisia pic
By Edo Kumwembe

KATIKA mtandao wa Wikipedia inaonyesha kwamba Injinia Hersi Said amezaliwa Julai 27, 1984. Hajafikisha miaka 40. Maisha yanaenda kasi katika mchezo wa soka nchini. Endapo atachaguliwa kuwa rais wa Yanga basi anaweza kuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kuiongoza Yanga.

Yaani tangu wakati ule watu wanaitwa wenyeviti mpaka leo ambapo Yanga wamebadilisha katiba yao na kuna cheo cha urais hajawahi kupatikana kiongozi mwenye umri mdogo kama yeye. Ana miaka 38 kwa sasa.

Wakati fulani Iman Madega alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Yanga ikaonekana alikuwa na umri mdogo kuliko kina Rashid Ngozoma Matunda waliowahi kuongoza kabla yake. Halafu akaja Yusuph Manji ambaye alionekana kuwa mdogo kuliko kina Madega. Lakini kama Hersi akifanikiwa kupenya basi atakuwa mdogo zaidi kuliko wote.

Kuna mambo yananifikirisha kiasi.

Jambo la kwanza ni namna ambavyo wanachama wa siku hizi wamebadilika. Sikuwahi kujua kwamba siku moja wanachama wataamini kwamba mpira ni pesa. Haya ndio yaliyochangia kwa kiasi kikubwa vijana wadogo kuanza kushika madaraka makubwa katika soka.

Zamani hizi zilikuwa nafasi za watu waliopitisha miaka 60 ambao wanajua jinsi jengo la Yanga au Simba lilivyojengwa miaka hiyo. Ambao wanajua namna ya kumfunga mtani. Ambao wanajua namna ya kutafuta ‘mafundi’ wa nje ya uwanja kwa ajili ya kusaidia mafanikio ya timu.

Advertisement

Lakini nyakati hizo pia maisha yalikuwa rahisi kwa viongozi hao kukusanya wachezaji. Wachezaji wote walikuwa wanacheza ndani. Usajili wao? Ilikuwa rahisi na kichekesho kidogo. Mchezaji angeweza kusajiliwa kwa kupewa feni ya ukutani na Sh2,000.

Zamani pia ilikuwa inachekesha. Wazee wa Kigoma wanaweza kumtuma mchezaji hodari mkoani humo akacheze Yanga. Yaani tawi la Yanga Kigoma linatoa zawadi ya mchezaji kuja Yanga. Ni kama walivyomtuma Said Maulidi kuja Yanga.

Zama hizi maisha yamebadilika. Kuna mchezaji ambaye ada yake ya uhamisho ni Shilingi 100 milioni. Aliyetanua goli hili alikuwa Yusuph Manji. Uhamisho wa Donald Ngoma kutoka Platinum ya Zimbabwe kwenda Yanga uliigharimu Sh120 milioni. Kuanzia hapo Yanga ikatamba Simba ikaenda chini ikajifanya inataka kuwa bize na sera ya makinda. Ilishindikana.

Manji alipoondoka Yanga rafiki zetu wa Jangwani wakahaha kweli kweli. Walianza kutupa namba za michango ya simu. Mwinyi Zahera akaibuka kuwa shujaa. Hata nahodha wa timu, Ibrahim Ajibu alitumika katika kuchangisha michango.

Simba akatawala soka letu kwa wachezaji wa bei mbaya na wenye ubora. Akatanua lango zaidi kwa kufanya vizuri Afrika. Lakini sasa Yanga kwa kupitia GSM wanajaribu kupindua meza.

Ni hapa ambapo ghafla unashangaa kukuta wanachama wanaingiwa na adabu ambayo zamani isingekuwepo.

Kwanini Injinia Hersi anagombea peke yake? Ni kitu ambacho kimenitafakarisha.

Zamani katika siasa tuliwahi kupiga kura za kumchagua Mwalimu Julius Nyerere huku kando yake kukiwa na kivuli. Hata Rais Ali Hassan Mwinyi tuliwahi kumchagua kwa picha yake na kumshindanisha na kivuli.

Katika soka haikuwahi kutokea. Zamani nafasi ya mwenyekiti ilikuwa inagombewa na watu 14 wanaochukua fomu. Makamu mwenyekiti ungeweza kukuta watu 24. Mweka hazina watu 20. Katibu mwenezi watu 13.

Sasa hivi naona umepita ukimya mzito. Kisa? Nahisi wanachama wameingiwa na adabu kwamba mpira ni pesa. Kwa hiyo ambaye alikuwa anajaribu kuipitisha Yanga katika kipindi cha matanuzi ya pesa nje ya uwanja ndiye ambaye wameona wamuangushie mzigo wa kuwapeleka nchi ya ahadi.

Hapa najiuliza mambo mawili. Wale wenye uwezo wa kugombea wanahisi kwamba kuendesha timu nyakati hizi ni mzigo ndio maana hawataki kugombea? Au wanaogopa kuonekana wasaliti endapo watajitokeza kumpinga Injinia Hersi? Inawezekana majibu yote mawili ni sahihi.

Sikutegemea kama kuna siku Simba au Yanga itakuwa na mgombea mmoja wa nafasi ya mwenyekiti wa urais. Bwana Manji alijikuta mbele ya wagombea wenzake wawili katika uchaguzi wake uliompeleka madarakani kama mwenyekiti wa Yanga. Walikuwepo Edgar Chibura na John Jambele.

Lakini leo Hersi yuko peke yake. Najiuliza kama ni adabu iliyopitiliza kwa Injinia pamoja na mmiliki wa GSM, Ghalib Mohamed au kuna jambo jingine? Labda baada ya Simba kutikisa katika miaka ya karibuni basi ujio wa kina Mayele umewapa nidhamu na mafanikio ya msimu huu yamewafanya kuwa watiifu waliopindukia.

Kuna ambao wanaamini usajili wa Aziz Ki ni kama kampeni za wazi kwa Injinia, Hersi lakini ukichunguza ni kwamba kama ni kampeni basi alianza miaka mitatu iliyopita. Tangu alipomrudisha Haruna Niyonzima klabuni na kina Ditram Nchimbi.

Halafu wakaja kina Michael Sarpong na David Molinga. Halafu mpaka sasa wamekuja kina Khalid Aucho, Djuma Shaban, Fiston Mayele, Jesus Moloko na wengineo. Na wameonekana kuimarika zaidi. Nadhani kama ni kampeni basi zilianzia huku.

Tukiachana na hilo ni wazi kwamba kampeni hazijaanza. Hatuhitaji kumpigia kampeni za kumpinga au kumsapoti Injinia Hersi kwa sasa. Lakini ni bora tu tuanze kusapoti mwamko wa vijana kuanza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi nchini, hata katika michezo.

Labda kuna mambo mapya wanayoweza kuyaleta lakini kitu cha msingi zaidi ni kwao kujua kwamba kuna matumaini makubwa ya mashabiki dhidi yao. Isiishie katika masuala ya kunyang’anyana kina Aziz Ki tu au kufika robo fainali ya michuano ya CAF.

Mashabiki wanataka kitu zaidi. Wanataka kuona timu zao zinakuwa na miundominu ya kisasa katika soka. Viwanja vizuri vya mazoezi, kambi nzuri kwa timu, vifaa bora vya wachezaji na mashabiki na mengineyo. Haishangazi kuona siku hizi jezi mpya za klabu zao zinakuwa dili.

Lakini zaidi kuwe na msingi wa mafanikio ambao pindi mtu mmoja anapoondoka klabuni bado klabu isiterereke kifedha.

Kuna viongozi wetu wanakuwa wabinafsi. Wanapenda wakumbukwe pale wanapoondoka. Mara nyingi hawafanyi mambo ya msingi ya kuiingizia klabu mapato ili hata kama hawapo klabu iendelee kuwa imara.

Kwa mfano, haikutazamiwa kama Yanga ingetetereka vile siku Manji angeondoka. Kumbe ndio tukagundua kwamba hakuweka misingi ya Yanga imara bila ya yeye. Leo hatujui kama Mohamed Dewji anafanya hivyo kwa Simba. Tutajua kama ataamua kuondoka zake.

Advertisement