Hawachuji, miaka 20 kwenye gemu na bado wakali

HABARI ndiyo hiyo! Jamaa hawachuji kwenye gemu. Licha ya kucheza kwa miaka 20, yaani tangu Tanzania ikiongozwa na Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, akapita Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Hayati Dk John Pombe Magufuli hadi sasa nchi iko chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, wao bado wanakomaa na gemu.

Wengi wao wanasema kujitunza, nidhamu ya mchezo na mazoezi ndivyo vimewafanya kudumu kwa muda mrefu na bado wapo kwenye ubora uwanjani.


JUMA KASEJA

Kwa mara ya mwisho kipa huyu kuitwa kwenye mechi za kimashindano za timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ilikuwa fainali za CHAN zilizofanyika nchini Cameroon 2021 ukiachana na mechi za kirafiki za timu hiyo ambapo alikuwa anapigania namba na damu changa kwenye kikosi hicho.

Wakati anaitwa kwa mara ya mwisho, Stars ilikuwa chini ya kocha Ettiene Ndayiragije ambaye sasa anaifundisha Geita Gold na baada ya kutua Kim Poulsen hajaitwa tena.

Kaseja ni miongoni mwa makipa tegemeo kwenye kikosi cha KMC inayocheza Ligi Kuu Bara.

Kipa huyo amecheza Ligi Kuu kwa miaka 21 akiwa kwenye ubora na kupata namba kikosi cha kwanza kwenye timu nyingi alizocheza tangu mwaka 2000 alipokuwa Moro United hadi 2003 alipojiunga Simba ambako alicheza kwa mafanikio hadi 2014.

Alijiunga Yanga msimu mmoja, ingawa aliingia kwenye mvutano na uongozi na mwaka 2015 alijiunga Mbeya City kisha akatimkia Kagera Sugar 2017 na msimu wa 2018/2019 alihamia KMC hadi sasa.

Kaseja aliwahi kusema yeye ni muumini wa mazoezi, ambayo mbali na mazoezi ya timu, hupenda kujifua peke yake kwenye muda wa ziada ili kujiweka fiti zaidi na hiyo imezidi kumjenga na kubaki kwenye kiwango bora kwa muda mrefu.


FRANCIS MIYEYUSHO

Anawatoa jasho vijana ulingoni, pambano lake la kwanza la ndondi za kulipwa alicheza Februari Mosi, 1998 na kumchapa kwa pointi Issa Athuman. Hadi sasa Miyeyusho anakamata nafasi ya 16 kwenye ubora wa mab ondia wa kila uzani (pound for pound) akiwapiku wengine 408 nchini.

Amecheza mapambano 68 na kushinda mara 44 ni wa 240 kati mabondia 1,753 duniani na namba mbili kati ya mabondia 51 wa uzani wake wa light nchini, hivi karibuni ametoka kuwachapa, Habibu Pengo na Deo Samwel, mabondia wenye mashabiki Manzese na Mabibo.


JACOB MARENGA

Ni point guard na shooting guard tegemeo kwenye kikosi cha JKT kilichotinga robo fainali ya Ligi ya Taifa ya mpira wa kikapu (NBL) msimu huu.

Marenga ‘Bobonator’ alipachikwa jina la Terminator kutokana na uwezo wake uwanjani. Tangu 1998 alipojiunga na klabu ya Jogoo, nyota huyo ameendelea kutamba na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo ya Vijana, Shearing na Falcon za Uganda, Ukonga Kings, Oilers na sasa yuko JKT.

“Nitakuwa na JKT kwa muda mrefu kidogo kutokana na makubaliano baina yetu, niko kwenye kiwango bora kutokana na kujitunza, hakuna kingine,” anasema.


ALLAN KAMOTE

Ni bondia namba 231 kati ya 1,268 duniani na wa tatu kati ya mabondia 46 nchini kwenye uzani wake, Kamote aliingia kwenye ngumi mwaka 1998 na bado anaendelea kuwakimbiza vijana.

Hivi karibuni mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) umemtaja bondia huyo kuwa namba 19 kwenye ubora wa mabondia wa kila uzani nchini akiwapiku wengine 405.


PASCAL NDOMBA

Pambano lake la kwanza la Juni 22,2000 alichapwa na George Sabuni kwa pointi, lakini hiyo haikumkatisha tamaa. Ndomba bondia wa uzani wa cruiser ameendelea kukomaa kwenye gemu ingawa Juni 5, 2021 alichapwa na Rolly Lambert Fogoum huko Hilton Al Habtoor City, Dubai, kabla ya pambano hilo alitwaa ubingwa wa Afrika wa World Boxing Organisation alipomchapa Kaminja Ramadhan kwa KO, Januari 31, 2020.


ABDALLLAH RAMADHAN ‘DULLAH ZUNGU’

Nyota wa kikapu nchini, Dullah Zungu hivi sasa ana umri wa miaka 47 na bado anakiwasha ile mbaya. Amesema atastaafu akiwa na miaka 50. Aliisaidia Pazi kutinga nusu fainali ya Ligi ya taifa ya mpira wa kikapu (NBL) msimu huu. Mkali huyu ambaye awali, aliondoka nchini mwaka 2001 kwenda kucheza kikapu nchini Shelisheli, amepitia kwenye timu mbalimbali za ndani kama Rangers na Stone Town za Zanzibar na nje ya nchi na bado anaendelea kutamba na Pazi.

Kabla ya Hasheem Thabeet, Dullah ndiye mcheza kikapu aliyekuwa maarufu zaidi.


FABIANO JOSEPH

Amewahi kuwa bingwa wa dunia wa mbio za nusu marathoni za 2005 nchini Canada, hakuishia hapo, aliwahi pia kutwaa medali mbili za fedha kwa nyakati tofauti kwenye mashindano hayo. Mwanariadha huyo wa mbio ndefu ambaye alichukuliwa na jeshi la Wananchi (JWTZ) bado ameendelea kukomaa akichuana na vijana kusaka medali.

Fabiano ambaye safari yake ya riadha ilianzia kwenye mbio za Desemba 31, 2001 za Babati Half Marathon, alipokimbia kwa saa 1:04:44 bado ni tegemeo kwenye timu ya riadha ya jeshi na alikuwa kwenye kikosi kilichoshiriki mashindano ya majeshi mwaka huu.