Dah wamepotea moja kwa moja

Wamepotea moja kwa moja

SOKA siku zote ni mchezo wa namba zinazopanda na kushuka na ili mchezaji aendelee kusalia katika timu anayocheza au kwenda sehemu nyingine, lakini kama namba zikiwa zinashuka moja kwa moja unaweza kupotea haraka.

Katika soka la Tanzania wapo wachezaji ambao walikuja kwa spidi, lakini baada ya hapo wamepotea na mpaka sasa hawajarejea tena kwenye ulimwengu wa soka la ushindani.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wachezaji ambao walitamba, lakini wakapotea ghafla na kuwaachia wadau wa soka maswali wakijiuliza wako wapi.


SAID BAHANUZI

Ni miongoni mwa washambuliaji waliotamba na Yanga kwa muda mfupi baada ya kung’ara kwenye michuano ya Kombe la Kagame 2012 na kuibuka kuwa mfungaji bora alikofunga mabao sita.

Baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo mashabiki wa Yanga walikuwa na imani naye kubwa, huku wengine wakitengeneza jezi zenye jina la mchezaji huyo. Hata hivyo, Bahanuzi alishindwa kuwika kwenye Ligi Kuu Bara na kuacha maswali kwa mashabiki kuwa ilikuwa ni nguvu ya soda tu au?

Jambo lililowakera zaidi mashabiki ni baada ya kukosa penalti 2014 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ambapo Yanga ilitolewa kwa penalti 4-3.

Yanga waliachana na Bahanuzi wakati huohuo na msimu wa 2014/15 akajiunga na klabu yake ya zamani - Mtibwa Sugar, lakini huko akashindwa kurejea katika ubora wake. Akiwa na Mtibwa alidumu hadi msimu wa 2015/16, lakini napo hakuwa katika kiwango na timu hiyo kuamua kuachana naye na hadi sasa hajulikani alipo.


AME ALLY ‘ZUNGU’

Alitamba na Mtibwa Sugar msimu wa 2014 jambo lililowafanya mabosi wa Azam wamsajili 2015 ili kwenda kuziba nafasi ya Didier Kavumbagu ambaye alikuwa na wakati mzuri akiwa na kikosi hicho. Baada ya kutua Azam, Zungu hakuwa katika kiwango bora sana, badala yake alitolewa kwa mkopo kwenda Simba 2016, lakini hakuonyesha kiwango hivyo Azam kuamua kumtema.

Msimu wa 2017/2018 aliibukia Ndanda FC na hapo ndipo alianza kushuka na kupotea kwenye ramani ya soka kutokana na kukaa nje ya uwanja muda mrefu, kisha aliibukia Singida United 2020. Akiwa na Singida aliikuta timu hiyo ikiwa na ukata mkubwa wa fedha na yeye alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao waliikacha na kuondoka, lakini mpaka sasa hajulikani alipo.


MALIMI BUSUNGU

Mshambuliaji huyu mpaka sasa ni miaka minne hayupo kabisa kwenye soka la ushindani baada ya kuamua kukaa pembeni akiendelea na shughuli zake zingine huko Dodoma. Busungu ni miongoni mwa washambuliaji ambao walikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, lakini pia umakini wa kufunga mabao jambo lililowavutia Yanga na kuamua kumsajili 2015 akitokea Mgambo JKT.

Baada ya kutua Yanga na kuitosa Simba iliyokuwa ikimtaka pia, Busungu alionyesha kiwango kizuri lakini alijikuta akiingia matatani mara kwa mara na viongozi wa klabu yake kwa madai ya utovu wa nidhamu. Mwaka 2017 alijiunga na Lipuli ya Iringa, lakini nako hakudumu sana na msimu uliofuata akatimka zake na hajarejea kucheza soka la ushindani mpaka sasa.


SALUM MACHAKU

Machaku alitamba miaka ya nyuma akiwa na Mtibwa Sugar na kuwavutia mabosi wa Simba kumpa mkataba 2011, lakini akadumu na Wekundu wa Msimbazi kwa mwaka mmoja baada ya viongozi wa timu hiyo kuamua kuachana naye. Inaelezwa licha ya kufanya vizuri uwanjani alikuwa na matukio mengi nje ua uwanja yaliyosababisha viongozi wengi wa Simba kutaka atolewe kwa mkopo.

Machaku ambaye alikuwa anaitwa mara kwa mara katika kikosi cha Stars alijikuta akipotea polepole kwenye ramani ya soka la Tanzania licha ya kucheza mpaka timu ndogo ili arudi kwenye kiwango chake. Msimu wa 2018-2019 alijaribu kurejea kwa nguvu akiwa na Rhino Rangers ya Tabora, lakini akili ilionekana kutaka huku mwili ukigoma badala yake amepotea kabisa kwenye soka la ushindani.


OSCAR JOSHUA

Joshua alikuwa miongoni mwa mabeki bora wa kushoto katika kikosi cha Yanga na alidumu katika timu hiyo tangu 2011 alipojiunga nayo akitokea Ruvu Shooting hadi 2017. Beki huyo alikuwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza muda wote akiwa na Yanga, lakini yeye mwenyewe akaamua kukaa pembeni nje ya soka baada ya kuona inatosha alipomalizana na Yanga.

Ni takriban miaka mitano sasa tangu Joshua alipolipa kisogo soka la ushindani na kuendelea na maisha yake huku ikidaiwa kwamba kwa sasa ni mfanyabiashara.