HESABU 4 ZAIBEBA SIMBA

Sunday April 18 2021
hesabu pic2
By Mwandishi Wetu

SIMBA imetinga kibabe hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuongoza kundi A la mashindano hayo na inapewa nafasi kubwa ya kutinga nusu fainali ingawa haitajwi katika orodha ya timu zinazoonekana zinaweza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Nafasi kubwa ya timu itakayotwaa ubingwa katika mashindano hayo zimekuwa zikipewa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia na Al Ahly ya Misri ambazo kila mara zimekuwa zikifanya vyema pindi zinaposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo takwimu za Simba yenyewe na baadhi ya wachezaji wake zinaiweka Simba katika nafasi kubwa na nzuri ya kushindania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwani nyingi zimekaribiana, kuwa sawa au kuzipiku zinazopewa kipaumbele cha kuondoka na taji hilo msimu huu.


Ulinzi Simba kiboko

Ukiondoa Wydad Casablanca ya Morocco ambao nyavu zao zimetikiswa mara moja tu katika hatua ya makundi, sio Al Ahly, Esperance au Mamelodi Sundowns ambayo inafua dafu mbele ya safu ya ulinzi ya Simba ambayo imeruhusu mabao mawili tu kwani timu hizo zimefungwa zaidi ya idadi hiyo ya mabao ambayo wawakilishi hao wa Tanzania nyavu zao zimetikiswa.

Advertisement

Al Ahly imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano, Mamelodi imefungwa mabao manne huku Esperance wenyewe wakifungwa mabao sita.

Haijaishia tu kwa kuruhusu idadi ndogo ya mabao bali pia kipa wa Simba, Aishi Manula amewapiga bao makipa wa Esperance, Mamelodi na Al Ahly kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa ambapo katika mechi tano alizocheza, tatu alimaliza bila kufungwa bao.

Kipa wa Al Ahly, Mohamed El Shenawy hajafungwa katika mechi tatu kati ya sita za makundi, kipa wa Mamelodi, Denis Onyango amecheza mechi mbili tu bila kuruhusu bao kati ya nne za hatua ya makundi alizopangwa wakati Farouk Ben Mustapha wa Esperance yeye nyavu zake hazijatikiswa katika mechi moja tu kati ya tano alizoidakia timu hiyo katika hatua ya makundi.

Miquissone, Chama wawapa jeuri

Kama kuna wachezaji wanaoifanya Simba iwe na imani ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu basi nyota hao ni Clatous Chama na Luis Miquissone.

hesabu pic

Wawili hao wameonekana kukabana koo na hata kuwafunika baadhi ya nyota wa klabu za Esperance, Mamelodi, Wydad Casablanca na Al Ahly katika vipengele tofauti.

Kwanza wawili hao kila mmoja yuko juu katika chati ya wachezaji waliohusika na idadi kubwa ya mabao katika hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu.

Themba Zwane wa Mamelodi anaungana na Miquissone na Chama kuongoza kwa kuhusika na idadi kubwa ya mabao ambapo kila mmoja amehusika na mabao matano sawa na Mohamed Magdi ‘Afsha’ wa Al Ahly.

Miquissone amefunga mabao matatu na kupiga pasi mbili za mabao wakati Chama amepiga pasi tatu za mwisho na kupachika mabao mawili kama ilivyo kwa Zwane.

Chama anaungana na Themba Zwane katika chati ya wachezaji wanaoongoza kwa kupiga pasi za mwisho wakati Miquissone yeye anaongoza chati ya nyota waliofunga idadi kubwa ya mabao katika hatua ya makundi akiwa sawa na Ayoub El Kaabi (Wydad), Amir Sayoud (CR Belouizdad), Mohamed Ali Ben Romdhane (Esperance), Mohamed Sherrif (Al Ahly)

Ukiondoa hivyo, Miquissone na Chama pia wapo juu katika chati ya nyota wenye wastani bora wa ufanisi kwa mechi katika hatua ya makundi.

Miquissone anashika nafasi ya nne akiwa na alama 7.72 kati ya 10 wakati Chama yuko nafasi ya tano akiwa na alama 7.7 na mchezaji mwingine wa Simba aliye katika 10 bora ni Mohamed Hussein ambaye ana pointi 7.45

Katika orodha ya wachezaji wanaoongoza kwa kukokota mpira, Chama yuko nafasi ya pili nyuma ya Shaban Djuma akiwa na wastani wa kukokota mara 2.8 kwa mechi na Miquissone yuko nafasi ya nne akiwa nafasi ya nne akiwa na wastani wa kukokota mara 2.6 kwa mechi

Miquissone pia anaongoza chati ya wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi za hatari ambapo amefanya hivyo mara nne

Mugalu naye yumo

Mshambuliaji Chris Mugalu anaongoza katika orodha ya wachezaji walioshinda umiliki wa mpira mara nyingi katika eneo la hatari la timu pinzani akiwa amefanya hivyo mara tano.


Lwanga Saluti

Kiungo namba sita wa Simba, Lwanga Taddeo ameingia katika chati mbili tofauti za nyota waliofanya vyema katika hatua ya makundi

Kwanza yupo nafasi ya tisa katika wachezaji waliopiga pasi sahihi akiwa na wastani wa pasi 50 kwa mechi lakini pia yuko nafasi ya sita katika orodha ya wachezaji waliopiga ‘tackling’ nyingi akifanya hivyo kwa wastani wa mara 2 kwa mechi.

Advertisement