Bruno: Visa vya kusisimua vilivyomleta kwenye ndondi

Muktasari:

  • Bruno akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia duni ya hali ya chini ya Melkiory Tarimo ambaye alilazimika kutoendelea na elimu ya sekondari baada ya kumaliza elimu ya msingi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ya familia.

"HAIKUWA rahisi kufika hapa ni nguvu zake, isingekuwa rahisi kufika hapa ila ni mkono wake." Ni nukuu ya mistari wa wimbo wa injili kutoka kwa Obby Alpha, sawa kabisa na maisha ya kijana kutoka Rombo mkoani Kilimanjaro, Bruno Tarimo 'Vifuaviwili' kwamba haikuwa rahisi kwake kuweza kuishi Australia pamoja na familia yake.

Bruno akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia duni ya hali ya chini ya Melkiory Tarimo ambaye alilazimika kutoendelea na elimu ya sekondari baada ya kumaliza elimu ya msingi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ya familia.

Hali hiyo ilimfanya bondia huyo kuingia mtaani na kufanya shughuli mbalimbali za kumpatia kipato kwa ajili ya ndugu zake wengine wawili wa familia moja kuishi kabla kuingia jijini Dar es Salaam.

Tarimo ambaye kwa sasa ni bondia wa ngumi za kulipwa nchini Australia akiwa anashikilia rekodi ya ubingwa wa kimataifa wa Shirikisho la Ngumi Duniani (IBF) na ubingwa wa muda wa dunia wa upande wa Ocenia wa WBA kwenye uzani wa superfeather, alihamia Dar es Salaam kuja kuuza duka.

Lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda bondia huyo aliona kazi hiyo ni ngumu kwake jijini humo, akapata kibarua cha kazi hiyo Bagamoyo mkoani Pwani ambako hata hivyo alikimbilia kwenye shughuli za uendeshaji wa pikipiki maarufu kama Bodaboda.

Wakati akiendelea na shughuli hiyo tayari alikuwa akiishi na mwenza, hivyo suala la kipato kupitia bodaboda ikawa changamoto na ikabidi ajiingize katika masuala ya ufundi ujenzi ili kupata fedha za kuendesha maisha.

Bondia huyo anayefahamika zaidi nchini kwa majina ya 'Vifuaviwili', lakini Wazungu wakimuita Terminator anashikilia rekodi ya kucheza mapambano 34 huku akifanikiwa kushinda 28 kati ya hayo saba akipata ushindi wa Knockout (KO), amepigika mara nne na moja ikiwa ni KO ilhali ametoka sare mara mbili.

Nyota ya bondia huyo iliwaka mara ya kwanza 2018 baada kufanikiwa kushinda mkanda wa ubingwa wa WBA Oceania kwa kumchapa kwa pointi Billel Dib ‘Baby Face’, raia wa Australia likiwa pambano lake la kwanza nje ya mipaka ya Tanzania.

Mkanda wa ubingwa huo ndiyo ulimfungulia milango bondia hiyo nchini humo, kwani alifanikiwa kupata mkataba wa pambano la marudiano na wa kuishi kwa miaka minne.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na bondia huyo ambaye kwa sasa anaishi kwenye mji wa Southport sambamba na familia  aliyoitoa Tanzania.

Bondia huyo anaanza kwa kujibu swali aliloulizwa kuwa ni kitu gani kilimfanya awe bondia wa ngumi za kulipwa.

JIBU: "Binafsi sijui ni kitu gani ambacho kimenifanya niwe bondia kwa sababu kwenye familia yetu hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kuwa bondia. Nahisi ni umasikini ndiyo umenipelekea kuwa hivyo.

SWALI: Kabla ya kuwa bondia uliwahi kuwa mjenzi na muuza duka?

JIBU: "Unajua kabla ya kuwa bondia nimepitia changamoto nyingi hadi nakuja kujipata kwenye ngumi haikuwa rahisi, maana niliamua kuondoka nyumbani Rombo kwenda kutafuta (pesa) kutokana hali ya kimaisha haikuwa nzuri hata shule sikuweza kuendelea nayo.

"Ni'shapigwa sana ngumi za kichwa sikumbuki vizuri, ila niliondoka nikiwa na umri mdogo kwa sababu kwetu sisi tupo watoto wa tatu na wote wa kiume ila mimi ndiyo nilikua mkubwa hivyo nimeuza duka, nimekuwa dereva bodaboda pamoja na kazi za ujenzi nimefanya sana."


SWALI: Ni nadra sana kwa Wachaga kuwa bize na mambo ya michezo kwa nini kwako iliwezekana?

JIBU: "Ni kweli asilimia kubwa ya Wachaga hawapo bize na mambo ya michezo, wengi wanawaza biashara na kumiliki magari ila kwa upande wangu sikuwa na chaguo kwa sababu elimu yangu ilikuwa duni.

"Lakini katika biashara zile nafasi za kuajiriwa nilizokuwa napata zilikuwa finyu kwangu na siku hizi mambo yanakwenda kwa kujuana halafu nilikuwa naonekana mdogo na huu ufupi wangu ndiyo kabisa ulikuwa tatizo.

"Ninachoshukuru ni kwamba tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda mazoezi na baba yangu alikuwa akinifanyisha mazoezi ingawa hakuna ambaye aliwaza wala kutambua kama ipo siku nitakuja kuwa bondia.

"Lakini nilivyofika Bagamoyo ndiyo nikakutana na watu ambao wakaniambia naweza kuingia kwenye ngumi na nitapata pesa kutokana na asili yangu ya kupenda mazoezi ndiyo nikajiunga na Sharif Boxing Gym ya Bagamoyo.

"Pia haikuwa rahisi kwa sababu wakati huo tayari kulikuwa na mabondia wakubwa kama Francis Cheka, Thomas Mashali na Mohamed Matumla na mimi nilikuwa nimeweka mitego yaani mazoezi nafanya, bodaboda naendesha na kazi za ujenzi nafanya sikuwahi kujua natokea wapi.

"Nakumbuka nilikuwa nagombana na mke wangu juu ya mambo ya ngumi kwa sababu hakuna nilichokuwa napata yeye akawa nataka niendelee na kazi za ujenzi, lakini nilichokuwa nalipwa kilikuwa kinaishia jikoni na wala hakikuwa kinaongezeka."

SWALI: Ni kweli njaa ndiyo imesababisha uwe ulipo sasa?

JIBU: "Naweza kusema ni njaa kwa sababu umasikini wa familia umechangia pakubwa kufikia hapa na sina uhakika kama familia ingekuwa vizuri kama ningekuwa hapa, labda huenda ningekuwa nimeridhika japokuwa Mungu ndiyo anajua.


SWALI: Pambano lako na Tony Rashid liliishia wapi?

JIBU: "Kweli nilikuwa na pambano dhidi ya Tony Rashid na lingekuwa moja kati ya mapambano bora kuwahi kutokea, wengi wanamjua Bruno, lakini hawajawahi kumuona anavyopigana.

"Halafu wakati bado Tanzania ngumi hazikuwa zimekuwa kama zilivyo sasa kwa maana wadhamini kuwa wengi hata migogoro ilichangia kabla ya Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kufanya mabadiliko makubwa.

"Lakini nikuhakikishie kwamba kama lingetokea au litakuja kutokea, basi sina uhakika kama kuna bondia mzawa wa Tanzania katika kilo zangu anaweza kufikia uzoefu wangu."

SWALI: Kuna bondia Mtanzania aliwahi kukusema hadharani baada ya kupigwa na Zelfa Barret, lakini yeye akapigwa Technical Knockout Uingereza unadhani kwa nini alikusema?

JIBU: "Ni kweli kuna bondia alinisema baada ya kupigwa pambano langu la Uingereza dhidi ya Zelfa Barret, ila huo ulikuwa ni mtazamo wake, huwa sifikirii chochote nikishapoteza pambano kwa sababu najua siku zote kwenye ngumi kuna matokeo matatu kushinda, kupigwa na sare.

"Binafsi nilikubali kwamba mpinzani wangu alinizidi vitu vingi ikiwemo urefu, halafu sikuenda pale kwa ajili ya pesa ila ndoto yangu ilikuwa ni kufika mbali maana siku zote napigana kwa ajili ya familia yangu.

"Lakini kabla ya kauli ile aliyosema kwamba fursa ile kama angeipata basi watu wangekuwa wanasimulia mambo mengine baada ya pale, ukweli ilinichosha maana kabla ya pale mimi na yeye tulikuwa tukiwasiliana sana sijui aliwaza nini.

"Upande mwingine nilimpuuza kwa kushindwa kuelewa mchezo wa ngumi hata alivyopata nafasi ya mara pili kwenda Uingereza na alivyopoteza akatoa sababu ya kiatu, nilisema kwamba unapata nafasi hakikisha unaitumia vyema ili kuweka heshima kwenye mchezo hata mara ya kwanza aliweka hicho kitu. Naheshimu mchango wake."

SWALI:Umekaa mbali na familia yako kwa miaka mingapi?

JIBU: "Nimekaa mbali na familia yangu kwa takribani miaka mitano na nusu na kitu ambacho kimesababisha familia yangu kuwa  Australia ni mimi mwenyewe kwa sababu ndiyo nilioteseka nao, sasa haikuwa sawa kukubali kuwa mbali nao.

"Nakumbuka hata awali nilizuiwa na watu walionileta (Australia) nisiorodheshe familia, lakini niliweka ingawa niliambiwa nionyeshe juhudi ya kuishawishi serikali ya Australia kwamba wanastahili kuja nilipo, ndiyo vile nikashika nafasi ya nne duniani kwenye mabingwa wa IBF, lakini kufuata masharti yote ambayo nilipewa ikiwemo la kutofanya kazi."


SWALI: Kazi ya kufundisha watu mazoezi kwa saa ulikuwa unalipwa kiasi gani na wanafunzi wangapi?

JIBU: "Huku mimi siyo mwalimu wa ngumi, bali bado ni bondia isipokuwa kuna changamoto zilitokea baina yangu na menejimenti yangu ya zamani, ila sasa nipo na menejimenti nyingine ndiyo sababu ya ukimya wa miaka miwili, ila hivi karibuni mtasikia kuna jambo kubwa litafanyika.

"Suala hilo la kufundisha ni wale watu wangu wa karibu kama mdhamini ananiomba nimfundishe mazoezi mtoto wake ambaye kwa saa ananilipa Dola 200 na washkaji zangu wa gym  huwa wananipa Dola 50 kila mmoja, ila siyo kwamba nimekuwa mwalimu."


SWALI: Kitu gani ambacho huwezi kukisahau kwenye ngumi?

JIBU: "Safari ya pili nilivyokuja Australia kupigana baada ya pambano 'matchmaker' niliyekuja naye namhifadhi kwa jina kidogo. Tulivyorudi hotelini aliniambia nipakie vitu kwamba tunarudi Tanzania nikamuuliza narudi vipi Tanzania ikiwa tumeshasaini mkataba wa kuishi hapa miaka minne. Kiukweli nililia sana na siwezi kusahau.

"Halafu wakati huo Serikali ya Tanzania, waandishi wa habari walikuwa wakijua kwamba Bruno amesaini mkataba wa kuishi Australia na familia yake halafu jamaa ananiambia nirejee Tanzania, niende moja kwa moja nikashukie Moshi, nikiulizwa niseme matatizo ya viza. Nakumbuka nilimwambia nitakuchoma kisu, tuishie hapo ila nililia sana."

SWALI: Ni kweli umeshabadilisha uraia?

JIBU: "Hapana, binafsi bado ni Mtanzania na naendelea kutumia hati ya kusafiria ya Tanzania. Hili nimekuwa nikilisema mara kwa mara kwamba sijabadilisha uraia."

SWALI: Familia yako kwa maana ya mke na watoto wapo huko kwa muda au ndiyo wameshahamia?

JIBU "Familia yangu kifupi kwa sasa huku wamehamia moja kwa moja. Niliwafuata mwenyewe na wamekamilisha kila kitu na watoto wameshaandikishwa kwenye shule za serikali hapa, wasoma."


SWALI: Chakula gani wewe na watoto wako mnakikukumbuka?

JIBU: "Chakula ambacho nakikumbuka baada ya kuwa naishi huku ni ndizi na ugali wa dagaa, maana kama ugali wa dagaa wenzetu huku wanaziona zinanuka sana. Ukipika watu wanaona sijui kama umepika kitu gani."