Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndiyo tofauti ya miguu ya Clement Mzize

Mzize Pict

Muktasari:

  • Mzize anaongoza orodha kwa kufunga mabao tisa, akimshusha Elvis Rupia wa Singida Black Stars, aliyekuwa kinara hadi ligi inasimama akiwa na mabao manane (hii ni kabla ya mechi za jana).

UMEIANGALIA orodha ya wafungaji mabao katika Ligi Kuu Bara? Pale juu kuna kinara wa mabao, nyota wa Yanga, Clement Mzize akiwaburuza wachezaji wa kigeni katika mbio hizo kwa sasa.

Mzize anaongoza orodha kwa kufunga mabao tisa, akimshusha Elvis Rupia wa Singida Black Stars, aliyekuwa kinara hadi ligi inasimama akiwa na mabao manane (hii ni kabla ya mechi za jana).

Nyota huyo wa Yanga alifikisha mabao hayo baada ya Jumatano kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya KenGold na kufikisha idadi hiyo akiwafunika mastaa wa kigeni anaocheza nao Jangwani na hata wa timu nyingine wakiwamo wale wa Simba.

Hapa chini ni aina ya mabao aliyofunga Mzize na kumbeba katika orodha hiyo hadi sasa wakati Ligi Kuu ikiwa imemaliza raundi ya 17 na kujiandaa kuingia raundi ya 18 kuanzia kesho Jumapili.

MZ 01

Mfungaji Bora huyo wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa msimu uliopita ni kati ya wachezaji walioiwezesha Yanga kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiipiku Simba kwa tofauti na alama moja, Yanga ikiwa na 45 na watani wao wakiwa na 44 kila moja ikicheza mechi 17. Endelea.

TOFAUTI YA MIGUU YA MZIZE 

Kwenye mabao tisa aliyofunga Mzize hadi sasa manane ameyafunga kwa mguu wa kulia ambao ndio mguu hatari zaidi kwa mshambuliaji huyo  akiwa uwanjani kwenye kutikisa nyavu.

Mzize msimu huu hajafunga bao lolote kwa mguu wa kushoto, ingawa ni mguu ambao anaweza kuutumia kufunga kama ambavyo alifanya msimu uliopita alipofunga dhidi ya Azam FC.


NDANI YA BOKSI

Mzize kwenye mabao yake hayo amefunga mara sita akiwa ndani ya eneo la hatari ambapo ni mabao mawili pekee ameyafunga kwa mguu akiwa nje ya eneo la hatari, hii ni kuonyesha mwamba huyu hutakiwi umruhusu aingie ndani ya boksi kwani hakuachi.


MZ 05

BAO LA KICHWA

Mshambuliaji huyo ambaye anatajwa kuwa na ofa nyingi za klabu za Afrika na hata Ulaya, msimu huu amefunga bao moja pekee la kichwa alipotupia mawili katika mchezo wa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji akitumia kona iliyopigwa na kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua.


HANA PENALTI

Mzize hahitaji penalti kufunga mabao yake kwani ndani ya msimu huu hajashughulika na pigo lolote la penalti huku mabao manane akiyafunga kwa mashambulizi ya wazi wakati bao moja pekee la kichwa ndio alilofunga kwa mpira wa kutengwa kwa kona ya Pacome.

Kutofunga kwake penalti kunamfanya nyota huyo kuwa na pointi nyingi kulingana na kanuni ya mabao katika tuzo ya Mfungaji Bora, kwani kufunga bao la kawaida lina alama mbili na la penalti ni pointi moja tu, ikiwa na maana kwa pointi hadi sasa Mzize amekusanya 18 katika mabao aliyonayo.


MZ 02

AMEVUNJA REKODI BINAFSI

Msimu uliopita Mzize alifunga mabao saba, lakini msimu huu ndani ya mechi 17 ameshaivunja rekodi yake akifunga mabao tisa wakati akisaliwa na michezo 13 kabla ya kumaliza msimu.

Kama ataendelea na mwendo huo wa kutupia ni wazi, mshambuliaji huyo anaweza kumaliza na mabao ya kutosha na pengine kuvuka rekodi ya nyota wa kizawa kufunga mabao mengi ambayo inashikiliwa na John Bocco na Feisal Salum kufunga 19 kwa miaka ya sasa, lakini akijiweka katika mbio za kuifikia rekodi ya muda wote ya mabao 26 iliyowekwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.


MZ 03

BADO TISA

Kuna timu tisa tu zimesalia kufungwa na mshambuliaji huyo msimu huu ambazo ni Simba, Azam, Singida Black Stars, JKT Tanzania, Mashujaa, Pamba, Pamba, Namungo na KMC, huku sita zilizoruhusu mabao yake ni Kagera, Tabora United, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Fountain Gate na KenGold


KAGERA WANYONGE

Kama ulikuwa hufahamu Mzize bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu tangu apandishwe na Yanga alifunga dhidi ya Kagera Sugar mchezo uliopigwa pale CCM Kirumba jijini Mwanza na msimu huu ameshaifunga timu hiyo kwenye mechi zote mbili za nyumbani na ugenini.

MZ 04

YEYE ANAONAJE?

Mzize ameliambia Mwanaspoti mapema kwamba anafurahia kufunga mabao mengi kadri anapopata nafasi uwanjani, furaha yake ni kuona timu inapata matokeo mazuri.

“Kufunga ndio kazi ya mfungaji, mani naona raha kila ninapoisaidia timu, kwa ishu ya Mfungaji Bora ni maperma kuzungumza kwa sasa, kwani ligi bado, lakini kiu ni kuona Yanga inatetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo,” alisema Mzize.

Makocha walioondoka Yanga, Miguel Gamondi na Sead Ramovic kwa nyakati tofauti wakikaririwa wakimsifia Mzize kwamba ni mmoja ya wachezaji wanaozingatia maelekezo na pia kubebwa na umri, kasi na uwezo sambamba na kipaji cha soka, na uzuri anatumika katika nafasi zaidi ya moja uwanjani.

“Ni moja ya hazina ya taifa, ni mchezaji anayejua kutumia nafasi, akiendelea kuwa na utulivu na kuacha papara ni dhahiri atafika mbali zaidi, kwani ana kipaji kikubwa cha soka na kujituma uwanjani bila kuchoka,” anasema Gamondi aliyemnoa kwa misimu karibu miwili kabla ya kuondoka Yanga.