Dabi za Camara, Diarra kitawaka Machi 8

Muktasari:
- Camara amedaka mechi 20 akiwa hajaruhusu bao (clean sheet) katika mechi 15, lakini akiruhusu mabao katika michezo tano dhidi ya Coastal Union pale Wekundu wa Msimbazi walipotoka sare ya mabao 2-2
KATI ya maeneo yatakayokuwa magumu kwenye mechi ya Machi 8, 2025 ya Dabi ya Kariakoo ni la makipa kutokana na Djigui Diarra wa Yanga na Moussa Camara anayeidakia Simba kuonyesha viwango vya juu katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu Bara.
Camara amedaka mechi 20 akiwa hajaruhusu bao (clean sheet) katika mechi 15, lakini akiruhusu mabao katika michezo tano dhidi ya Coastal Union pale Wekundu wa Msimbazi walipotoka sare ya mabao 2-2; dhidi ya Yanga walipofungwa bao 1-0, Fountain Gate (bao 1-1), dhidi ya Azam (mabao 2-2) na dhidi ya Kagera Sugar ambapo Simba ilishinda kwa mabao 5-2 mchezo huo uliopigwa Desemba 21,2024, hivyo kacheza dakika 1,800 akifungwa mara nane.
Kukosekana kwa Camara dhidi ya Coastal Union ambapo alidaka Ally Salim mchezo huo Mnyama alishinda kwa mabao 3-0 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Machi Mosi,2025.

Kwa upande wa Diarra kacheza mechi 16 akiwa na clean sheets 11, kafungwa mabao saba akicheza dakika 1451 na miongoni mwa michezo aliyoruhusu mabao ni dhidi ya KenGold pale Yanga iliposhinda 6-1 ambapo alifungwa bao la mbali na Suleman Bwenzi, dhidi ya Tabora United walipofungwa mabao 3-1; dhidi ya KMC kwenye ushindi wa 6-1, Azam walipofungwa 1-0 na Singida Black Stars waliposhinda 2-1.
Hata hivyo, katika mchezo wa keshokuwa nani anaweza akaibuka shujaa kwa kuisaidia timu yake, Mwanaspoti linakuletea dabi walizocheza na kilichoelezwa na makocha wa makipa wakitaja ubora na udhaifu ambao washambuliaji wanaweza kuutumia kuwafunga makipa hao.
DABI ZA DIARRA
Diarra ni mzoefu zaidi ya Camara tangu ajiunge na Yanga 2021 akianza kucheza mechi ya dabi ya Aprili 30, 2022 (0-0) lakini katika mzunguko wa kwanza Julai 3,2021 alidaka Farouk Shikhalo ambapo dakika 90 zilimalizika kwa Simba 0-1 Yanga.

Mechi nyingine alizodaka Diarra za dabi katika Ligi Kuu ni Oktoba 23, 2022 (Yanga 1-1 Simba), Aprili 16, 2023 (Simba 2-0 Yanga), Novemba 5, 2023 (Simba 1-5 Yanga) na Oktoba 19, 2024 (Simba 0-1 Yanga).
DABI ZA CAMARA
Camara alianza na dabi ya Oktoba 19,2024 Simba ilipofungwa bao 1-0 akiokoa hatari nyingi katika mchezo huo, na endapo akipangwa kucheza Machi 8 itakuwa mechi yake ya pili ya dabi katika Ligi Kuu Bara.
MAKOCHA WA MAKIPA
Akiwazungumzia makipa hao wa Simba na Yanga, kipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi 'Father' anasema licha ya ubora wa Camara na Diarra washambuliaji wakigundua udhaifu wanafungika katika mechi hiyo, ingawa alikiri haitabiriki.
"Mfano bao alilofungwa Diarra na Suleiman Bwenzi wa KenGold alimwangalia akaona ameshatoka katika 'zone namba sita', akapiga shuti, kosa alilofanya Diarra ni kurudi kinyumenyume badala ya kurudi upandeupande angeweza kuupangulia mpira nje," anasema Father.
"Vivyo hivyo kwa Camara aliyofungwa dhidi ya Coastal Union alikuwa nje ya eneo lake, bao lingine alilofungwa na Ladack Chasambi wakati wanacheza dhidi ya Fountain Gate - mwelekeo wa mpira alipaswa aokoe na mguu wa kushoto yeye akatumia kulia akakuta anajifunga. Udhaifu kama huo wapinzani wakiujua ni rahisi kufungwa."
Aliyekuwa kocha wa makipa wa Yanga, Peter Manyika Sr anasema makipa wote wawili wakianza katika mechi hiyo anaamini watazisaidia timu zao kuwa imara, ingawa anawaona wanajiamini kupita kiasi jambo ambalo washambuliaji wanaweza kulitumia kuwafunga.

"Sina maana kujiamini kwao ni kubaya, ila kitendo cha kutoka eneo lao. Kuna washambuliaji ambao wana uwezo wa kufunga mabao ya mbali na wamefungwa mabao ya aina hiyo. Wote ni wepesi wa kuona hatari za mbali na wanaweza wakazipangua. Alichozidi Diarra ni kucheza dabi nyingi na ana uwezo wa kuanzisha mashambulizi," anasema kocha huyo.
Kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Ivo Mapunda anasema Camara na Diarra kila mmoja ana ubora na udhaifu wake, ilhali kuhusu dabi atakayekuwa makini ndiye anaweza kuibuka shujaa kuisaidia timu yake.
"Ingawa Diarra kadaka mechi nyingi za dabi, ila siyo kitu kinachoweza kikafanya Camara akashindwa kufanya vizuri," Anasema.