EXCLUSIVE: Garincha huyo Mo Dewji ni mtu sana, kiboko ya Yanga

KAMA kuna somo ambalo amehitimu vizuri, staa wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garincha’ basi ni nidhamu ya kujua namna ya kuishi na mashabiki. Staa huyo anasema mashabiki ni mtaji baada ya kustafu soka na anawasisitiza mastaa wa sasa kupunguza majivuno.

Garincha anawaambia mastaa wa sasa kwamba mashabiki ni mtaji wao wa baadaye kuliko pesa wanazozipata, .

“Nilikuwa na nidhamu, kuna ofisi za wakubwa wananisaidia bila shida kutokana na hilo, kama mastaa wetu hawa wasiponielewa maisha yatawaelewesha,”anasema.

Jambo la muhimu zaidi, anawashauri wazawa kama wamecheza Yanga basi wasihamie Simba, uzoefu wake anaona kuna imani inayoondoka kwa mashabiki wao.

“Hayo yote ninayaona sasa, kuna watu wa Yanga wananisaidia wanasema sikuwa mnafiki, ila kwa wageni wahame tu maana wakimaliza wanarudi makwao, Simba na Yanga zinaishi mioyoni mwa watu.”

Mapunda anafunguka mengi, ikiwemo namna ambavyo kigogo wa Simba alivyomuonyesha maisha mapema anayoyafurahia kwa sasa, wakati baadhi ya mastaa wengine aliocheza nao wanapitia maisha magumu tofauti na ukubwa wa majina yao.


WACHEZAJI WAONGOZE SOKA

Hivi sasa wachezaji wengi wa zamani kuanzia miaka ya 2000 wameingia kwa kasi kusomea ukocha, jambo ambalo Mapunda anasema ni zuri huku akiwataka wengine kusomea mambo ya utawala wa mpira.

“Nafurahi kuwaona wanajitokeza kusomea ukocha, ingawa nilishindwa kwa sababu nina shughuli zangu za kufanya.

“Ujue wachezaji waliocheza kwa kiwango kikubwa hawapendi kuwa makocha, inawezekana wana shughuli zao, pia wanaelewa mpira ulivyo kwani wamepita mikononi mwa makocha wengi na wameonea jinsi wanavyopata shida, hivyo wanaona bora wafanye tu mambo mengine.

“Mtu ambaye hakucheza sana mpira ndio anakuwa na morali ya kuwa kocha na ndio maana angalia makocha wengi duniani ni hawakucheza sana mpira.

“Kazi ya ukocha sio ngumu kwa mimi ambaye nimecheza mpira kwa sababu tunaongea lugha moja na wachezaji, mtu ambaye amecheza mpira ana uwezo wa kujua tabia na matatizo ya wachezaji, lakini mtu ambaye hajacheza hawezi kuzijua changamoto zao, ndio maana ni vizuri viongozi wawe wenye uelewa na soka.”

Anasema sio kama hataki kusomea utawala au ukocha ila shughuli za kimaisha zimembana.

“Nina kampuni yangu ya ukandarasi wa barabara ambayo tunashea na mdogo wangu, iko Dar es Salaam. Wakati nacheza nilijipanga maisha baada ya soka, ikiwemo kujenga shule ya michezo tayari nimenunua eka 50 Songea ingawa bado sijaanza kujenga ila muda ukifika nitatimiza malengo ya kujenga kituo cha michezo,” anasema. Mapunda anadai shule hiyo itakuwa na nyumba za kulala wachezaji, viwanja vya wakubwa na wadogo, madarasa ya kufundishia soka na anataka iwe ya kisasa zaidi.


HAISAHAU MAJIMAJI

Mapunda anasema katika maisha yake ya soka hataisahau timu ya Majimaji ya Songeza kwani ndio imemlea tangu akiwa mdogo.

“Wakati huo kina Madaraka Selemani walikuwa wanaitumikia, nilikuwa mdogo, nilikuwa naokota mipira, baada ya mazoezi ama mechi nilikuwa nabakia nayo naanza kuichezea nje. Pia na kuitumikia timu za shule.

“Kulikuwa na Mzungu anaitwa Dimitar Samsarov ndiye aliyekuwa kocha wa Majimaji na alikuwa akinipenda sana kutokana na kipaji changu, alikwenda nyumbani kuwaambia wazazi wangu anataka kunipeleka Ulaya ili akaniendeleze kipaji changu, baba alikataa.

“Baada ya kuona amekataliwa na baba yangu, akawaambia viongozi wa Majimaji wanitunze nitawasaidia baadaye. Wakati huo nilikuwa nasoma shule ya msingi na nilikuwa sielewi chochote nachukulia poa tu hilo jambo la kupelekwa Ulaya.”

Mwaka 1997 alisajiliwa timu ya wakubwa na mwaka uliofuata Majimaji wakachukua ubingwa Ligi Kuu Bara, ndipo alipoonekana na viongozi wa Simba na Yanga.


USAJILI WAKE SIMBA

Wakati nikiwa Majimaji niliitwa Timu ya Taifa mwaka 1999 na tulikua tunaweka kambi pale Jeshi la Wokovu (Salvation Army) Kurasini alikuja Mohammed Dewji ‘MO’ na Azim Dewji na ndipo MO alipomwambia anataka akacheze Simba.

“Baada ya muda MO akatuma watu Songea na wakati huo Yanga nao walishafika zaidi ya mara mbili wakiongozwa na Francis Kifukwe lakini sikwenda Yanga kwani niliipenda Simba.

“MO alinipa vitu vingi sana wakati ananisajili, nje na pesa alinipa mashine za kusaga na wakati huo zilikuwa zinauzwa milioni tano, kuna vingine siwezi kuvitaja lakini ukivikusanya vitu vyote nilivyopewa jumla ilifika 10 milioni kwa wakati huo zilikuwa pesa nyingi sana.”

Anasema hadi sasa wana mawasiliano na MO ambapo wanashauriana mambo ya kibiashara na maisha.

“Tangu zamani MO alijua akili kubwa ya kimaisha ambayo nilikuwa nayo, alinishauri vitu vingi vya msingi na kunisisitiza umarufu bila kitu unitesa baadaye, hivyo alitaka niwekeze maisha baada ya soka nitafanya kitu gani,” anasema.


MIKOA IAMKE

“Ebu fikiria wakati ule Majimaji ndio tulikuwa mabingwa wa nchi je Simba na Yanga hawakuwepo? Timu za mikoani zilikuwa bora sana tofauti na sasa Simba na Yanga ndio bora,” anasema Mapunda akiitaka mikoa kuamka ili kutengeneza timu bora zitakazoleta ushindani kwenye ligi.

“Kwa sasa Simba na Yanga ndio kioo cha Timu ya Taifa na kama zinafanya vibaya ujue hakuna Taifa Stars kwa sababu wachezaji wazuri wote wanawachukua wao na timu nyingine wachezaji wanapambana wasajiliwe na timu hizo.

“Lakini wakati ule Simba na Yanga zikienda kumchukua mchezaji mikoani anakataa anasema anabaki kwenye timu yake kwa sababu timu nyingi za mikoani zilikua bora na wachezaji walikuwa wanapata kila kitu.

“Mashirika yameua sana timu, hebu ona Pamba iko wapi? Timu za mashirika nyingi zimekufa. Mfano Majimaji ilikuwa timu inayohudumiwa na mkoa ndio manaa ilifanya vizuri lakini kwa sasa mikoa mingi haizihudumii timu na kufanya ligi kukosa ushindani.”

Mapunda anashangaa kwa nini mikoa au halmashauri zinashindwa kuzihudumia timu kama ilivyo kwa Mbeya City.

“Serikali yetu ni sikivu, kwani haijui kama Mbeya City inahudumiwa na halmashauri na hata kwenye ilani ya CCM inasema michezo lazima iwepo kila mkoa kwa nini mikoa mingine inashindwa kufanya vile kama inavyofanya Mbeya City, wanakwama wapi?

“Sisi Songea kulikuwa na mfuko wa maendeleao ya mkoa, ule mfuko halmashauri zote zilichangia na ulikuwa unatumika kwenye maendeleo yote ya mkoa kama kujenga shule, hospitali na hata kuihudumia Majimaji na ndio maana ilikuwa inafanya vizuri,

“Hiyo ishu ya mkoa kuihudumia timu aliianzisha Gama na baadaye Anna Makinda akaja kuiendeleza hadi timu ikachukua ubingwa, yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa mkoa ila alipoondoka tu waliofuatia wakaufuta huo mfuko”.


UTAIFA KWANZA

Mapunda anasema Simba na Yanga ndio timu kubwa nchini lakini zinasababisha anguko la Taifa Stars.

“Kwa sasa kuna timu unaweza kuiangalia ukasema pale kuna mchezaji mmoja au wawili wa kuitwa Taifa Stars, tofauti na wakati ule tunacheza unakuta timu kama Majimaji inatoa wachezaji hata watano Stars.

“Angalia leo Yanga na Simba wana wachezaji wangapi wa kigeni, je, wanaachwa nje?, Ni lazima wacheze kwa sababu wamewalipia pesa nyingi za usajili. Hivyo mtu uliyemlipia pesa nyingi anakaaje benchi, haya wazawa je wanacheza wangapi.

“Hizo ndio timu tunazitegemea labda ziwe na wachezaji wengi wa Stars, lakini wazawa hawapati nafasi halafu leo unataka timu ya Stars ifanye vizuri Afcon hao wachezaji huo uzoefu wanaupata wapi?

Mapunda licha ya kucheza soka na kupata mafanikio makubwa lakini hataki kabisa mtoto wake wa kiume acheze huku akimtaka asome kwanza.

“Nina mtoto wangu mmoja anajua sana mpira lakini sitaki acheze nataka asome kwanza ndio kwanza yuko kidato cha tatu,” anasema na kuongeza;

“Elimu ndio itambeba baadaye, asome kwanza halafu atacheza labda huko siku zijazo.

“Naona jinsi watangulizi wangu ambao walikuwa wachezaji mastaa lakini hali zao za maisha kwa sasa ni tofauti na majina yao, ni kitu ambacho nakichukia sana ndio maana namkazania mwanangu asome na pia hata wachezaji wa sasa wanatakiwa kuamka na kusoma kwani mpira sio mchezo wa muda mrefu, ukicheza sana ni miaka 12, “anasema Mapunda.


KIBOKO YA YANGA

“Tangu nikiwa Majimaji kama kuna timu nimeifunga sana ni Yanga ingawa siwezi kukumbuka yalikuwa mabao mangapi hapo nitakuwa naongopa, nilipojiunga na Simba pia niliifunga sana, walionishuhudia wakati nacheza ni mashahidi wa hilo,” anasema.


KIKOSI CHAKE

Kipa ni Mohamed Mwameja, Said Swedi, Ramazan Wasso, Boniface Pawasa, Christopher Alex (marehemu), Seleman Matola, Steven Mapunda ‘Garincha’, Shekhan Rashid, Nteze John, Yusuf Macho ‘Musso’, Athuman Machupa huku kocha akiwa ni James Siang’a (marehemu).