Prime
Rafiki yetu Morrison anafurahia maisha nchi ya ahadi

Muktasari:
- Hata akifanya utovu wa nidhamu wanadamu wa nchi hii wanafurahia. Katikati ya wiki iliyopita aliitwa katika benchi na kocha wake, Omari Kapilima katika pambano kati ya KenGold anayoitumikia dhidi ya Simba pale Tabora. Morrison aligoma kutoka.
RAFIKI yetu Bernard Morrison yupo nchi ya ahadi hapa Tanzania. Anafurahia kila sekunde ya kuwa hapa. Aende wapi zaidi? Ameipata nchi ambayo watu wake wanaendana na tabia zake. Kila anachofanya wanadamu wa hapa wanakifurahia.
Hata akifanya utovu wa nidhamu wanadamu wa nchi hii wanafurahia. Katikati ya wiki iliyopita aliitwa katika benchi na kocha wake, Omari Kapilima katika pambano kati ya KenGold anayoitumikia dhidi ya Simba pale Tabora. Morrison aligoma kutoka.
Waliokuwa wanafuatilia pambano waliona kama kituko cha kufurahisha. Mtangazaji wa mechi kupitia Azam TV aliona kama kituko cha kufurahisha. Kwa mara nyingine tena Morrison akawa ametuonyesha tabia ya utovu wa nidhamu ambayo kwetu tuliichukulia kama kituko.
Kwa nini Morrison aligoma kutoka kumpisha mchezaji mwingine kama kocha alivyotaka? Ni kwa sababu kocha alikuwa Kapilima. Kocha Mtanzania. Kocha mweusi. Angekuwa mzungu unadhani Morrison angegoma? Thubutu.
Angekuwa anacheza AS FAR Rabat unadhani angegoma kutoka? Hapana. Alidharau tu kwa sababu kocha alikuwa Kapilima. Alidharau kwa sababu alijua alikuwa anatengeneza filamu nyingine ambayo Watanzania wangeipenda badala ya kuichukulia kuwa ni utovu wa nidhamu.
Ni kitu cha kawaida kwa mchezaji kuchukia kutolewa. Huwa imetokea mara nyingi. Anachoweza kufanya ni kwenda nje na kuonyesha kukasirika kwake.

Anaweza kupiga teke chupa za maji, lakini tayari ametoka. Anaweza kwenda nje na kumfokea kocha wake, lakini tayari ametoka.
Jose Mourinho aliwahi kumwingiza uwanjani Nemanja Matip akitokea katika benchi na ndani ya dakika mbili akamtoa kwa sababu hakufuata maelekezo yake.
Matip alitoka nje shingo upande. Kocha ni bosi. Ni wazi Nemanja alikuwa amechukia, lakini hakuna ambacho angeweza kufanya.
Mchezaji ambaye kiasi anaweza kugoma kutoka, tena kwa busara, ni yule ambaye ameumia uwanjani na benchi la ufundi linakata kumtoa nje, huku yeye mwenyewe akiamini ana uwezo wa kuendelea na mechi.

Anaweza kuyagomea kwa busara maamuzi ya benchi la ufundi, huku akiungana na daktari wake. Lakini hata katika hili bado kocha anaweza kusisitiza mchezaji atoke nje.
Hili alilotupa Morrison ni jipya, lakini sababu ni kama hiyo ambayo nimeisema. Na bahati nzuri vyombo vyetu vya habari hadi mitandao huwa vinafurahia vituko hivi na kuviweka katika kurasa za mbele bila ya kukemea.
Hapo ndipo Morrison anapojikuta yupo katika nchi ya ahadi. Nchi ambayo watu wake wanampenda na kumvumilia.
Hakuna kwingineko ambako angeweza kuishi kwa raha zaidi ya Tanzania. Labda ndiyo maana aliomba uraia.

Morrison akitafutwa na polisi raia wanafurahia wanaona ni kituko. Akitoroka katika kambi ya timu yake raia wanafurahia wanaona kituko.
Mwenyewe anajua namna ambavyo Watanzania wamempokea na ndiyo maana hii ni nchi yake ya ahadi.
Jaribu kuangalia mambo ambayo alifanya nchini, lakini bado aliporudi alipata timu. KenGold walimchukua akiwa na majeraha wakamlipa hela nzuri. Katika kundi la masela ambao walitakiwa kwenda kuikoa KenGold isishuke Morrison naye alikuwepo, lakini ndiye mchezaji ambaye hakuwa na mchango kuliko wengine. Kina Kelvin Yondani, Zawadi Mauya na wengine walau walijitahidi.
Hii ndiyo raha ambayo Morrison anaipata Tanzania. Na bado ataendelea kupata timu na bado ataendelea kufanya vituko. Kitu pekee ambacho alipotea maboya ni kuzichezea Simba na Yanga. Mjinga wakati wa kwenda na sio wakati wa kurudi.

Licha ya uchakaramu wake, lakini Morrison alipotea maboya wakati huu hizi timu mbili kubwa za Kariakoo zikiwa na ushindani mwingi ndani na nje ya Tanzania.
Aliondoka zake Yanga kwa vituko kwenda Simba. Ilikubalika kwa mazingira ya wakati ule.
Akaondoka zake Simba kwa vituko kurudi zake Yanga. Pale alipaswa kutulia vyema. Hata hivyo, alidhani Watanzania ni maboya alipoanza tena vituko vyake Yanga. Akaenda zake Ghana akakaa miezi mitatu bila ya kucheza mpira. Mwishoni mwa msimu Yanga wakaachana naye.
Wakati Yanga wanaachana naye, aliamini Simba ingeweza kumrudisha tena. Kumbe Simba ilikuwa imejiapiza haimtaki tena Morrison. Kilichofuatia ni Morrison kuwa na hasira na timu yake ya mwisho ambayo ilikuwa imemtupa. Yanga. Ndio maana anajinasibu yeye ni shabiki wa Simba.

Hakuamini baada ya Yanga kupambana kumrudisha ingeendelea kumvumilia kuwa naye, licha ya vituko vyake. Haishangazi kuona Morrison akiwa na jezi ya Simba akitazama mechi mbalimbali za Simba.
Kipaji? Kipaji anacho kikubwa. Kama angetulia vizuri asingekuwa shabiki wa Simba sasa hivi. Angekuwa uwanjani na jezi ya Simba au Yanga. Wenzake wenye vipaji vizuri kama vyake wamekula pesa ya nchi hii kwa muda mrefu.
Clatous Chama amekula pesa yetu kwa muda mrefu. Chama amekula zaidi ya bilioni mbili za Kitanzania ukiangalia kuanzia muda aliokuja nchini hadi sasa. Kuanzia ‘signing fee’ hadi mishahara yake. Emmanuel Okwi pia ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa aliyekula pesa nyingi nchini.
Mtazame Khalid Aucho. Umri umesogea, lakini anakula pesa ya Yanga kimya kimya tu kwa kuwa na nidhamu na kutuliza kichwa.
Wenzake ndivyo wanavyofanya. Yeye ameamua kuwa mchekeshaji zaidi lakini angeweza kutuliza kichwa na akala pesa yake vizuri tu.
Morrison ni mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji vikubwa waliowahi kufika nchini. Na amekuja katika nyakati ambazo mpira wetu una pesa nyingi huku vipaji vya kina Edibily Lunyamila vikiwa vimetoweka.
Angetuliza kiwango kidogo tu nadhani angeweza kuwa milionea katika nchi hii.