Hii sasa sifa

Sunday April 04 2021
BRUNO PIC

LONDON, ENGLAND

HII sasa kufuru kama si kutaka sifa. Kuna timu nne sasa hivi zinazotajwa kuwa na uwezo wa kumnasa Erling Haaland kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kutoka Borussia Dortmund.

Kwenye Ligi Kuu England, miamba inayopewa nafasi kubwa ya kumnasa Haaland ni Manchester City, ikielezwa kwamba ndio wenye jeuri ya kulipa mshahara anaotaka, Pauni 600,000 kwa wiki.

Na Man City hawana ujanja, wanataka kulitumia dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kunasa straika mpya kwa sababu watakwenda kumpoteza mshambuliaji wao namba moja, Sergio Aguero, ambaye ataondoka Etihad kwa sababu mkataba wake utakuwa umefika tamati. Ripoti zinafichua, Man City wapo tayari kulipa mshahara wa Pauni 600,000 kwa wiki, hiyo ni nje ya ada ya uhamisho, ambayo itakuwa si chini ya Pauni 150 milioni.

Kwenye hilo la mshahara wa Pauni 600,000 kwa wiki, timu nyingine inayoweza kulipa ni Paris Saint-Germain.

Lakini, kama Man City itamnasa Haaland na kumlipa mshahara huo, basi straika huyo atakuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya soka la England, akipiku rekodi ya Alexis Sanchez.

Advertisement

Kwa sasa, mchezaji anayeongoza kwa mshahara mkubwa ni kipa wa Manchester United, David De Gea, anayepokea Pauni 375,000 kwa wiki na kufuatiwa na nahodha wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang anayelipwa Pauni 350,000 kwa wiki, akiwa kinara huko Emirates baada ya Mesut Ozil kuondoka.

Kevin De Bruyne anashika namba tatu, ambapo Man City inamlipa mshahara wa Pauni 320,000 kwa wiki, na kufuatiwa na staa wa Chelsea, Kai Havertz, anayekamilisha tano bora akipokea Pauni 310,000 kwa wiki na winga wa Man City, Raheem Sterling yupo namba sita akiwa analipwa Pauni 300,000 kwa wiki.

Kwenye namba saba, yupo Paul Pogba, anayelipwa Pauni 290,000 kwa wiki huko Man United, huku mchezaji mwenzake kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, Anthony Martial akishika namba nane kwa kulipwa Pauni 250,000 kwa wiki, sawa na Thomas Partey wa Arsenal, akipokea kiasi kama hicho na anayekamilisha 10 bora ya wenye mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa ni straika Sergio Aguero, anayelipwa Pauni 230,000 kwa wiki huko Man City. Mishahara hiyo, haimhusu Gareth Bale, ambaye mshahara wake wa Pauni 650,000 kwa wiki unaolipwa na timu mbili, Tottenham Hotspur anakocheza kwa mkopo msimu huu na Real Madrid ambayo ni timu yake mama.

Balaa la mshahara wa Haaland akitua huko Etihad ina maana, kile atakachovuna ndani ya wiki tu, kitatosha kumlipa mshahara Pogba na Sterling na chenji inabaki. Au mshahara huo mmoja tu wa Haaland, utatosha kuwalipa masupastaa wawili matata kabisa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, De Bruyne na Bruno Fernandes, ambaye kwa wiki anapokea Pauni 180,000 huko Old Trafford. Hiyo ndo kufuru ya mshahara wa Haaland akitua Etihad, kwamba unaweza kulipa mishahara kwa mafungu ya mastaa kibao kwenye vikosi vya Arsenal, Man United, Chelsea, Spurs, Liverpool na hata Chelsea, ambazo ni timu za Big Six za EPL.

Advertisement