COSMAS CHEKA: Tunauza sana mapambano nje

Muktasari:
- Cosmas ni mdogo wa bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka ‘SMG’ ambaye amekuwa na rekodi kubwa kimataifa zaidi ya kaka yake lakini hatajwi.
KAMA siyo kupenda mchezo wa ngumi za kulipwa basi huenda bondia Cosmas Cheka naye angewika kwenye soka kama maswahiba zake Jonas Mkude na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wanaokipiga Yanga SC.
Cosmas ni mdogo wa bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka ‘SMG’ ambaye amekuwa na rekodi kubwa kimataifa zaidi ya kaka yake lakini hatajwi.
Bondia huyo ana rekodi ya kushinda mapambano manne nje ya Tanzania ikiwemo ubingwa wa WBO Asia Pasific nchini Thailand ambayo haijafikiwa na kaka yake ambaye amekuwa chachu ya yeye kuingia kwenye mchezo huo licha ya akili na malengo yake awali yalikuwa katika soka kutokana na uwepo wa maswahiba zake ambao ni mastaa wakubwa kwenye soka.
Cosmas amecheza jumla ya mapambano 58, kashinda 29, kati ya hayo saba kwa KO na amepigwa 21, tisa yakiwa ni KO huku akitoka sare nane.
Licha ya mara kadhaa wadau wengi wa ngumi kudai amekuwa akitembelea nyota ya kaka yake, lakini mwenyewe amekuwa akiwafumba mdomo kutokana na rekodi ya kuwa miongoni mwa mabondia wachache walioshinda mapambano nje ya mipaka ya Tanzania.
Jina lake limebaki katika vitabu vya kumbukumbu Thailand baada ya mwaka 2015 kushinda ubingwa wa WBO Asia Pasific kwa kumchapa kwa TKO, Aphinan Rengron pambano lililopigwa kwenye Kituo cha Maduka ya Westgate, Thailand.
Mwaka 2017 katika viwanja vya Carnivore, Nairobi, Kenya, Cheka alimtandika Mkenya, David Rajuili kwa TKO ya raundi ya nane katika pambano la raundi 10.
Desemba 2017, alirejea tena Kenya katika viwanja hivyo, safari hii alimteketeza kwa pointi Kenneth Kidega katika pambano la raundi nane.
Utawala wa Cosmas Kenya ulikuwa mkubwa kabla ya kutoa kipigo cha mwisho mwaka 2018 kwa Geoffrey Nyamu na alimchapa kwa pointi katika pambano la raundi sita lililopigwa katika Viwanja vya Kibera Kamuļunji, Nairobi.
Bondia huyo amekiri na kukubali mchango wa kaka yake kwake kwenye mchezo huo huku akipinga suala la yeye kubebwa na jina la Cheka kwani rekodi zao hazifanani.
“Ninakubali Francis Cheka ni kaka yangu na yeye amekuwa na mchango mkubwa sana kwangu kwenye ngumi, lakini suala la kubebwa na jina lake siyo kweli.
“Ukiangalia rekodi yangu na yake ni tofauti, mimi nimeshinda mapambano mengi nje ya nchi, lakini kaka hajawahi kushinda nje ya Tanzania pambano lolote, inawezaje kuwa sawa?” alihoji.
“Siku zote ulingoni napanda peke yangu, watu wanatakiwa waelewe hilo na hayo unayosema kila ninapokwenda huwa nakutana nayo, sipewi heshima yangu ila maneno hayo hayawezi kunivunja nguvu kwa sababu nimezoea.”
Washkaji zako ni Mkude na Sure Boy wanacheza soka wewe umekimbilia ngumi ilikuwaje?
“Mungu huwa anampa kila mtu riziki yake, Sure Boy na Mkude ni marafiki zangu sana kwa sababu tumecheza wote ila Mungu ameniwekea riziki yangu kwenye mchezo huu. Hata kama ningecheza soka huenda nisingepata mafanikio haya kwa kuwa sijaandikiwa kupata huko.”
“Kikubwa nashukuru Mungu, wamekuwa wakinipa sapoti na mambo ambayo Mungu amekuwa akimwandikia kila binadamu katika utafutaji wake wa riziki.”
Umewahi kucheza nao soka?
“Siyo mara moja, Mkude nimecheza naye sana mechi za shule lakini Sure Boy katika mechi za mtaani, hivyo ni vitu vya kawaida kwa watu ambao tumekua wote katika maisha.”
Kati yao hakuna aliyekwambia anataka kuwa bondia?
“Unajua mara nyingi Sure Boy ndiye amekuwa akinitania sana juu ya yeye kutaka kuja kuwa bondia ingawa na Mkude naye alishawahi kusema, yupo pia Mussa Nampaka ‘Chibwabwa’ (kiungo wa zamani wa Lipuli, Mtibwa Sugar, Ashanti na Mwadui) lakini ni vizuri wakajifunza kwa ajili ya ulinzi binafsi.”
Kaka yako hajawahi kushinda nje ya Tanzania, unadhani ni kwa nini?
“Kitu pekee ninachoweza kukwambia, kushinda nje ya Tanzania hasa Ulaya si kwa uwezo wako zaidi ya bahati na hakuna bondia aliyeenda nje akarejea na ushindi ule wa kusema naenda kushinda isipokuwa huwa inatokea, sasa yeye hakupata hiyo bahati.”
Hata wewe ule ushindi wa mapambano yako ni bahati?
“Hilo ndiyo jibu, isipokuwa mimi ndiye bondia niliyepata bahati ya kushinda mechi nyingi mfululizo nje ya Tanzania, nimeshinda Ufaransa, nikashinda Thailand na Kenya.”
Ngumi peke yake imekupa maisha au shule imechangia?
“Kwanza nashukuru Mungu, ukiondoa diploma ya uhasibu ambayo nipo nayo, pia nina elimu ya cheti upande wa ‘Hotel Management’ na niliwahi kufanya kazi Nashera Hotel Morogoro.”
“Shule inanisadia na ngumi imenipa mafanikio kwa sababu kama ngumi hakuna, basi narejea kufanya kazi nyingine za kuajiriwa ingawa ngumi ndiyo imenifanya nimekuwa Cosmas Cheka.”
Ulishawahi kupigwa ngumi ukatamani kuacha kabisa mchezo huo?
“Nakumbuka haikuwa kuacha ngumi lakini nakumbuka wakati nakaribishwa kwenye ngumi za kulipwa kuna bondia anaitwa Yohana Robert nilimpiga sana ila raundi ya mwisho zilibaki sekunde tu pambano kuisha, alinipiga ngumi kali nikapepesuka ulingoni kutoka kona moja hadi nyingine na pambano likamalizwa kwa sare.”
Tatizo gani la Cheka lilikupa wakati mgumu?
“Kiukweli lile tukio la ajali ya moto wa Morogoro (ilitokea Agosti 2019) iliyosababishwa na lori la mafuta, iliniumiza kwa sababu watu walimzushia kifo kwa sababu ajali ilitokea karibu na sehemu yake ya biashara ya makopo.”
“Lakini kitu ambacho hawakijui ni wakati tukio linatokea Cheka tayari alikuwa Msumbiji ila kwa kuwa walikuwa hawamuoni wakaamua kumzushia ameungua kwenye ile ajali.”
Hivi ni kweli mabondia wakienda nje wanauza mapamano?
“Kitu cha kwanza watu wanatakiwa kuelewa ngumi za kulipwa ni biashara binafsi ndiyo maana zikaitwa ngumi za kulipwa, ulipwe halafu ndiyo upigane.”
“Suala mabondia kuuza mapambano linatokana na mazingira hasa sisi tunaotokea Afrika, unakuta pambano labda mkataba unalipwa Dola 2000 halafu mpinzani wako anakufuata na Dola 3000 ili umuachie ashinde, sasa wewe unaweza kuacha Dola 3000 ambayo ukichanganya na malipo halali unakuwa na Dola 5000.
“Lakini mara zote hata kama hawajakununua kushinda nje siyo kazi nyepesi, ndiyo maana nikasema kushinda nje mara zote ni bahati, siyo rahisi mtu akulipie hoteli, chakula, ndege na malipo yake halafu ukampige bondia wao ndiyo maana wakati mwingine wanafanya umafia kabisa ili wapate rekodi yako.
“Nakumbuka wakati fulani mimi nilienda nje siwezi kuitaja nchi sasa baada ya kufika kule siku moja kabla ya pambano, usiku mpinzani wangu alikuwa anahangaika kunitafuta na yule mtu niliyefuatana naye alienda kutembea na wenyeji wake.
“Sasa yule mpinzani wangu akanifuata kwenye upande ambao ulikuwa chumba changu, alipokuja akawa ananiomba nimuachie ashinde ili anipe kiasi cha Dola kadhaa, ukweli nilimwambia akaongeze, jamaa kweli akaongeza nikaona pesa yangu itakuwa ya kutosha kumalizia mambo yangu.
“Lakini siku ya pambano nilimkazia hadi watu wake wakaenda kumuuliza mtu niliyekwenda naye kwa nini siachii wakati walinipa pesa, nilipoulizwa nilikataa kabla ya kupigwa raundi ya saba,” anasema Cheka.