First 11 ya Warundi Ligi Kuu

Wednesday July 21 2021
burundi pic
By Ramadhan Elias

LIGI Kuu Bara 2020/21 imemalizika rasmi wikiendi iliyopita. Kila timu imevuna ilichopanda. Wapo waliofurahi na wengine wameumizwa na matokeo waliyoyapata hadi mwisho wa msimu.

Simba ndio mabingwa wa ligi hiyo wakitwaa

ubingwa kwa mara ya nne mfululizo, huku Yanga, Azam na Biashara United wamepata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) baada ya kuwa timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Wakati Ligi Kuu inaanza kila timu ilifanya usajili kutoka maeneo tofauti ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kuimarisha vikosi ili viwe na ushindani ikiwa ni pamoja na kupata matokeo mazuri.

Msimu uliomalizika wachezaji kutoka Burundi ndio walionekana kuwa wengi kwenye ligi hiyo ukilinganisha na nchi zingine kama Zimbabwe, Zambia, Uganda na Rwanda.

Makala haya yanakuletea kikosi cha wachezaji 11 kutoka Burundi waliocheza ligi msimu uliomalizika.

Advertisement


NAHIMANA - NAMUNGO

Jonathan Nahima ni kipa wa timu ya Taifa ya Burundi. Akiwa hapa nchini aliwahi kuichezea KMC kabla ya kuhamia Namungo FC.

Kwa kipindi alichokaa nchini amekuwa kipa namba moja kwenye timu zote alizocheza, huku akijizoelea mashabiki wengi kutokana na uwezo wake mkubwa anapokuwa langoni.


NDIKUMANA - KMC

Yusuph Ndikumana ni beki kitasa anayekipiga KMC alikosajiliwa msimu mmoja uliopita akitokea Mbao FC ambako pia alicheza kwa ubora.

Msimu huu haujawa bora kwake kutokana na majeraha, lakini bado ameliwakilisha vizuri taifa lake.


SAIDO - YANGA

Said Ntibazonkiza ni straika aliyesajiliwa wakati wa dirisha dogo akitokea Vital’O ya Burundi. Pamoja na kutocheza mara kwa mara lakini aliiwakilisha vyema nchi yake katika mechi alizobahatika kuzicheza, Vital’ O ya nchini kwao.

Saido tangu ajiunge na Yanga amekuwa na kuwango bora na pia amekuwa akitumika kama mchezaji kiongozi.


EMANUEL MVUYEKURE (KMC)

Kiungo huyu fundi anayekipiga kikosi cha KMC aliwahi kucheza Azam FC. Ameipeperusha vyema bendera ya taifa lake akiwa Tanzania.


NZIGAMASABO STIVE -NAMUNGO

Eneo la kiungo la Namungo FC mara nyingi limetawaliwa na fundi huyu raia wa Burundi.

Nzigamasabo ni mdogo wa kuzaliwa wa Saido. Alijiunga na Namungo mwaka juzi akitokea Bugesera FC ya Rwanda.


FISTON ABDULRAZACK (YANGA)

Wakati wa dirisha dogo msimu uliomalizika ndipo mwamba huyu alitua hapa nchini baada ya kuachana na ENPPI ya Misri.

Nusu msimu wa Fiston ndani ya Yanga umetosha kuitangaza nchi yake kwa Watanzania ingawa kiwango chake sio kile kilichotarajiwa na mashabiki wengi wa soka nchini.


MUSTAFA - COASTAL UNION

Francis Mustafa ni kiungo mshambuliaji aliyesajiliwa na Coastal Union kwenye dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Bugasera ya Rwanda.

Tangu amejiunga na Coastal Union amekuwa na kiwango cha kuridhisha ingawa timu hiyo haikuwa na matokeo mazuri kwenye mechi zake. Pia aliwahi kuzichezea Gor Mahia na Kiyovu Sports.


BLAISE - NAMUNGO

Miongoni mwa washambuliaji waliofanya vizuri Namungo msimu huu ni pamoja na Bigirimana Blaise.

Alijiunga na Namungo msimu uliopita akitokea Alliance ya Mwanza. Nyota huyu pia amewahi kukipiga Stand United aliyojiunga nayo akitokea Kiyovu Sports ya Rwanda.


JEAN DIDIER - MBEYA CITY

Katika dirisha dogo la usajili msimu huu Mbeya City ilizama nchini Burundi na kunasa saini ya mshambuliaji huyu.

Licha ya kwamba hajapata muda wa kutosha kucheza kwenye kikosi hicho, lakini uwepo wake Tanzania ni uwakilishi tosha kwa nchi yake.


ERICK KWIZERA - NAMUNGO

Namungo walinasa saini ya kiungo mshambuliaji huyu wakati wa usajili wa dirisha dogo na kuongeza idadi ya warundi nchini.

Kwizera aliwika na Namungo zaidi kwenye michuano ya Kombe la Mapindizi iliyofanyika Zanzibar msimu huu na Yanga kubeba ubingwa.


MOSI - KAGERA SUGAR

Moussa Hadji Mosi ni mshambuliaji aliyesajiliwa Kagera Sugar mwanzoni mwa msimu huu akitokea Les Lierres ya Burundi.

Licha ya kwamba Mosi hakupata muda wa kutosha kucheza kikosi cha Kagera lakini anatimiza idadi ya wachezaji 11 wa Burundi waliocheza Ligi Kuu Bara msimu uliopita.


KOCHA VIVIER BAHATI

Katika kikosi hiki, kocha mkuu atakuwa Vivier Bahati ambaye ni raia wa Burundi na anahudumu kwenye kikosi cha Azam kama kocha msaidizi.

Advertisement