Dalali: Wanachama walijaza nyumba yangu kinyesi

Tuesday September 14 2021
dalali pic
By Olipa Assa
By Charity James

JANA tulianza kuchapisha makala iliyotokana na mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali aliyeeleza mambo mengi ikiwamo chimbuko la Simba Day, Uwanja wa Mo Simba Arena na hata alivyoingia madarakani pamoja na ukomandoo aliokuwa nao Msimbazi. Hata hiyo, leo Dalali anaendelea kuzungumzia mambo mbalimbali katika klabu hiyo ukiwamo ukomandoo na jinsi alivyojitosa kuwania uongozi na maisha yake kwa ujumla Msimbazi na alivyo sasa. Lakini kubwa anasimulia mkasa uliofanywa na baadhi ya wanachama waliokuwa hawamtaki waliomvamia nyumbani kwake na kuipaka nyumba yake kinyesi. Kivipi? Endelea...!


KUJITOSA SIMBA
Ukiachana na ukomandoo Dalali alikuwa mwenyekiti wa matawi ya Simba Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka 20, ambapo aliutumia kujifunza mengi hasa kiu ya wanachama kuhusu timu yao.
“Niligombea mara nane kwenye nafasi tofauti sikubahatika kuwa kiongozi hadi ilipofika 2006 ambapo nikawa mwenyekiti nikiingia na kina Omar Gumbo (makamu mwenyekiti), Mwina Kaduguda (katibu mkuu), msaidizi wake akiwa Mohammed Mjengwa, mhazini akiwa Ally Hassan na msaidizi wake, Chano Almasi na katibu mwenezi akiwa ni Said ‘Seydou’ Rubeya hadi nilipostaafu kwa kumpisha Rage uchaguzi wa Mei 9, 2010,” anasema.


CHANGAMOTO ZA KAZI
Anasema 2008 ni mwaka ambao hatausahau katika maisha yake. Anasimulia tukio baya alilofanyiwa na mashabiki baada ya kufungwa na Azam FC mabao 2-0 wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
“Zilikuja Costa tatu (gari) zilizojaza mashabiki ambao walikuja kunifanyia vurugu nyumbani, ila kuna mtu alinipenyezea taarifa. Basi wakashuka kwenye gari wakaanza kupiga mawe nyumba. Nikaificha familia yangu. Baadaye nikatoka ndani kwenda kuzungumza nao,” anasema Dalali.
“Nikawauliza mnataka nini? Wakanijibu ujiuzulu kwa sababu umefungwa na Azam FC. Nikawaambia zimebakia mechi nyingi na tupo nafasi ya pili, wakasema hatukutaki. Nikawajibu sijiuzulu haya mnataka nini kingine, wakajibu kujisaidia ndani kwako. Nikawafungulia milango.”
Baada ya kuwajibu hivyo, Dalali anasema: “Waliingia walijisaidia kila sehemu, nadhani watakuwa walipita Kariakoo kula mapera kwanza. Nikawaambia mmemaliza nendeni mkajisafishe uani kuna jaba la maji, wakajisafisha wengine walienda mbali kujisaidia sehemu ambapo naswalia.”
Anasema baada ya kufanya tukio hilo wakaondoka na siku ya pili akaenda makao makuu ya klabu akawakuta mashabiki akawaambia amejiuzulu.
“Kuna waziri aliona tukio hilo akanipigia simu nirudi kazini, akanisaidia kuwapeleka mashabiki polisi. Baada ya kuwabana wakamtaja kiongozi mwenzangu aliyewakodisha aliwapa laki tatu (300,000) wakaniomba msamaha nikawasamehe,” anasema.
Dalali anasema baada ya wiki mbili alirejea tena klabuni na kufuta kauli ya kuachana na uongozi kwa madai kuwa alitamka maneno mdomoni bila maandishi. Wakampokea na kumshangilia huku wakimuunga mkono hadi alipostaafu 2010.
“Wale ambao walijisaidia sehemu ambayo nilikuwa naswalia walikufa kama sita. Baadhi wakaja wakaniomba msamaha niliwaambia wamuombe Mwenyezi Mungu. Hayo ni baadhi ya matukio niliyokutana nayo wakati wa uongozi wangu.”

USAFI BAADA YA MKASA
Anaulizwa nani alifanya usafi baada ya mashabiki hao kuchafua nyumba yake? Dalali kwa sauti ya kinyonge anasema: “Nilimuomba mke wangu anisamehe, anivumilie na akubaliane na kazi yangu. Alifanya usafi ingawa familia ilinikataza nisiendelee kufanya kazi hiyo, ila haikuwezekana kwa vile soka limekuwa sehemu ya maisha yangu na hasa klabu ya Simba tangu nikiwa kijana,” anasema.
Mbali na hilo anasema anakumbuka mwaka huohuo hawakuweza kuchukua ubingwa, kisa ilikuwa ni beki Juma Nyosso.
“Simba ilimsajili Nyoso kutoka Ashanti United kupitia dirisha dogo, lakini alikuwa na kadi nyekundu. Bahati mbaya akacheza mechi ya mwisho tukapata pointi za ubingwa. Coastal Union wakakata rufaa tukanyang’anywa pointi tukaishia nafasi ya pili.”

Advertisement

MASHABIKI WAKIMBIZA WADHAMINI
Dalali anasema 2006 alipata udhamini wa benki ya Afrika Kusini ambayo ilikubali kujenga ghorofa 25 kama kitegauchumi cha klabu.
“Kuna makubaliano tulifanya, lakini kuna wanachama walifanya vurugu hadi kumuumiza mzungu aliyekuja kuchora ramani, wakidhani nilitaka kuuza mali za klabu,” anasema.
“Ndani ya miaka 10 ghorofa tano (wabia) wangekuwa wanafanyia shughuli zao, 20 zetu na baada ya miaka hiyo tungekabidhiwa kabisa (jengo lote). Sasa hivi tungekuwa na vitega uchumi vingi tu.
“Wanachama wakaja wakampiga yule mzungu aliyekuja kupiga picha na video ili kupeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kupata ramani. Wakamgalagaza kwenye matope na hakurudi tena.
“Ni uelewa mdogo na jazba za wana Simba wa miaka ile. Kwanza lazima ningerudi kwao kuwaambia, kwani hata jengo la Kariakoo hatukuweza kupangisha watu bila kuwataarifu wanachama, sasa nitashangaa kwa nini walifanya yale na kuwakimbiza wadhamini wake.”


MATUKIO YA KUSISIMUA
Dalali anasema hakuna tukio lililobaki kichwani mwake kama lile la 1975 Simba ilipofungwa na Yanga kwa bao 1-0 katika fainali za Afrika Mashariki matokeo yaliomuumiza shabiki mmoja aliyemtaja kwa jina la Malenda ambaye aliamua kujiua.
“Fainali hizo zilipigwa Zanzibar, Malenda alikuwa anafanya kazi katika kiwanda cha nyuzi. Katika kiwanda hicho chini kulikuwa na mapipa ya maji ya moto ambayo yalikuwa yanachuja nyuzi, akajitumbukiza humo na kufa kifo kibaya sana,” anasema Dalali.
“Lilikuwa tukio la kuumiza sana ambalo liliacha simanzi nzito kwa wana Simba na familia kwa ujumla. Hata msiba wa mtoto wa miaka tisa Joshua aliyejinyonga juzi baada ya kufungwa na Yanga mzunguko wa pili ilinikumbusha tukio hilo la zamani.”
Tukio lingine analolikumbuka Dalali ni la Said Salim Bakhresa aliyekuwa anajitoa sana Simba, lakini kuna shabiki alimfanyia tukio la ajabu lililomfanya ajiweke kando.
“Sikumbuki mwaka sawasawa, lakini Bakhresa alileta timu ya nje kucheza na Simba, akaleta walinzi wa kazini kwake sasa kama unavyojua timu hizi kuna wazee ambao wanakaa langoni kupata chochote kitu,” anasema.
“Kuna mzee mmoja kwa sasa ni marehemu alikuwa anaitwa Mzee Lambalamba, wakati Bakhresa anaingia getini akamchomolea kisu.... Lilikuwa tukio kubwa, akachukizwa tangu hapo akajiweka pembeni.
“Wakati huo alikuwa amenunua vifaa vya kujenga hospitali ya timu. Kifupi alipanga kufanya mengi sana, akili ya mashabiki ndio hiyo.”


SOKA NA ELIMU
Dalali anasema baada ya kuwa mwenyekiti wa Simba alibadilisha katiba ya kiongozi wa kujitolea angalau awe na elimu ya kidato cha nne ambayo ndiyo inayotambulika Shirikisho la Soka nchini (TFF).
“Wakati nabadilisha katiba elimu yangu ilikuwa darasa la saba japokuwa baadaye nilikwenda kusoma hadi kidato cha nne na nikafaulu. Hiyo ndiyo ilileta changamoto kuniona kama nataka nirejee kwenye uongozi, jambo ambalo halikuwa kweli,” anasema Dalali.
“Ninachokiona kwenye klabu zetu hiyo ngazi ya digrii iwe ya waajiriwa kama mtendaji mkuu, msemaji na mhasibu, ila wa kujitolea kama mwenyekiti watumie katiba iliyopo TFF ambayo inatambua elimu ya kidato cha nne, kwani walio na elimu hiyo wanaujua vizuri mpira na pia hizo digrii watuambie wamesomea nini.”Usikose sehemu ya mwisho ya kesho mahojiano na Mzee Dalali

Advertisement