Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu kufunga busta Angola, hii hapa sababu ya kujaza viungo

Muktasari:

  • Kocha Fadlu ameondoka na msafara wa wachezaji 22 kama ilivyokuwa katika pambano lililopita dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, lakini safari hii akimuacha beki Valentin Nouma na kuongeza kundini, winga Edwin Balua na akimchomoa Steven Mukwala ili nafasi yake izibwe na Valentine Mashaka.

KIKOSI cha Simba kimetua salama jijini Luanda, Angola kwa ajili ya kuwahi mchezo wa tano wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis utakaopigwa wikiendi hii, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akionyesha dalili za wazi za kutaka kufunga busta katika mchezo huo wa Jumapili.

Kocha Fadlu ameondoka na msafara wa wachezaji 22 kama ilivyokuwa katika pambano lililopita dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, lakini safari hii akimuacha beki Valentin Nouma na kuongeza kundini, winga Edwin Balua na akimchomoa Steven Mukwala ili nafasi yake izibwe na Valentine Mashaka.

Kuachwa kwa Nouma na Mukwala kulishtua baadhi ya mashabiki wa Simba, lakini uongozi wa klabu umeweka bayana hakuna sababu yoyote zaidi ya mpango wa kocha kubadilisha mziki wa kukabiliana na Bravos yenye hasira ya kupoteza mechi iliyopita ugenini kwa mabao 4-0 dhidi ya CS Constantine na pia kipigo cha 1-0 ilichopewa na Simba katika mchezo uliopita uliopigwa Kwa Mkapa Novemba mwaka jana.

Katika msafara huo wa Simba, Fadlu ameondoka na makipa Moussa Camara, Ally Mustafa na Hussein Abel, wakati mabeki ni Karaboue Chamou, Fondoh Che Malone, Abdulrazack Hamza, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shomari Kapombe na Kelvin Kijili, wakati washambuliaji ni Leonel Ateba na Valentino Mashaka.

Viungo 11 walioondoka na kocha huyo raia wa Afrika Kusini ni; Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Yusuf Kagoma, Ellie Mpanzu, Augustine Okejepha, Kibu Denis, Debora Mavambo, Ladack Chasambi, Jean Charles Ahoua, Awesu Awesu na Edwin Balua aliyejumuishwa safari hii kuiongezea Simba nguvu zaidi eneo la mbele.


KWANINI VIUNGO ZAIDI

Kitendo cha kocha Fadlu kuondoka na nusu ya wachezaji wakiwa viungo, kumefanya kuibuka mjadala katika mitandao ya kijamii, lakini hapa chini ni uchambuzi wa kitu gani kimechangia kocha huyo kubeba nyota hao 11, wakiwa sawa na idadi ya wachezaji wa nafasi nyingine kikosini.

Katika mechi ya Jumapili itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa wa Novemba 11, Simba inahitahaji kushinda au kupata sare ili kufuzu robo fainali kutoka Kundi A la michuano hiyo kabla ya kurejea nyumbani kumalizana na vinara wa kundi hili, CS Constantine ya Algeria.

Constantine na Simba zinatofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, lakini zote zinalingana zikiwa na pointi tisa baada ya mechi nne, huku Bravos ikiwa na alama sita ikishika nafasi ya tatu na CS Sfaxien ya Tunisia ikiburuza mkia bila pointi yoyote hadi sasa.

Katika kuhakikisha sare inapatikana timu nyingi zimekuwa zikitumia njia mbili, aidha kukubali timu pinzani iwashambulie na wao kumeza mashambulizi hayo kwa kuzuia muda wote, japo huwa inakuwa ngumu ikiwa timu A itakutana na timu B yenye wachezaji wa daraja la juu.

Mabeki wengi huwa wanakuwa na hatari ya kufanya makosa ikiwa watapewa presha kubwa, ingawa baadhi ya timu hufanikiwa zaidi katika aina hiyo ya uzuiaji.

Aina ya pili ambayo timu nyingi zimekuwa zikiitumia ni kuwa na umiliki wa mpira kwa asilimia nyingi ili kutowapa timu pinzani nafasi ya kubwa ya kuandaa mashambulizi.

Timu nyingi duniani zimekuwa zikitumia mfumo huu hususani Manchester City na Barcelona za Pep Guardiola.

Eneo la pili la kumiliki mpira kwa muda mrefu mbali ya kuwanyima timu pinzani nafasi kubwa ya kufanya mashambulizi, pia ni kujaribu kuchosha akili zao kwa kuwafanya wakabe muda mwingi wa mchezo hali inayosababisha ufikirivu na utumiaji wa nguvu kwa kiasi kikubwa.

Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hiyo, uliopigwa Dar es Salaam, Bravos ilionyesha ni hatari inapokuwa na mpira, pia ikibebwa zaidi na uwezo wa viungo wenye uwezo wa kuliteka eneo hilo, kiasi wenyeji Simba ilitaabika licha ya kuwa na viungo bora na kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 la penalti.

Huenda Fadlu alishaisoma vya kutosha Bravos tofauti na ilivyocheza mechi ya kwanza nyumbani hasa kwa kiungo Antonio Dipoco Teodor ‘Edmilson’ aliyefanya kazi nzuri eneo la kati akiwa ndio mhimili wa timu hiyo katika kumiliki mpira, huku Messias Neves akiwa anakata umeme.

Mbali na viungo hao wawili, lakini Bravos ilisaidiwa pia Francisco Marta aliyekuwa anacheza juu yao ambapo walifanikiwa kuibana vizuri safu ya kiungo ya Simba ambayo kwa kiasi kikubwa mhimili alikuwa ni Fabrice Ngoma aliyecheza kama namba nane.

Neves alikata mirija yote ya Ngoma kisha Marta na Edmilson wakikaa na mpira muda mwingi kisha kupiga pasi za mbele kwa ajili ya kupandisha mashambulizi na hili limemuamsha Fadlu na kuamua kubeba silaha zote ili kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri ugenini na kukata tiketi ya robo fainali mapema ikiwa ugenini.

JINSI YA KUIFUNGA BRAVOS

Moja kati ya maeneo ambayo katika mechi ya kwanza Bravos ilifanikiwa sana mbele ya Simba ilikuwa ni kwenye eneo lao la kiungo ambapo kwa kiasi kikubwa walijua mchezaji hatari ni Ngoma, hivyo baada ya kuzia mirija inayomzunguka kwa pande zote, Simba ilielemewa sana katikati.

Hata hivy,o mara kadhaa ambazo Simba ilishambulia kupitia pembeni bado haikufanikiwa kuifungua Bravos kiasi cha kuwawezesha kupata bao.

Katika mchezo huu moja ya maeneo ambayo inaweza kuyatumia kwa ajili ya kuhakikisha Bravos inafunguka aidha katikati ama pembeni ni kupitia viungo.

Kimsingi Bravos imeonekana kutumia mifumo ya aina mbili, wa kwanza ni 4-2-3-1 ambao mara nyingi huutumia wanapokuwa ugenini na wanapokuwa nyumbani huwa na 4-3-3.

Ukiacha  4-2-3-1 ambao asili yake ni 4-4-2 na wamekuwa wakiutumia zaidi ugenini, katika mfumo wa 4-3-3 wanaopendelea kuutumia nyumbani moja ya sifa kubwa ni katika umbo la kujilinda.

Mfumo huu huiruhusu timu pinzani inapokuwa haina mpira kuwa na wachezaji watano katika eneo la katikati ya kiwanja ambapo mawinga huwa wanashuka chini kuungana na viungo watatu.

Hii husababisha iwe ngumu sana kuifungua kupitia katikati kwa timu ambayo ina idadi ndogo ya viungo.

Hivyo, huenda Fadlu anahitaji kuanza na viungo wengi kwenye mchezo huu ili kuhakikisha anavunja na kuifungua safu ya kiungo ya Bravos.


UKUTA CHUJIO

Jamba zuri kwa Simba ni kwamba ukuta wa Bravos unavuja kama chujio. Hamna mechi ya Kundi A iliyocheza msimu huu bila ya kuruhussu bao.

Ukiacha kupigwa 4-0 na CS Constantine na kulala 1-0 dhidi ya Simba, Bravos imeruhusu mabao mawili mawili hata katika mechi ambazo ilishinda nyumbani 3-2 dhidi ya CS Constantine na 3-2 dhidi ya CS Sfaxien. Kiujumla katika mechi nne, Bravos imeruhusu mabao tisa ikifunga sita, wakati Simba imeruhusu mabao matatu tu ikifunga matano. 


SIMBA WENYEWE

Kocha Fadlu alipozungumza na Mwanaspoti akiwa Angola, alifafanua sababu ya kusepa na viungo wengi kuliko wachezaji wa maeneo mengine.


“Nimesafiri na viungo wengi sio kwa sababu ninakwenda kujilinda, lakini ni kutokana na utayari wao kuelekea mchezo husika dhidi ya Bravos,” Fadlu alijibu kwa ufupi, wakati Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally alisema wachezaji walioachwa nyumbani, hasa Mukwala na Nouma hawana tatizo lolote isipokuwa ni uamuzi wa kocha kufanya mabadiliko ya kikosi tofauti na mechi zilizopita.

Simba katika mechi nne zilizopita ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos, kisha ikaenda kulala ugenini kwa mabao 2-1 mbele ya Constantune na kuifunga nje ndani Sfaxien ikiinyoa 2-1 na 1-0 mtawalia. Baada ya Angola, Simba itarudi nyumbani kuipokea Constantine.