HISIA ZANGU: Ilinishangaza Simba walipomsaini Jeremiah Kisubi

MASHABIKI wa Simba wamewahi kumuona Kipa Jeremiah Kisubi katika lango? Hapana. Binafsi sijawahi kumuona akidaka. Mara ya mwisho nilimuona akichezea Prisons. Nikasikia amesajiliwa Simba. sasa hivi anakwenda zake Mtibwa kwa mkopo.

Kuna maswali mengi kuhusu Kisubi. Kwanini Simba ilimsajili? Sielewi. Kwanza inawezekana tamaa ya viongozi. Kwamba wanajaribu kuwa na wachezaji wazuri kila idara. Lakini unawezaje kuwa na makipa watatu bora bila ya sifa tofauti?

Aishi Manula ni kipa mzuri. Beno Kalolanya ni kipa mzuri. Kisubi ni kipa mzuri. Nini sifa ya kipa wa pili ambaye ni Kakolanya? Sifa yake kubwa ni kuwa hodari na kumtia presha Aishi Manula. Sifa yake kubwa ni kupambana kuwa kipa wa kwanza.

Nini sifa ya kipa wa tatu. Wazungu wanamtengeneza kipa wa tatu katika makundi mawili. Kundi la kwanza awe na umri mdogo. Anaweza kuwa kipa namba moja wa timu ya vijana. Huyu anakua taratibu huku akichota uzoefu. Hana presha kubwa ya kuwania namba kwa sababu umri wake haujafika. Anaisaka nafasi yake taratibu.

Kundi jingine ni la kipa mwenye umri mkubwa. Veterani ambaye ana miaka zaidi ya 35. Yupo kwa ajili ya dharura. Tayari alishatamba kwingine na ubora wake umepungua. Kwa sasa anaweza kuwasaidia kudaka kwa kutumia uzoefu zaidi pindi mambo yanapoharibika kwa kipa wa kwanza.

Kwa mfano, pale Ulaya kuna kipa anaitwa Willy Caballero. Ana miaka 40. Chelsea na Manchester City wamewahi kumtumia kwa kazi hii hii ya kuwa kipa wa akiba. Wakati mwingine anarudi kuwa kipa wa pili lakini muda mwingi ni kipa wa tatu.

Nimesoma mahala Kisubi ana umri wa miaka 32 tu. Huu ni muda ambao kipa anakuwa katika ubora wake. Ni umri ambao kipa anazidi kuwa kama mvinyo. Hakupaswa kwenda Simba kama kipa wa tatu. Alipaswa kwenda kama kipa wa pili au kipa mkuu. Nikashangaa Simba wanamchukua Kisubi.

Ambacho Simba walipaswa kufanya ni kumsaka kipa yeyote kinda mwenye urefu mzuri ambaye angeweza kuwa kipa wa tatu. Kipa ambaye wangempika na baada ya miaka michache angeweza kusimama katika lango lao.

Ni kama vile ambavyo Yanga walikuwa wanakwenda taratibu na Ramadhan Kabwili. Makipa wa namna hii kama umri unaanza kusogea huku wakiwa hawajafanikiwa kuichukua nafasi ya kwanza huwa wanatolewa kwa mkopo. Ndio maana kuna wakati nilikuwa nawashangaa Yanga kwanini walikuwa hawataki kumtoa Kabwili kwa mkopo.

Umri wa Kisubi haukupaswa kumfanya awe kipa wa tatu hasa ukizingatia kwa kiwango chake alichokuwa anaonyesha Prisons alistahili kukaa katika lango lolote la timu kubwa. Iwe Yanga, Simba au Azam. kwanini alikwenda kuwa kipa wa tatu?

Kwanza kabisa Simba yenyewe haikujitendea haki. Walipaswa kumfanya Kisubi kuwa kipa wa pili na kuachana na Kakolanya. Halafu kipa wa tatu awe kijana. Wangeokoa pesa nyingi katika bajeti yao ya dirisha hilo. Hayakuwa matumizi mazuri ya pesa.

Lakini upande mwingine nachelea kudai kwamba Kasubi pia hakujitendea haki. Soka la nchi yetu lina mfumo mgumu. Kama hautakiwi na Simba, Yanga au Azam basi haupati pesa. Ukitakiwa na moja kati ya hizi timu hauwezi kuacha.

Wakati mwingine tunawalaumu wachezaji wanaokwenda katika timu hizi kwa madai kwamba wanakwenda kuua vipaji vyao lakini tunashindwa kuelewa kiasi gani cha pesa wamewekewa mezani. Zinakuwa ni pesa ambazo hawajawahi kuziona maishani.

Bahati mbaya klabu nyingine ambazo wangeweza kwenda kucheza huwa hazina uwezo wa kuweka mezani madau ambayo Simba, Yanga na Azam huwa wanatokea. Tofauti ya walionacho na wasionacho ni kubwa katika soka letu.

Barani Ulaya sawa kuna klabu tajiri lakini klabu nyingine za kawaida zina mishahara mikubwa. Kuna mchezaji anaweza kuamua kwenda kuendeleza kipaji chake kwingine huku akiwa analipwa vizuri. Ni tofauti na soka la Tanzania.

Kwa mfano, Erling Haaland wakati anatoka Red Bull Salzburg alikuwa anatakiwa na klabu mbalimbali kubwa zaidi duniani. Hata hivyo wakala wake, Mino Raiola akaamua kumuweka Borussia Dortmund ambayo haipo daraja la akina Bayern Munich, Manchester United, Barcelona wala Real Madrid.

Hata hivyo klabu ambayo alikwenda, Dortmund, inaweza kumlipa vizuri tu akaendesha magari ya kifahari na kuwa tajiri. Wakala wake alitaka Haaland apate uzoefu zaidi na akomae zaidi. Na ndicho ambacho kinatokea kwa sasa.

Tatizo kwa hapa hauwezi kumwambia Denis Nkane asubiri wakati anatakiwa na Yanga na Simba. hauwezi kumwambia aende Coastal Union kwanza wakati akisubiri kwenda Yanga. Jaribu kufikiria. Inaweza Haaland amekosa Pauni 100,000 kwa wiki kwa kutokwenda Real Madrid au Bayern Munich, lakini Dortmund wanaweza kumlipa Pauni 50,000 kwa wiki.

Kwa Nkane hapa nchinikama alipaswa kulipwa Pauni 100,000 kwa wiki basi klabu ya kawaida ingemlipa Pauni 5,000 kwa wiki. Pengo ni kubwa kati ya walionacho na wasionacho. Ukijiweka katika viatu vya akina Kasubi ndio utaelewa kwanini wanasaini klabu hizi bila ya kujali kwamba ataenda kuwakuta Aishi na Kakolanya.

Usingeweza kumshauri Kisubi aachane na Sh50 milioni kwa ajili ya kuhofia nafasi yake. Hawezi kuacha kiasi hicho kwa hofu ya kuwekwa benchi. Hawezi kuacha kiasi hicho na kwenda Biashara Mara kwa ajili ya kulinda kipaji chake. Katika suala lake sina tatizo na Kisubi. Nina tatizo na Simba. Kwanini waliamua kumchukua Kisubi. Hata kama alipatikana bure baada ya mkataba wake kumalizika lakini sayansi ya mpira inaonyesha haukuwa uamuzi sahihi kwao kumchukua.

Manchester City hata kama wana pesa lakini hawawezi kuwanunua Ederson, Allison Becker na Manuel Neur kukaa katika lango moja. Sayansi ya mpira inakataa. Kipa wa kwanza hadi wa tatu lazima wawe na sifa tofauti katika vigezo kadhaa.