SI MCHEZO: Timu zimeshuka, wao wanabaki Ligi Kuu

Muktasari:
- Timu hizo mbili ni KenGold ya Mbeya ikiongozana na wenzao Kagera Sugar ambao rasmi zitacheza Ligi ya Championship kwa msimu ujao.
Timu hizo mbili ni KenGold ya Mbeya ikiongozana na wenzao Kagera Sugar ambao rasmi zitacheza Ligi ya Championship kwa msimu ujao.
Msemo wa timu ndiyo inashuka ila mchezaji hashuki zimejidhihirisha kwani kuna mastaa wa vikosi hivyo licha ya klabu zao kuteremka lakini wao wamekuwa gumzo sokoni wakiwa na ofa mbalimbali.
Hili sio geni kwani miaka ya nyuma limetokea sana kwa timu kushuka lakini wachezaji wake kuendelea kupiganiwa na klabu zingine akiwemo mshambuliaji Waziri Junior ambaye timu ya Mbao iliteremka ila yeye akatua klabu kubwa ya Yanga.

PETER LWASA (KAGERA SUGAR)
Ni kiungo mshambuliaji wa Kagera Sugar na msimu wake wa kwanza amefanya kazi kubwa iliyompambanua juu ya ubora wake akimaliza kinara wa ufungaji katika kikosi hicho na mabao nane.
Raia huyu wa Uganda amebakiza mwaka mmoja katika timu hiyo lakini hadi sasa haionekani kama atashuka na timu hiyo akiwa na ofa mbalimbali kutoka Dodoma Jiji, Fountain Gate na Azam FC.

SELEMAN BWENZI (KENGOLD)
Jina lake halisi ni Seleman Rashid ‘Bwenzi’ Kiungo mshambuliaji wa KenGold, ambaye ameichezea timu hiyo nusu msimu tu, lakini akaonyesha kiwango kikubwa akimaliza kinara wa ufungaji kwa timu hiyo iliyoshuka akiwa na mabao matano.
Bwenzi mapema tu ameshalamba dili zuri akisajiliwa na Mashujaa hata kabla ya msimu kumalizika na hapohapo akakaa zake pembeni akiiacha timu yake ikipambana kumaliza mechi za mwisho na kabla ya hapo alikuwa na ofa nyingi za Coastal Union, Tabora United na JKT Tanzania.
RAMADHAN CHALAMANDA (KAGERA SUGAR)
Kipa huyu wa Kagera Sugar ambaye licha ya timu yake kushuka alikuwa na kiwango bora golini akishika nafasi ya tatu kwa makipa waliookoa mashambulizi akifanya hivyo mara 57.
Chalamanda anamaliza mkataba alionao na Kagera Sugar akiwaniwa na Mbeya City, Pamba na JKT inayohofia kipa wake namba moja Yakoub Seleman anaweza kutimka.
HEBERT LUKINDO (KENGOLD)
Ni kiungo mshambuliaji wa KenGold na kwenye mzunguko wa kwanza alikuwa na moto kabla ya usajili wa dirisha dogo uliofanywa na timu yake kufifisha nafasi yake.
Lukindo ana uzoefu mkubwa kwenye ligi, msimu huu amefunga mabao manne tu lakini kiwango chake kinajulikana ambapo Stand United inayovizia kupanda ligi imesharusha ndoano kwake pamoja na Tabora United sio rahisi kushuka na timu yake.
CLEOFAS MKANDALA (KAGERA SUGAR)
Ni kiungo mshambuliaji wa Kagera Sugar, alisajiliwa na timu hiyo akitokea Azam FC, msimu huu alikuwa kwenye kiwango cha kawaida akifunga mabao mawili pekee.
Mkandala ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na Mashujaa, JKT Tanzania Prisons na hata Dodoma Jiji zinapiga hesabu ya kumzuia asishuke na timu yake.

OBREY CHIRWA (KENGOLD)
Raia wa Zambia, ni mshambuliaji mwenye nguvu na akili ya kufunga, amekwenda na kuishusha KenGold ingawa ubora wake unajulikana.
Msimu huu Chirwa amefunga mabao mawili pekee ndani ya nusu msimu, lakini licha ya uchache wa mabao hayo bado anapigiwa hesabu na klabu mbalimbali zikiwemo Mbeya City na Stand ambayo inasubiri hatma yake kupanda.
HIJA SHAMTE (KAGERA SUGAR)
Ni kinda anayeichezea mpaka timu ya taifa na amemaliza msimu akiwa na Kagera Sugar, msimu huu amefunga bao moja pekee lakini kiwango chake na umri bado vimembeba.
Kagera Sugar itathibitishja kinda huyo anatakiwa kwenda kufanya majaribio England na Norway ambako amepata mwaliko kupitia uwezo anaouonyesha katika klabu yake na timu za taifa za vijana.

MISHAMO DAUDI (KENGOLD)
Mshambuliaji wa KenGold alipanda na tilmu hiyo na sasa ameshuka nayo, akiwa amefunga mabao matatu pekee lakini bado kuna kitu kimeonekana kwa timu zingine.
Mshamo anawinda na Namungo ya Lindi na Mbeya City zikiona kuna kitu kwenye kipaji chake zikipigana vikumbo kumuwania.