Hii ni Azamlona, yaani ni kama Barcelona ya Pep

JUMAMOSI ya Julai 30 Azam FC ilianza wiki ya pili ya kambi ya mazoezi hapa El Gouna Misri.

Tofauti na wiki ya kwanza, wiki hii imeanza kwa mazoezi ya kukabia juu pressing kwa kasi ya hali ya juu sana.

Kocha Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’ anataka mpira ulio kwa adui upatikane ndani ya sekunde sita baada ya kuupoteza.

Anahimiza kasi ya kuusaka mpira iwe kubwa zaidi mara tu baada ya kuupoteza na wachezaji waongeze kasi zaidi wanapopoteza mpira kuliko hata wanapokuwa na mpira.

Sasa huo msako wake wa kuutafuta mpira ndiyo kiboko yake.

Kwanza wanaanza kubanwa wapinzani ambao hawana mpira ili mwenye mpira akose wa kumpasia.

Halafu ndiyo anavamiwa mwenye mpira, lazima tu aupoteze, kwa kunyang’anywa au kuupiga nje.

Hili linafanyika kwa haraka kiasi kwamba wenye mpira wanajikuta kwenye msako mkubwa kama wa operesheni maalumu ya kipolisi.

Hii ndiyo staili iliyompa umaarufu na mafanikio makubwa kocha wa sasa wa Manchester City, Pep Guardiola, enzi zake akiwa FC Barcelona.

Katika makala maalumu kuhusu aina yake ya ufundishaji na uchezaji kati ya 2008 na 2012 katika ile Barcelona ya moto ya Xavi-Xavi again.

Moallin anasema anataka Azam FC icheze kwa wa kumiliki mpira na kushambulia kwa kasi kiasi cha kutowapa wapinzani muda wa kujipanga uwanjani.

‘Kucheza kama Barcelona ni mbali sana, nataka tuch eze vizuri tuwaburudishe mashabiki wetu huku tukipata matokeo bora.

Wachezaji bora tunao, tunachotaji ni mbinu bora na moyo wa kujitoa wa wachezaji.

Tuko hapa Misri na tunafanya mazoezi kwenye jua kali sana, lengo ni kujenga ustahimilivu kwa wachezaji.’

Moallin yuko sahihi, kucheza kama Barcelona ile ya Pep ni kitu kigumu sana kwa sababu hata Pep mwenyewe kashindwa kufanya hivyo baada ya kuondoka, na Barcelona wenyewe wameshindwa kucheza tena vile baada ya Pep

Lakini kucheza vizuri na watu kujikuta wakiifananisha Azam hii na Barcelona ile, inawezekana.

‘Labda, kwa sababu ukiangalia tulivyocheza dhidi ya Wadi Degla, tulijitahidi sana kumiliki mpira na kushambulia kwa kasi.

Lakini ile ilikuwa wiki ya kwanza ya pre season ambayo kwa kawaida huzingatia sana utimamu wa mwili.

Matumaini yangu ni kwamba katika wiki hii ya pili ambayo sasa tutacheza zaidi mpira na kufundishana mbinu, timu itaimarika zaidi.

Moallin anaonekana amekamia sana safari na hataki hutani hata kidogo. Anakataza kutoa pasi za kufurahisha majukwaa lakini bila kusaidia timu.

Anawaambia wachezaji kwamba mtu akipoteza mpira kwa pasi ya masihara, anatolewa uwanjani hata kama ni sekunde ya kwanza ya mchezo.

Haya ni maelekezo mazito yanayoonesha ni namna gani kocha hataki masihara.

Msimu wangu wa kwanza na Azam FC ulinifundisha mengi sana. Tulianza vizuri sana na hata kwenye Mapinduzi tulicheza vizuri sana.

Lakini ghafla mambo yakabadilika, tukawa hatuchezi vizuri na mbaya zaidi hatupati matokeo.

Hapo kila mtu alichanganyikiwa na hata wakubwa wangu wangefanya maamuzi ya kuniondoa nisingewalaumu.

Lakini kwa Imani yao kwangu, nadhani nina deni kubwa la kulipa ili kuthibitisha kwamba hawakukosea kuendelea kuniamini.

Kocha huyo raia wa arekani mwenye asili ya Somalia anataka kuandika historia yake na ya Azam.

Nataka tufike hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika, hiyo ndiyo ndoto yangu.

Nikifanikiwa hilo nadhani sitokuwa na deni kubwa. Lakini hata hivyo, siwezi kujitoa kwenye mbio za ubingwa.

Hii timu tunayoiandaa inastahili kuwa mabingwa kabisa. Lakini ubingwa wa ligi unahitaji muendelezo bora wa kiwango msimu mzima, na ndicho tunachokitafuta huku Misri

Kwa kuwaangalia Azam FC wanavyofanya mazoezi unaweza kuona picha kubwa sana ya baadaye ya klabu hiyo.

Ili uweze kucheza soka la kumiliki mpira na kupigiana pasi nyingi unahitaji kuwa na wachezaji wenye ufundi mwingi wa kuuchezea mpira, kitu ambacho Azam FC imebarikiwa nacho, hasa eneo la kiungo.

Tape Edinho, Yahya Zayd, Ibrahim Ajib, Cleophas Mkandala, Kenneth Muguna, Isah Ndala na James Akaminko.

Hawa ni wachezaji wenye uwezo mkubwa sana wa kuuchezea mpira yaani technical players.

Pia kuna viungo wa pembeni kama Tepsie Evans, Idd Nado, Kipre Junior, Ayoub Lyanga na Ismail Aziz Kader.

Hawa ni wachezaji wanaoweza kukupa uhuru ya kucheza unavyotaka kwa sababu unakuwa na uhakika wa kumiliki mpira.

Lakini kocha anaona hiyo haitoshi.

Ni rahisi sana kuamini kwamba wachezaji aina hiyo wanaweza kukusaidia.

Lakini vipaji vyao pekee havitoshi kwa soka la ushindani la kisasa, inatakiwa kujitoa kwa kiasi kikubwa sana.

Messi, Ronaldo na hata Lewandowski ni wachezaji wenye vipaji vikubwa sana.

Lakini kiwango chao cha kujitoa ni kikubwa sana, vikubwa kupita maelezo.

Kwa hiyo tunataka wajitoea sana ili vipaji vyao vitusaidie.

Msimu uliopita nilifanya mahojiano na kusema Ajib simtumii kwa sababu hajitoi vya kutosha. Hiyo ipo hata kwa Yahya Zayd na wachezaji wengi duniani wenye vipaji vikubwa, kujitoa kwao ni kidogo sana.

Kwa hiyo ni lazima wajitoe sana. Na baada ya yale mahojiano Ajib akaanza kujitoa, na nikawa nampanga.

Kama utakumbuka hata kadi nyekundu aliyoipata Dodoma, ilitokana na kujitoa na sikumlaumu.

Azam inatarajiwa kucheza mechi ya pili ya kirafiki hapa Misri mapema juma lijalo dhidi ya Suez SC.