Hii ni sababu ya kifo cha Mobby

TASNIA ya soka hapa nchini ilipata pigo mara baada ya aliyekuwa beki wa Mtibwa Sugar, Iddy Mobby kufariki dunia siku ya Jumapili Machi 5, 2023 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru ilieleza kuwa alianza kujisikia vibaya ghafla na kupelekwa hospitali ya Kiwanda cha Mtibwa.
Katika kituo hicho waliona hali haikua imara na ilikuwa nje ya uwezo wao hivyo baadaye akapewa rufaa kwenda hospitali ya Misheni ambao nao pia walimpa rufaa ya kwenda hospitali ya Benjamini Mkapa.
Mobby aliyekuwa na umri wa miaka 32, alifariki saa 7 usiku wakati akiendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo ambapo chanzo cha kifo chake kikielezwa ni mshtuko.
Ilielezwa kuwa mchezaji huyo alianza kulalamika kuumwa kichwa na kuishiwa nguvu ndipo ikalazimika kukimbizwa katika huduma za afya za juu kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Historia inaonyesha kuwa aliwahi kupatwa na hali hiyo Machi 4 mwaka huu mkoani Morogoro akiwa katika mazoezi binafsi ikiwa ni maandalizi ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya KMC.
Jicho la kitabibu linachukulia dalili zilizojitokeza na kifo cha ghafla na matatizo ya moyo ambayo ndio yanashika namba moja kwa kusababisha vifo vya ghafla.
Mshtuko wa mwili ni hali ambayo inampata mtu ghafla ikiambatana na kushuka kwa mapigo ya moyo kunakoweza kusababishwa na upungufu wa damu, ukosefu wa hewa ya oksijeni katika ubongo, mzio, mshtuko wa ghafla wa hisia.
Mtu aliyepata mshtuko wa mwili huwa na dalili kama kuishiwa nguvu, ngozi kuwa baridi, kupumua kwa shida, kasi ya unenepaji wa mishipa ya damu kuwa juu na mboni ya jicho kutanuka.
KICHWA KUUMA NA KUISHIA NGUVU
Viashiria vilivyojitokeza kwake inaonyesha kuwa huenda alikuwa na matatizo ya moyo yaliyojificha. Baadaye watalaam wa Afya wa Hospitali hiyo ilielezwa kuwa alipata mshtuko.
Watu wa karibu wa mchezaji huyo na wachezaji wenzake wanaeleza kuwa mchezaji huyo alikuwa na matatizo ya moyo ambayo hayakuwa tishio na majukumu yake ya soka.
Dalili ya kwanza ya kuumwa na kichwa linaweza kusababishwa mara kwa mara na uvamizi wa vimelea ikiwamo parasaiti wa malaria au shambulizi la bakteria, magonjwa ya moyo ikiwamo shinikizo la juu la damu au matatizo ya mishipa ya damu.
Vile vile kutokunywa maji ya kutosha au kupungukiwa maji mwilini, usumu katika damu, upungufu wa damu mwili, ubongo kukosa hewa safi, uchovu wa mwili, msongo wa mawazo, kukosa usingizi, magonjwa ya figo na ini, sukari kushuka na uvimbe katika ubongo.
Jicho la kitabibu likiangazia dalili ya pili ya kukosa nguvu inaweza kusababishwa na sukari ya mwili kushuka, kukosa hewa safi ya oksijeni, ubongo kukosa lishe ya damu na mapigo ya moyo kushuka.
MATATIZO YANAYOCHANGIA VIFO VYA GHAFLA
Ni kawaida ikatokea sababu ya kifo cha ghafla isijulikane moja kwa moja, lakini yapo matatizo ya kiafya yakuhusishwa na kifo cha ghafla ikiwa vinavyotokea tukiwa usingizini.
Ukiacha matatizo ya moyo kwa ujumla, katika sehemu nyingine za mwili yaani ubongo na figo vinaweza kupata matatizo ya kiafya na kusababisha kifo cha ghafla.
Moyo ndiyo ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, magonjwa au matatizo yake huwa ni ya kimya kimya na ndiyo yanayoongoza kusababisha vifo vya ghafla duniani.
Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimya kimya pasipo kujijua kwa anayeugua, mara nyingi watu hugundulika wakiwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.
Mara nyingi kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo ni sababu kubwa inayosababisha matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo.
Mishipa ya damu ya moyo ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa au kupata kiasi kidogo sana.
Hali hii husabisha misuli kushindwa kufanya kazi yakusukuma damu kwa ufanisi wa kawaida, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama.
Misuli ya moyo kututumka pia ni sababu mojawapo kwani husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo yakupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.
Sababu nyingine ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo ya kawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valve za moyo na kuzaliwa na moyo wenye hitilafu.
Vilevile uwepo wa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kuwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.
Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo lakini yanaweza leta vifo vya ghafla ni kama vile sumu, mrundikano wa taka mwili zilizo sumu, matatizo ya mfumo wa hewa, kupaliwa na kitu katika mfumo wa hewa, kuvuta hewa chafu na ajali katika ogani nyeti.
Hizi ni baadhi ya sababu zinazosababisha kutokea kwa vifo vya ghafla kwa mtu yoyote yule. Ni vizuri kuyajua haya kuchua hatua za mapema kabla ya madhara kutokea.
CHUKUA HII
Wanasoka wanahitajika kufanyiwa uchunguzi wa kina ikiwamo uchunguzi wa Moyo na mfumo wa damu kwa kuzingatia muongozo wa upimaji afya za wachezaji wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA.