Hawa hapa waheshimiwa wasanii Tanzania

Saturday June 05 2021
waheshimiwaaa pic
By Nasra Abdallah

KOTE duniani msanii ama mwanamichezo anapoingia katika siasa huwa na mvuto wa kipekee.

Staa wa filamu za Hollywood, Marekani, Arnold Schwarzenegger amekuwa gavana wa jimbo la California, mwanasoka George Weah ni Rais wa nchi ya Liberia na mwanamuziki Bobi Wine anaongoza chama cha upinzani Uganda na alishawahi kugombea urais.

Na kwa Tanzania hawa ni waheshimiwa wasanii.


Sugu

Joseph Mbilinyi ‘Sugu’. Huyu alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa miaka kumi kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, na kisha akachaguliwa tena mwaka 2015 na kukaa hadi 2020.

Advertisement

Huyu ndiye Mbunge katika uchaguzi wa mwaka 2015 aliongoza kwa kuwa na kura nyingi kuliko wabunge wote nchini.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilionyesha orodha ya wabunge waliochaguliwa na idadi ya kura zao, kati ya 10 walioongoza, saba walitoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), huku Sugu akishika namba moja kwa kupigiwa kura zaidi ya 100,000 kati ya 166,256 zilizopigwa na watu wa jimboni kwake.

Enzi zake kwenye muziki Sugu alitesa na nyimbo kama Wananiita Sugu, Nipo Mikononi mwa Polisi, Moto Chini, Sema Nao na nyingine nyingi.


Profesa Jay

Ni kama alivutiwa na besti wake Sugu kuingia kwenye siasa, naye mwaka 2015 akijitosa kugombea Jimbo la Mikumi kupitia Chadema chama ambacho pia ndio Sugu yupo.

Tofauti na Sugu, Profesa Jay yeye alikaa kipindi kimoja yaani 2025 hadi 2020 na kujipachika jina la Mbunge wa Binadamu na Wanyama, kutokana na Mikumi kuwa na moja ya mbuga kubwa za wanyama nchini.

Badaa ya kuukosa ubunge, hivi sasa ameamua kurudi zake rasmi kwenye muziki na kushusha madude ya nguvu, kwani wakati wimbo wa Baba alioshirikishwa na msanii Stamina ukiwa haujapoa, kaachia wimbo mwingine wa ‘Utaniambia Nini’ na kuonekana kukimbiza haswa.

Kipindi anawika kwenye soko la muziki, nyimbo kama Nikusaidieje, Zali la Mentali, Hapo Vipi, Bongo Dar es Salaam na Ndio Mzee zilikimbiza kwelikweli.


MwanaFA

Huyu ni mkali wa vibao kama Mabinti, Unanitega, Nangoja Ageuke, Wee Endelea Tu na Asanteni kwa Kuja.

Kuwepo kwa zaidi ya miaka 15 kwenye muziki na maisha ya kujiheshimu aliyokuwa akiishi amejikuta akipenya hadi kuwa mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Muheza baada ya uchaguzi wa mwaka 2020. Mbunge huyu kupitia chama tawala CCM, hivi sasa, anafanya yake Bungeni Dodoma akiwapambania wananchi wa Muheza na wasanii wenzake.


Mkubwa FelLa

Jina lake halisi ni Said Fella. Huyu alikuwa meneja wa awali wa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva na pia mwaka 2008 aliwahi kuimba baadhi ya nyimbo ukiwemo Simuachi, Chakachua na Najutia.

Hivi sasa Fella ni Diwani wa Kata ya Kilungule iliyopo Jimbo la Mbagala, hii ikiwa ni kipindi cha pili anaongoza Kata hiyo kwani alianza 2015 hadi 2020 na uchaguzi ulipoitishwa tena Oktoba 2020 alitetea kiti chake hicho.

Hakuna mdau wa muziki wa Bongofleva asiyejua mchango wa Fella katika muziki huo, kwani ndiye alikuwa akisimamia kundi la muziki la TMK wanaume lililokuwa na wasanii kama Juma Nature, Chege, Mh Temba na wengine wengi.

Pia ndio alianzisha kundi la Yamoto, lililoibua vipaji vya wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa akiwemo Aslay, Mbosso, Beka Flovour na Enock Bella.

Ukiachilia kuendelea kituo cha kukuza vipaji cha Mkubwa na Wanae, ambacho pia ndio kimewatoa wasanii kama kina Mabantu, Dulla Makabila na Young Lunya wanaofanya vizuri kwa sasa , hivi sasa Fella ni mmoja wa mameneja wa msanii Diamond Platnumz akisaidiana na kina Salam SK na Babu Tale.


Keisha

Unakumbuka vibao kama Uvumilivu, Nalia, Nimechoka ambao ulivyotingisha navyo msanii Keisha?

Basi tangu wakati huo jina lake limekuwa kwenye ramani na sasa ni mmoja wa wabunge wa viti maalum kupitia CCM.

Kabla ya hapo, Keisha ambaye jina lake halisi ni Khadija Shabani mwaka 2018 aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC). Keisha alikuwa mmoja wa wasanii wa kike pekee katika lebo ya Tip Top Connection iliyokuwa imesheheni wasanii wakali kama Madee, Tundaman, Mb Dogg, Cassim Mganga, Z-Anto, Pingu na Desso.


Babu Tale

Unapomtaja Diamond Platnumz, huwezi kuacha kumtaja Babu Tale kwani huyu ni mmoja wa mameneja walio na nguvu pale lebo ya Wasafi ambapo kazi hiyo ya umeneja aliianzia pale Tip Top Connection.

Wakati Meneja Sallam SK yeye akionekana zaidi kudili na soko la nje, Tale yeye amejikita zaidi hapa nchini na amekuwa akionekana mbele katika shoo mbalimbali za msanii huyo.

Tetesi za kugombea kwake ubunge zilianza pale Mkoani Kigoma kwenye tamasha la kuadhimisha miaka kumi ya Diamond Platnumz kuwa kwenye muziki.

Tale ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini.


Baba Levo

Jina lake halisi ni Clayton Chipando. Kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, alikuwa Diwani wa Kata ya Mwanga, mkoani Kigoma kupitia chama cha ACT Wazalendo, mwaka 2020 katika uchaguzi wa bahati haikuwa yake, na hivyo sasa kaamua kurudi kwenye muziki. Nyimbo alizorudi nazo ni pamoja na Yes No na ule wa High and Low. Pia ni mtangazaji pale Wasafi Media.

Advertisement